Thursday, 10 December 2015

RISALA YA KATIBU MKUU (TOC) KWENYE UFUNGUZI WA KAMISHENI YA WANAMICHEZO ZANZIBAR TAREHE 10/12/2015.Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kamisheni ya Wachezaji ya Kamati ya Olimpiki Tanzania (Kawata) leo Zanzibar. Kushoto ni mwenyekiti wa Kawata, Ramadhan Zimbwe. Kushoto kwa Bayi ni Katibu Msaidizi wa TOC Jamal Adi na rais wa Toc Gulam Rashid.

 TANZANIA OLYMPIC COMMITTEE (TOC)
KAMATI YA OLIMPIKI TANZANIA

RISALA YA KATIBU MKUU (TOC), FILBERT BAYI KWENYE UFUNGUZI WA KAMISHENI YA WANAMICHEZO ZANZIBAR TAREHE 10/12/2015.

Ndugu Mgeni Rasmi Jamal Adi, Katibu Mkuu Msaidizi TOC

Ndugu Gulam Rashid, Rais wa TOC,

Ndugu Ramadhani Zimbwe, Mwenyekiti, KAWATA Taifa,

Ndugu Amina Ahmed, Katibu KAWATA Taifa

Viongozi Kamati yaUtendaji Waalikwa

Kamati ya Utendaji, KAWATA Taifa,

Wanamichezo Washiriki

Mabibi na Mabwana.

Kwa niaba ya Kamati ya Olimpiki Tanzania na kwa niaba yangu mwenyewe sina budi kumshukuru Katibu Mkuu Msaidizi wa TOC, pamoja na kuwa moja wa viongozi wa juu wa TOC kukubali mwaliko wa ofisi ya TOC kwa kuja hapa leo  kutufungulia Mkutano huu Mkuu wa Kamisheni ya Wanamichezo.

Ndugu Mgeni Rasmi, ofisi ya TOC imekuwa hapo awali ikialika wageni rasmi hasa katika shughuli hizi za ufunguzi wa mikutano yetu kutoka nje hasa taasisi na serikali, lakini kuanzia sasa itakapobidi shughuli hizi zitafanywa na viongozi wa TOC au Vyama/Mashirikisho ya Michezo.

Ndugu Mgeni Rasmi, tangu Kamisheni ya Taifa ilipoundwa hapo mwaka 2006, kazi kubwa ilikuwa kuhamasisha na kutoa wito kwa Vyama/Mashirikisho ya Michezo kuanzisha Kamisheni ya wachezaji katika Vyama/Mashirikisho yao ya Michezo. Ni Vyama/Mashirikisho chache ambayo yameitikia wito wetu kwa kufanya uchaguzi halali wa kidemokrasia.
Vyama vingi mpaka sasa vimekuwa vikiteua wajumbe wake kuhudhuria Mikutano Mikuu ya Kamisheni inayoandaliwa na TOC, lakini cha kushangaza kwa utafiti ulioofanywa na TOC/KAWATA Taifa, wachezaji hao siyo wajumbe katika Kamati za Utendaji na Mikutano Mikuu ya Vyama na Mashirikisho husika kama Muongozo wa Kamisheni unavyosema.

Sijui ni kwa nini Vyama/Mashirikisho ya Michezo yaogope kuwaingiza wachezaji kwenye chombo cha maamuzi (Kamati ya Utendaji/Mkutano Mkuu). Kuna siri gani kubwa katika vikao vya Kamati ya Utendaji na Mkutano Mkuu ambayo hayapaswi wachezaji kufahamu? 

Mimi nina imani kabisa wawakilishi wa wachezaji watakapokuwa kwenye vyombo hivyo vya maamuzi malalamiko na manung’uniko mengi ya wachezaji hayatakwepo, kwani watakuwa wameshiriki kikamilifu katika maamuzi.

Mahali ambako Mkutano Mkuu wa Kamisheni ya Wachezaji (Kawata) unapofanyikia leo Zanzibar.
Ndugu Mgeni rasmi, Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC), Vyama/Mashirikisho ya Kimataifa (IFs), ANOCA na NOCs kama TOC  zina Kamisheni zao ya Wanamichezo ambazo kazi zao kubwa ni kama:

1.     Kutoa ushauri, nasaha kwa wanamichezo waliostaafu na ambao bado wanaendelea na michezo.
2.     Kulinda maslahi ya wanamichezo ndani ya maadili ya Olimpiki.
3.     Kutoa mapendekezo kwa mambo yanayohusu maslahi ya wanamichezo ndani ya vikao ya Kamisheni husika.
4.     Kufanya lolote lile ambalo ni kwa faida ya wanamichezo kwa ujumla wake.

Kamisheni yetu ya Kitaifa tangu ianzishwe mwaka 2006 na wajumbe wake Kitaifa kuchaguliwa tena mwaka 2012 mjini Dodoma  imechelewa kwa kiasi fulani kutokana na sababu ambazo ni pamoja na kukwamishwa na viongozi wa Vyama/Mashirikisho yao Kitaifa (NFs).

Baadhi ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa Kawaita mjini Zanzibar leo Alhamisi.
Wanamichezo wana uwezo mkubwa wa kushauri viongozi wa vyama/mashirikisho yao katika masuala yanayohusu maendeleo ya michezo, pia kushauri mashirika mbalimbali kuhusu ajira za wanamichezo pamoja na hali ya baadaye mchezaji mhusika anapostaafu.

Mhe. Mgeni Rasmi, michezo kwa sasa ni ajira, ndiyo maana IOC imehamasisha NOCs kuunda Kamisheni za Wanamichezo ili watambuliwe kuwa sekta muhimu ya maendeleo ya michezo katika Taifa letu.

TOC  inaamini kwamba kukiwa na uwakilishi wa wanamichezo katika vyama/mashirikisho ya michezo na asasi za umma nchi yetu itakuwa imepiga hatua katika kupiga vita madawa ya kuongeza nguvu katika michezo ambayo kwa sasa yamepamba moto duniani.
Baadhi ya waalikwa katika mkutano Mkuu wa Kamisheni ya Wachezaji Tanzania (Kawata) Kutoka kushoto Irine Mwasanga, Peter Mwita na Mwinga Mwanjala wakati wa mkutano huo leo Zanzibar.
Mhe. Mgeni Rasmi, bado vyama/mashirikisho ya michezo ya kutothibitisho yanaendelea. Mwaka huu kutoka Bara ni Vyama/Mashirikisho ya Kuogelea, Mpira wa Magongo na kwa Zanzibar Mpira wa Meza na Kikapu havikuthibitisha, lakini wakatma washiriki. Riadha Tanzania kuwasilishwa na wajumbe 3 (wm 2, mk 1).

Kwa haya machache naomba nikukaribishe ili uzungumze na wanamichezo walio mbele yako kisha utufungulie Mkutano huu wa Kamisheni ya wanamichezo kwa mwaka 2015 kama tulivyokuomba.


Ahsanteni kwa kunisikiliza.
Katibu Mkuu wa TOC Filbert Bayi akifuatilia jambo na mjumbe wa Kamati ya TOC Irine Mashanga wakati wa Mkutani Mkuu wa Kawata Zanzibar leo.
 Katibu msaidizi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Jamal Adi akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Kamishenu ya Wachezai (Kawata) leo Zanzibar. Kulia kwa Adi ni Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi.

No comments:

Post a Comment