Friday, 18 September 2015

Katibu Mkuu Fifa asimamishwa kwa madai ya kulangua tiketi za Kombe la DuniaZURICH, Uswisi
KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), Jerome Valcke (pichani), amesimamishwa kwa muda usiojulikana kutokana na madai ya badhirifu.

Taarifa ya fifa ilisema kumekuwa na tuhuma kibao zinazomuhusu katibu huyo.

Gazeti moja Alhamisi lilidai kuwa Valcke, 54, alihusika na kuongeza bei ya tiketi za Kombe la Dunia zilizofanyika Afrika Kusini mwaka 2010.

Kiongozi huyo Mfaransa ambaye alianza kuitumikia Fifa mwaka 2007, alisema kuwa anakanusha madai hayo nay eye ahusiki kwa lolote.

Chombo hicho cha juucha soka kimekuwa katika wakati mgumu tangu kuzuka kwa tuhuma za rushwa Mei, wakati polisi wa Uswisi walipovamia hoteli moja jijini hapa na kuwakamata watendaji wakuu wa Fifa.

Marekani tangu wakati huo imewashtaki watendaji hao saba na viongozi wengine wawili wa Fifa kuhusu rushwa na kushiriki katika upangaji wa kula rushwa.

Rais wa Fifa Sepp Blatter alitangaza kuachia ngazi mara baada ya kuchaguliwa tena kukalia kiti hicho Juni mwaka huu kutokana na tuhuma hizo.

Valcke, ambaye mwezi uliopita alikuwa akifikiria kugombea urais wa Fifa, ni msaidizi namba mbili wa Blatter katika taasisi hiyo,  lakini sasa anakabiliwa na uchunguzi kutoka katika Kamati ya Maadili.

Mapema juzi, Eugenio Figueredo, mmoja katika ya viongozi wwa Fifa waliokamatwa Mei, Marekani iliidhinisha kiongozi huyo kurejeshwa katika nchi aliyofanya kosa.

Pamoja na Marekani kuwahoji, mamlaka ya Uswisi pia inachunguza mchakato wa maombi ya kuandaa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2018 na 2022, ambao unadaiwa nao uligubikwa na rushwa.

Fifa hivi karibuni iliunda kamati ya kupambana na rushwa ikiwa na lengo la kuisafisha taasisi hiyo.

Valcke pia katika miezi ya hivi karibuni alikuwa akichunguzwa kuhusu madai ya kuhusika kwake katika madai ya rushwa na pauni milioni 10 (dola za Marekani milioni 6.5), ambayo aliyakanusha.

Mwendesha mashtaka wa Marekani alisema kuwa fedha hizo zililipwa na Afrika Kusini kwa makamu mwenyekiti wazamani wa Fifa Jack Warner ili aweze kuipigia debe nchi hiyo iweze ikiwa ni iahsante baada ya nchi hiyo kufanikiwa kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia 2010.

Ilielezwa kuwa fedha hizo zilihamishwa kwenda kwa Warner kutoka akaunti ya Fifa baada ya kutolewa tena kutoka katika bajeti ya Kamati ya Maandalizi ya Afrika Kusini.

No comments:

Post a Comment