Saturday 12 December 2015

Jeshi Stars wajitoa mashindano ya netiboli ya Muungano yanayoanza Zanzibar Jumanne 2015



Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania Chaneta), Annie Kibira wakati wa mkutano mkuu wa TOC leo katika Kituo cha Amani Welezo, Zanzibar.
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
TIMU ya Jeshi Stars imejitoa kushiriki mashindano ya netiboli ya Muungano yanayotarajia kuanza Jumanne Desemba 15 kwenye Uwanja wa Gymkhana mjini Zanzibar.

Jeshi Stars ni miongoni mwa timu za Tanzania Bara zilizothibitisha kushiriki mashindano hayo kabla ya kujitoa katika dakika za mwisho kabisa za mashindano hayo.

Timu zingine za Bara zitakazoshiriki mashindano hayo ni pamoja na mabingwa Uhamiaji, JKT Mbweni, Polisi, Tumbaku ya Morogoro, Mbeya City ya Mbeya.

Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania Chaneta), Annie Kibira alisema jana mjini hapa, ambako anahudhuria mkutano mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) kuwa, alipewa taarifa juzi kuwa Jeshi Stars wamejitoa katika mashindano hayo.

Alisema kuwa anasubiri barua yao ili kujua sababu kamili iliyopelekea kujiondoa katika dakika za mwisho katika mashindano hayo.

Hatahivyo, taarifa zingine zinasema kuwa, timu hiyo imejiondoa baada ya baadhi ya wachezaji wake kwenda katika kozi ya kikazi.

Timu za Zanzibar zitakazoshiriki mashindano hayo ni JKU, Mafunzo, KBZ, Zimamoto, Chake Stars na Wete Stars.

Wakati huohuo, timu za Uhamiaji na JKT Mbweni zinatarajia kutua leo mjini hapa kwa ajili ya mashindano hayo.

No comments:

Post a Comment