Thursday 24 September 2015

Mamia ya Mahujaji wauawa Makka kwa kukanyagana



Na Mwandishi Wetu
WATU 717 ambao walikuwa wanashiriki ibada ya Hijja nchini Saudi Arabia wamefariki kutokana na kukanyagana karibu na mji mtakatifu wa Makka, maofisa wa Saudi wamesema.

Watu wengine 863 wamejeruhi katika tukio hilo lililotokea Mina, ambako mahujaji milioni mbili walikuwa wakishiriki katika shughuli ya mwisho ya ibada hiyo kubwa ya Hijja.

Ni ajali kubwa zaidi kuwahi kutokea katika miaka 25 ya Hijja.

Maandalizi ya ibada hiyo ambayo ni nguzo ya tano ya dini ya Kiislamu yaligubikwa na fadhaa baada ya winchi kuanguka katika Msikiti Mkuu wa Makka mwezi huu na kuua watu 109.

Mahujaji walikuwa wakisafiri kwenda Mina, bonde kubwa kiasi cha kilometa tano kutoka Makka, wakati wa mahujaji kurusha mawe katika nguzo saba zinazoitwa Jamarat ambazo zinawakilisha shetani.

Nguzo hizo zimesimama katika maeneo matatu, ambako Shetani inaaminika alijaribu kumrubuni Nabii Abraham.

Watu walikuwa wakielekea kwenda kumrushia mawe shetani wakati wengine walikuwa wakirudi upande mwingine. Kisha ikaanza kuwa vurugu na ghafla watu wakaanza kuanguka.

Kulikuwa na watu kutoka Nigeria, Niger, Chad na Senegal miongoni mwa mataifa mengine. Watu walikuwa wakikanyagana ili kwenda sehemu salama na hivyo ndivyo vifo vilivyotokea.

Watu walikuwa wakitaja jina la Mwenyezi Mungu wakati wengine wakilia wakiwamo watoto wadogo na wachanga. 

Wengine walianguka wakiomba msaada, lakini hakukuwapo na yeyote wa kufanya hivyo. Kila mmoja alionekana kuwa na lake.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Makka, viongozi wa Tanzania akiwamo Mufti Shekhe Mkuu wa Tanzania, Abubakari Zubery, walieleza wakati tukienda mitamboni kwamba hakukuwa na taarifa ya kuwapo kwa mwathirika ambaye ni Mtanzania, na taarifa rasmi zinatarajiwa kutolewa leo.

Katika hatua nyingine, Serikali imesisitiza amani, upendo na mshikamano katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, huku ikionya kuwa itakabiliana na wote watakaofanya vitendo vitakavyoashiria kutaka kuvunja amani ya nchi wakati huu wa kampeni, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.


No comments:

Post a Comment