Sunday, 6 September 2015

Wanafunzi 151 wa darasa la saba na kidato cha nne shule za Filbert Bayi wahitimu

Na Mwandishi Wetu

SHULE za msingi na sekondari za Filbert Bayi za Kimara na Kibaha mwishoni mwa wiki zilifanya mahafali ya darasa la saba na kidato cha nne Mkuza Kibaha mkoani Pwani, ambapo jumla ya wanafunzi 151 walikabidhiwa vyeti vyao vya kuhitimu shule.

Mahafali hayo yaligawanyika katika makundi matatu, ambapo kulikuwa na wanafunzi 21 ambao wanatokea katika shule ya msingi Filbert Bayi, ambayo iko Mkuza Kibaha wakati wengine 47 wanatokea katika shule yao ya Kimara huku wale wa sekondari walikuwa wanafunzi 83, ambao shule yao iko Kibaha.

Pamoja na shughuli hiyo ya mahafali ilifanyika pamoja na mgeni rasmi, ambaye ni Kaimu Meneja wa Mawasiliano kwa Umma wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Sam Mwakyanjala, shule ya msingi Kibaha hayo yalikuwa ni mahafali yao ya tano wakati ile ya Kimara yalikuwa ni ya 14 na sekondari yalikuwa mahafali ya 83.

Mitihani ya darasa ya saba itafanyika nchini kote Septemba 9 na 10, yaani Jumatano na Alhamisi ya wiki hii. wakati ile ya kidato cha nne itafanyika Novemba mwaka huu.

Kikubwa, haya ni mahafali ya mwisho ya shule ya sekondari ya Filbert Bayi kuhusisha wanafunzi wakiume, kwani tayari shule hiyo wanafunzi waliobaki ni wakike tu kuanzia kidato cha tatu na tayari inajulikana kama Filbert Bayi Girls Sekondary school, hivyo mahafali ya mwakani itakuwa ni ya wasichana pekee.
Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Filbert Bayi iliyopo Mkuza Kibaha wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa shule na mgeni rasmi kabla ya kuanza kwa mahafali mwishoni mwa wiki.
Wanafunzi wa shule za msingi za Filbert Bayi za Kimara na Kibaha wakiwa katika picha ya pamoja.
Wanafunzi wa sekondari wakati wa mahafali yao katika Uwanja wa Ndani wa FBF Mkuza Kibaha mkoani Pwani.

Wazazi na wageni waalikwa wakiwa katika mahafali ya shule za msingi na sekondari za Filbert Bayi katika Uwanja wa Ndani wa Filbert Bayi (FBF) mwishoni mwa wiki.

RISALA YA MKURUGENZI MKUU, MAHAFALI YA
 DARASA LA SABA NA  KIDATO CHA NNE 05/09/2015
  

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Ndugu Semu Mwakanjala, Kaimu Meneja Mawasiliano kwa Umma, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Meja Mstaafu Ndugu Filbert Bayi,
Viongozi wa Elimu Mkoa wa Pwani,
Wajumbe wa Bodi za Shule,
Wazazi, Wafanyakazi, Wanafunzi,
Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana.
Tunamshukuru Mungu kwa upendo na rehema tele kutuwezesha kukutana tena mwaka huu 2015, kwenye mahafali ya watoto wetu wa darasa la saba na kidato cha nne.

Ninawashukuru kipekee wazazi, na wageni wote mliokubali mwaliko wetu na kuhudhuria sherehe ya leo ya:-
-          Mahafali ya 5 ya shule ya msingi Kibaha yenye wahitimu 21
-          Mahafali ya 14 shule ya Msingi Kimara yenye wahitimu 47
-          Mahafali ya 10 shule ya Sekondari yenye wahitimu  83

HISTORIA YA  SHULE YA CHEKECHEA NA MSINGI

Mhe. Mgeni rasmi shule zetu za chekechea na msingi ziko katika makundi mawili kama ifuatavyo:-

i)  Kimara Dar es Salaam
Mwaka 1996 tulianzisha shule ya chekechea na msingi iliyopo Kimara na tulipata usajili mwaka 2000 kwa namba DS/02/7/007.  Mpaka sasa shule ina jumla ya wanafunzi 584 pia tunao waalimu 40 na wafanyakazi wasio waalimu 31.

ii)  Mkuza – Kibaha
Shule hii ilisajiliwa mwaka 2010 kwa namba PW.01/7/008.  Na ina jumla ya wanafunzi 339,  waalimu 17 na wafanyakazi wasio waalimu 10.

HISTORIA YA SHULE YA SEKONDARI
Mhe. Mgeni Rasmi Shule ya Sekondari Filbert Bayi ilianzishwa rasmi mwaka 2003 kule Kimara palipo na shule ya Msingi na hatimaye majengo yalipokamilika Februari, 2004 tulihamia huku Kibaha na tarehe 2 / 3 /2005 kuzinduliwa rasmi na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya tatu Mhe.   Benjamin William Mkapa. Shule imesajiliwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kupitia namba ya usajili S.1377 na kituo cha mtihani namba S.1437.

