Saturday 26 September 2015

Yanga yawalaza mapema Simba kwa kichapo cha mabao 2-0


Na Waandishi Wetu
MABINGWA wa soka Tanzania Bara Yanga leo iliwanyoosha wapinzani wao Simba baada ya kuibuka kidedea kwa mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezaji wazamani wa Simba, Amisi Tambwe aliinyoosha timu yake hiyo ya zamani baada ya kufunga bao dakika moja kabla ya mapumziko  kwa shuti kali la guu la kushoto akiwa ndani ya boksi akipokea pasi kutoka kwa Malimi Busungu.

Busungu aliyeingia uwanjani akitokea benchi, alirekebisha makosa yake alipoipatia Yanga bao la pili katika dakika ya 79 alilofunga kwa kichwa akiunganisha mpira uliotupwa na Mbuyi Twitte.


Simba ambayo ilitawala zaidi kipindi cha kwanza, ilikuwa ya kwanza kulilifikia lango la watani zao Yanga lakini krosi ya Hassan Ramadhani ilidakwa na Ally Mustapha.

Katika dakika ya sita, Simba walilifikia tena lango la Yanga na kusababisha mpira kuwa kona, lakini haikuzaa matunda baada ya kudakwa na Mustapha, ambaye aliumia kabla ya kupatiwa matibabu na kuendelea na mchezo.

Simba ilifanya shambulio la nguvu katika dakika ya tisa, lakini Mwinyi Kazimoto akiwa amebaki yeye na kipa wa Yanga Mustapha, alipiga mpira ukagonga nyavu za nje.

Beki wa Simba Juuko Murahid alioneshwa kadi ya njano kwa kumshika mshambuliaji wa Yanga Donaldo Ngoma.

Hamisi Kiiza nusura aipatie Simba bao la kuongoza katika dakika ya 13 baada ya beki wa Yanga, Nadir Haroub kuchanganyana na kipa wake Mustapha, lakini alishindwa kuuweka kimiani.

Kiiza tena nusura afunge katika dakika ya 27 baada ya kupiga shuti kali ambalo liliokolewa na kipa wa Yanga Mustapha.

Katika kipindi cha kwanza Yanga walishindwa kungara katika safu ya kiungo ambayo ilishindwa kuunganisha mabeki na washambuliaji na hadi kumfanya kocha wao kumtoa Simon Msuva.

Dakika ya 37 Kiiza alishindwa tena kuujaza mpira wavuni kufuatia krosi ya Said Ndemla, baada ya mpira wa kichwa kupaa juu ya lango.

Awadhi Juma alishindwa kufunga licha ya kuwa katika nafasi nzuri ya kufunga, lakini alipiga mpira nje.

Yanga walipata pigo baada ya mchezaji wake Mbuyi Twitte kutolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Israel Nkongo baada ya kuoneshwa kadi ya pili ya njano.

Huu ni mchezo wan ne Yanga inashinda na hivyo kuzidi kukalia kiti cha uongozi katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kujikusanyia pointi 12 huku Simba ikipokea kichapo cha kwanza na kubaki na pointi zake tisa.

Mbali na ushindi huo, Yanga ambayo imecheza nyumbani mechi zote kabla ya jana, ilishinda 2-0 dhidi ya Coastal Union, 3-0 dhidi ya Prisons na 4-1 dhidi ya JKT Ruvu.

Wenzao Simba kabla ya kibano cha jana walishinda ilishinda mechi mbili Tanga 1-0 dhidi ya African Sports na 2-0 dhidi ya Mgambo JKT, kabla ya kuifunga Kagera Sugar 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga wikiendi ijayo itacheza mchezo wake wa kwanza ugenini wakati itakapoifuata Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati Simba wataendelea kucheza Uwanja wa Taifa wakati watakapokaribisha Stand United ya Shinyanga.

Simba: Peter Manyika, Hassan Ramadhani/Paper Abdoulaye, Mohamed Hussein, Hassan Isihaka, Juuko Murshid, Justice Majabvi, Said Ndemla, Mwinyi Kazimoto, Mussa Mgosi/Ibrahim Ajibu, Hamisi Kiiza na Awadhi Juma.

Yanga: Ally Mustapha, Mbuyu Twitte, Haji Mwinyi, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Thaban Kamusoko, Simon Msuva/Malimi Busungu, Salum Telela/Said Makapu, Amiss Tambwe/Deus Kaseke, Donald Ngoma na Haruna Niyonzima.

Mechi zingine leo: Stand United iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT, Tanzania Prisons ilishinda 1-0 dhidi ya Mgambo JKT, Coasta Union ilitoka suluhu na Mwadui ya Shinyanga na Mtibwa Sugar iliilaza Majimaji kwa bao 1-0.

No comments:

Post a Comment