Thursday 20 September 2018

Simba SC Yafia CCM Kirumba Mwanza, Yafungwa 1-0

Mchezaji wa timu ya soka ya Simba, Shiza Kichuya(kushoto) akimlamba chenga Pastory Athnas wa Mbao FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza jana. Mbao walishinda 1-0.

Na Mwandishi Wetu
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, Simba wamefungwa bao 1-0 dhidi ya Mbao katika mchezo uliochezwa leo kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba jijini Mwanza.
Ni mchezo wa kwanza Simba inapoteza tangu kuanza kwa msimu huu, lakini pia, rekodi yake ya kuifunga Mbao ikivunjwa.

Mbao ilipata bao hilo dakika ya 26 likifungwa na Said Khamis kwa mkwaju wa penalti baada ya Pastory Athanas kuzuiwa na kipa Aishi Manula alipokuwa akijaribu kufunga.
Kwa ushindi huo, Mbao unaisogeza hadi kileleni mwa msimamo wa ligi kwa pointi 10 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi tisa, JKT tisa, Azam nane na Simba ikiwa katika nafasi ya tano kwa pointi saba.

Wekundu hao wa Msimbazi walimiliki mpira kwa dakika 90 na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini walishindwa kuzitumia kutokana na ukuta uliowekwa na wapinzani.
Kocha Patrick Aussems wa Simba alifanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji akiwatoa Mohamed Ibrahim, Shiza Kichuya na kuingia Meddie Kagere na Rashid Juma lakini bado haikusaidia.

Mbao walicheza muda wote kwa kujihami na kuwaacha wachezaji wachache kushambulia kwa kushtukiza lakini walishindwa kuzitumia baadhi ya nafasi walizokuwa wakizipata ili kuendeleza mabao.

Rekodi zinaonesha tangu Mbao ipande Ligi Kuu haijawahi kuifunga Simba. Msimu wa 2016/2017  wekundu hao walivyokuwa nyumbani waliifunga bao 1-0 na kwenye Uwanja wa Kirumba walishinda 3-2.

Pia, msimu wa 2017/2018 Simba ugenini ilipata sare ya mabao 2-2 na nyumbani ilishinda 5-0.

Mechi nyingine zilizochezwa jana ni African Lyon iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Singida United naTanzania Prisons ikilazimishwa sare nyumbani ya mabao 2-2 dhidi ya Kagera Sugar.

No comments:

Post a Comment