Tuesday 18 September 2018

MAMLAKA VIWANJA VYA NDEGE KUSIMAMA BEGA KWA BEGA NA WAMILIKI WA VIWANJA KATA YA MSONGOLA



Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sekta ya Uchukuzi Mhandisi Atashasta Nditiye akiwa katika ofisi ya Mkurugezi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, TAA, Richard Mayongela.

 Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sekta ya Uchukuzi Mhandisi Atashasta Nditiye, akiongozana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Bw. Richard Mayongela leo wamefanya ziara katika mtaa wa Luhanga, Kata ya Msongola wilaya ya Ilala, eneo ambalo wananchi wa Kipunguni A na Kipunguni Mashariki wanapewa viwanja ili  kupisha upanuzi wa Kiwanja cha ndege cha Julius Nyerere (JNIA).


Mkazi wa Kiboga Luhanga Manispaa ya Ilala , Mrisho Kayete (katikati) akitoa malalamiko yake mbele ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sekta ya Uchukuzi Mhandisi Atashasta Nditiye, namna Kampuni ya Remix ilivyoshindwa kuwalipa toka walipoingia makubaliano juu ya uuzwaji wa mashamba yatakayokuwa viwanja ili kupewa wakazi waliopisha upanuzi wa Kiwanja cha ndege cha JNIA.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri Nditiye alipokelewa na malalamiko ya kutokulipwa fedha za fidia kutoka kwa wamiliki wa mashamba kabla ya upimaji wa viwanja katika mtaa wa Luhanga ambavyo ndivyo vinavyotakiwa  kugaiwa kwa wananchi wa Kipunguni A na Mashariki.

Akiwasilisha malalamiko yake kwa Mhandisi Nditiye, mmoja wa wamiliki wa viwanja katika eneo la Luhanga, Bw. Mrisho Hashim Kawete  alieleza kwamba mkataba unaelekeza kwamba ndani ya miezi minne walipaswa kuwa wamelipwa pesa zao zote lakini mpaka sasa, hilo halijatekelezwa.

Mwakilishi wa kampuni ya  Remix(T)ltd , Lwembu Henjewel (kushoto) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri Mhandisi  Atashasta Nditiye(kulia) , namna kampuni yao ilipofikia juu  ya zoezi la  ugawaji wa viwanja kwa wananchi.

“Kwa mujibu wa mkataba tulitakiwa kupewa malipo yetu ndani ya miezi minne tangu kusainiwa kwa mkataba lakini mpaka leo hii tunashangaa wanakuja watu wengine kupewa viwanja kabla hatujamaliziwa malipo yetu”, alisema Bw. Hashim.

Akiwasilisha pia malalamiko yake kwa Naibu Waziri Aliyekua mjumbe wa Luhanga  katika kipindi mchakato unaanza Bw. Elisante Kisingo Mmwiri ameeleza kwamba mradi huo wameupokea kwa mikono miwili lakini inawakatisha tamaa kuona kama ndani yake kuna ajenda za siri. 


Mkurugenzi  wa TAA, Mh .Richard  Mayongela akifanunua jambo mbele ya waandishi wa habari , namna TAA ilivyofanya mchakato wa malipo ya pesa  kiasi cha Sh bilioni 3.7  kwa Kampuni ya Remix (T) Ltd iliyopewa kwa ajili ya kusimamia kutafuta viwanja  537 vya wananchi waliobomolewa kupisha upanuzi wa Kiwanja cha dege cha JNIA.
“Kwa kweli tunashindwa kuelewa mkutano huu una ajenda gani ya siri, maana hata wananchi hawapewi taarifa juu ya ujio wa Viongozi, mradi huu tumeupokea na tunapenda maendeleo lakini kuna vikwazo vingi sana katika huu mradi”, alisema Bw. Mmwiri.

Naye mwakilishi wa Kampuni ya Tanzania Remix ambayo ndio imepewa jukumu la kusimamia upatikanaji na ugawaji wa viwanja kwa wakazi wa Kipunguni, Bw. Lwembu Henjewele ameeleza kwamba kutokana na uwepo wa asilimia arobaini na asilimia sitini tayari kuna mgawanyo, mfano kama mtu ana viwanja kumi basi vinne vya Tanzania Remix sita vya kwake na huyo hastahili kulipwa fidia isipokua kama anakubali sehemu ya viwanja vyake sita vilivyo bakia viingie kwenye mauzo basi atastahili kupata fedha yake inayotoka kwenye mauzo. 
 
Baada ya Malalamiko hayo Naibu Waziri Nditiye ametoa maagizo kwa Mkurugenzi Mkuu wa TAA kwamba ndani ya wiki moja atarejea tena kuja kuangalia viwanja na asikute migogoro katika eneo hilo.

“Mimi nakupa wiki moja na leo ni Jumatatu, mimi nitakuja jumatatu tena ili tuwe na uamuzi wa mara moja ili tuweze kuwakamata hawa watu wa Tanzania Remix kama watashindwa kutuonesha viwanja visivyokua na Mgogoro 537”, alisema Naibu Waziri Nditiye.

Naibu Waziri Muhandisi  Atashasta Nditiye  mwenye shati jeupe na kofia ( katikati) akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa Viwanja vya Ndege Tanzania, TAA, Richard Mayongela(kulia) wakikagua viwanja eneo la Kiboga Luhanga  Kata ya Msongola lililopo Manispaa ya Ilala ambavyo ilibidi wakabidhiwe wananchi waliopisha upanuzi wa kiwanja cha ndege cha kimataifa JNIA.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAA ameeleza kwamba ameyapokea maelekezo ya Naibu Waziri na kwamba Mkataba umeshaisha muda wake hivyo utekelezaji wake utafanyika ndani ya kipindi cha wiki moja.

“Ndani ya wiki moja kama atakua hajatekeleza maagizo haya yaliyotolewa basi hakutakua na njia nyingine zaidi ya kuchukua hatua za kisheria ikiwepo kudai viwanja ambavyo tulikua tunahitaji, pia napenda kusisitiza kwamba hatupendi kuona wananchi wanapata shida hivyo wananchi watambue kwamba hatujawaacha na kwamba tutashirikiana mpaka mwisho, hakuna haki ya mwananchi itapotea kila mtu atapata haki yake” alisema Bw. Mayongela

Mkataba kati ya Tanzania Remix na Mamlaka ya viwanja vya Ndege TAA ulisainiwa tarehe 28 mwezi Mei mwaka 2014 na ukomo wake ukiwa tarehe 27 mwezi Aprili 2015, ambapo malipo yalifanyika kwa awamu mbili, ya kwanza ikiwa ni Pesa za kitanzania milioni 700 na awamu ya pili pesa za kitanzania bilioni 3.

No comments:

Post a Comment