Wednesday 9 December 2015

Giroud afunga hat-trick Arsenal ikitinga kwa kishindo hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya



Olivier Giroud alikuwa shujaa wa Arsenal wakati alipofunga hat-trick na kuiwezesha Arsenal kuifuna Olympiacos na kutinga hatua ya mtoano ya 16 bora

ANTHENS, Ugiriki
LIVIER Giroud alifunga mabao matatu mwenyewe (hat-trick) wakati Arsenal ikijihakikishia nafasi ya kufuzu kwa hatua ya  16 bora ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kwa kuifunga Olympiakos mabao 3-0.

Ikihitaji ushindi wa mabao angalau mawili kwa bila ili ifuzu kwa hatua hiyo, the Gunners ilionesha kiwango kizuri na kujikuta ikimaliza ya pili katika Kundi F.

Giroud alifunga la kwanza katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo kabla hajafunga tena katika kipindi cha pili baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Joel Campbell.

ARSENAL YAENDELEZA REKODI
Arsenal haijawahi kushindwa kutinga hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya tangu michuano hiyo ilipoanza mfumo mpya katika msimu wa mwaka 2003-04, na uzoefu wao ulidhihirika usiku wa jana katika mchezo huo uliofanyika jijini hapa.

Arsenal iliuanza mchezo huo kwa kasi huku wenyeji wakicheza na kuungwa mkono na mashabiki wa nyumbani waliokuwa wakishangilia bila kuchoka.

Mathieu Flamini alikaribia kufunga baada ya mpira alioupiga kugonga mwamba kabla Giroud hajafunga la kwanza kwa kichwa cha karibu na lango akiunganisha krosi ya Aaron Ramsey.
Giroud akifunga kwa kichwa katika dakika ya 29 dhidi ya Olympiacos katika mchezo dhidi ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya katika mchezo wa Kundi F
Bao la pili lilikuwa bora kwa usiku huo wakati Giroud alilifunga baada ya kukimbia na mpira kutoka katika mstari wa nusu ya uwanja kabla hajapiga na kuujaza mpira wavuni.
Bao la tatu ni la penalty, ambapo Omar Elabdellaoui aliunawa mpira uliopigwa na Nacho Monreal na Giroud alifunga kirahisi.

NINI KINACHOFUATA?
Arsenal ilifanya vizuri na kufuzu baada ya kufungwa mechi za awali mbili dhidi ya Dinamo Zagreb (2-1 ugenini) na  Olympiakos (3-2 nyumbani) ikiwa na maana kuwa ilishindwa kabisa kupata hata pointi moja katika kundi lao baada ya kucheza mechi mbili.

Timu hiyo iliendelea kupata kisago kwa kufungwa 5-1 na mshindi wa kundi hilo, Bayern Munich katika mchezo uliofanyika Ujerumani baada ya kushinda 2-0 dhidi ya kikosi cha kocha Pep Guardiola katika mchezo uliofanyika England.

Sasa wamemaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Bayern ikiwa na maana kuwa timu hiyo sasa itakutana na ratiba ngumu wakati wa upangaji wa ratiba hiyo ya 16 bora ukilinganisha na timu hiyo ya Ujerumani.

Timu inazoweza kukutana nazo ni pamoja na vigogo ya Hispania Real Madrid, Atletico Madrid na Barcelona, Wolfsburg kutoka Ujerumani au ile ya Russia ya Zenit St Petersburg.

Wataungana na ndugu zao wa Chelsea na Manchester City katika ratiba hiyo itakayopangwa Jumatatu

UNACHOTAKIWA KUJUA
Olivier Giroud ni mchezaji wanne wa Arsenal aliyewahi kufunga hat-trick katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya (baada ya Thierry Henry, Nicklas Bendtner na Danny Welbeck).

Hii ni mechi ya kwanza kwa kikosi cha Arsene Wenger kushinda nchini Ugiriki tangu Desemba mwaka 1998 (wakati walipoifunga Panathinaikos kwa mabao 3-1).

Matokeo hayo yanamaliza umwamba wa kutofungwa kwa timu hiyo ya Ugiriki dhidi ya zile za Uingereza

No comments:

Post a Comment