Monday 28 December 2015

Mohamed Elneny: Arsenal yafanya mazungumzo kutaka kumsajili kiungo huyo wa Basel



LONDON, England
KLABU ya Arsenal iko katika mazungumzo na FC Basel kuhusu kumsajili kiungo wa kati Mohamed Elneny (pichani).

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Misri mwenye umri wa miaka 23 alijiunga na klabu hiyo yenye maskani yake Uswisi mwaka 2013 na ametwaa mataji ya ligi katika kila msimu alioichezea timu hiyo.

Kiasi cha ada kilichoelezwa ni kama pauni milioni 5 na Elneny anahitaji kibali cha kufanyia kazi ili kuichezea timu hiyo.

Mchezajji huyo ruksa kuichezea Arsenal katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya baada ya Basel kushindwa kufuzu mwaka huu katika hatua ya makundi.

Elneny alikuwemo katika kikosi cha Basel kilichoibuka na ushindi dhidi ya Chelsea katika mashindano ya msimu wa mwaka 2013-14.

Kocha wa Arsenal Arsene Wenger yuko mbioni kuimarisha kikosi chake hasa katika nafasi ya kiungo wa kati baada ya Francis Coquelin na Santi Cazorla kupata majeraha makubwa, huku Aaron Ramsey na Mikel Arteta nao pia wako nje ya uwanja na Jack Wilshere bado hajarejea uwanjani.

Hatahivyo, Elneny anaonekana kama sehemu ya mpango ya muda mrefu wa Wenger na sio kuziba pengo, wakati atakapojiunga na klabu hiyo yenye maskani yake kaskazini ya London.

Wilshere atakuwa nje ya uwanja angalau hadi mwezi Februari.
Kocha huyo wa the Gunners alikiri kuwa, hana uhakika kama Wilshere atarejea haraka uwanjani, lakini sio kabla ya Februari.

Kiungo huyo wa England alitarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa angalau miezi mitatu baada ya kufanyiwa upasuaji Septemba baada ya kuumia katika mguu wa kulia, lakini makadilio hayo yameongezeka.

"Nilisema Februari lakini ukweli sina uhakika, alisema Wenger wakati timu yake ilipochezea kichapo cha mabao 4-0 katika Ligi Kuu ya England kutoka kwa Southampton huku leo Jumatatu timu hiyo ikitarajiwa kuwa mwenyeji wa Bournemouth.

No comments:

Post a Comment