MAFANIKIO NA MAENDELEO YA SHULE
Mhe. Mgeni Rasmi shule zetu zimepata mafanikio makubwa kitaaluma na michezo tangu zilipoanzishwa  kama ifuatavyo:-

i)  Matokeo ya Mitihani upande wa Msingi
-      Mwaka 2014 shule za msingi Kimara na Kibaha waliomaliza darasa la saba walifaulu kwa asilimia mia moja (100%) na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwenye shule za serikali, japo wengi wao walirudi Filbert Bayi. 

ii) Matokeo ya Mitihani upande wa Sekondari
Mwaka 2014  wanafunzi 38 walifanya mtihani wa kidato cha nne na matokeo yao ni kama ifuatavyo:-
·        Daraja la 1     -      6  
·        Daraja la 2     -    11 
·        Daraja la 3     -    18 
·        Daraja la 4     -      3  
·        Daraja la 0     -      Hakuna
Tuna matarajio makubwa kwamba mwaka huu hawa wanafunzi wanaohitimu leo watafanya vizuri zaidi na hii ni kutokana na juhudi na mikakati kabambe waliojipangia Waalimu na wanafunzi.
      
ELIMU YA UJASILIAMARI
Pamoja na masomo ya darasani, vijana wetu wameanza kujifunza masomo ya ujasiliamali kama ufugaji wa kuku, upambaji wa kumbi kwa ajili ya sherehe mbalimbali, upishi, ususi, unyoaji, upambaji wa maharusi na utengenezaji nywele.

Taaluma hizi ninaamini zitawasaidia kuwa wajasiliamali wakati wakisubiri matokeo yao wamalizapo shule na vyuo.

Mhe. Mgeni Rasmi ni matumaini yangu kwamba utakuwa umepata kwa kifupi mafanikio na maendeleo ya shule zetu.

HITIMISHO
Mhe.Mgeni Rasmi ili kukamilisha sherehe hii siku ya leo tutakuomba ukabidhi vyeti na zawadi kwa wahitimu wote na zawadi maalumu kwa waliofanya vizuri ikiwa ni pamoja na Kitaaluma, Uongozi bora, Nidhamu na Michezo.


ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
                                 


HOTUBA YA MGENI RASMI KATIKA MAHAFALI YA KIDATO
CHA NNE TAREHE 05 /09 /2015
 
Ndugu Filbert Bayi Mwenyekiti wa Bodi ya shule na Taasisi ya Filbert Bayi
Bi. Anna Bayi Mkurugenzi Mkuu wa shule za Filbert Bayi
Wajumbe wa Bodi ya Shule
Wajumbe wa Kamati ya Shule
Waalimu Wakuu shule za Msingi na Sekondari
Wageni waalikwa , Wazazi ,Wahitimu
Mabibi na Mabwana
Awali ya yote napenda kutoa shukrani zangu nyingi za dhati kwa kunialika  katika siku hii muhimu ya mahafali mwaka 2015 kwa shule zenu za Msingi na Sekondari.
Pia nachukua nafasi hii kuupongeza Uongozi wa shule hizi kwa historia fupi ya shule. Ninawapongeza kwa uanzishwaji wa shule na mwendelezo mzuri wa kutia moyo unaosaidia kwa kiwango kikubwa kuinua elimu katika nchi yetu. Pia nimefurahishwa na tendo la uanzishwaji wa mafunzo ya ujasiliamali kwa vijana wetu.
Kama ulivyotaja kwenye historia kwamba wanafunzi wa darasa la saba na kidato cha nne mwaka jana 2014 walifanya vizuri na kupelekea kufaulu kwa asilimia 100, ni dalili njema kwamba kielimu mnafanya vizuri na mnastahili pongezi sana.
Kwenu nyie mnaohitimu leo nipende kuwapa pole sana kwa kupitia kipindi kigumu cha maandalizi, mkisubiri kufanya mitihani yenu ya mwisho wiki ijayo kwa darasa la saba na mwezi Novemba kwa kidato cha Nne.  Mungu awatie nguvu kuwafungua fahamu zenu na hatimaye kufaulu kwa kiwango kikubwa zaidi na kuendeleza rekodi nzuri ya shule hii.
Vijana wangu wapendwa mmalizapo mitihani yenu ninaamini mtarejea nyumbani kwa Wazazi wenu kukabiliana na hatua nyingine katika maisha. Niwakumbushe kwamba Taifa linategemea sana nguvu zenu kwenye maendeleo ya Taifa letu. Nawaasa kuepuka tamaa na vishawishi vyovyote vibaya mtakavyokutana navyo na  vitakavyowapeleka mahali ambapo si pazuri kimaadili.
Kumbukeni wazazi wamejitahidi sana kutafuta fedha na kuwalipia karo na mahitaji mengine kwa kipindi chote na Waalimu kutimiza wajibu wao kwa juhudi zote hadi leo hii, kazi nzito ya utekelezaji imebaki kwenu.
Mwisho ninapenda kuwapongeza wanafunzi wote mtakaopokea zawadi na tuzo katika Nyanja tofauti za Uongozi bora, kitaaluma, nidhamu, michezo n.k. Vipaji hivi mkaviendeleze huko muendako.
Ni mategemeo yetu kwa kupitia nyie tutaweza kupata viongozi wakuu katika nchi hapo baadaye.
ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA
                                                                                        


No comments:

Post a Comment