Thursday 6 September 2018

Uchukuzi Sports Club Yaanza Maandalizi ya Shimiwi


1.        Wachezaji wa timu ya wanawake na wanaume ya kuvuta Kamba ya Klabu ya Uchukuzi (USC) wakifanya mazoezi jana nyuma ya jengo la Aviation Banana ya kujiandaa na mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), iliyopangwa kuanza Septemba 25 mkoani Dodoma.

Na Mwandishi Wetu
KLABU ya michezo ya Uchukuzi (USC), imeanza kujifua kwa ajili ya kushiriki Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Wakala wa Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (Shimiwi), itakayoanza Septemba 25 kwenye viwanja mbalimbali mkoani Dodoma.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Mbura Tenga amesema wameanza kujifua kwa nguvu ili kurudi na ubingwa wa michezo mbalimbali waliyoshinda kwa mara ya mwisho michezo hiyo ilipofanyika mwaka 2014.
Katibu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bw. Vallery Chamulungu (wa kwanza kulia) akiwa ni miongoni mwa wachezaji wa klabu ya Uchukuzi walioanza mazoezi jana nyuma ya jengo la Aviation wakijiandaa na mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), iliyopangwa kufanyika mkoani Dodoma kuanzia Septemba 25, 2018.
Tenga amesema USC watashiriki kwenye michezo tisa, ambayo imeandaliwa na Shimiwi, ambayo ni mpira wa miguu, netiboli, kuvuta Kamba, riadha, bao, karata, draft, baiskeli na Darts.
   Sharifa Amiri (kulia) akifanya mazoezi ya mchezo wa bao na Bw. Ambakise Mwasunga jana kwenye  viwanja vya nyuma ya Jengo la Aviation wakijianda na mashindano ya Shirikisho la michezo ya Wizara, Idara za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (Shimiwi), iliyopangwa kuanza Septemba 25, 2018 mkoani Dodoma.
“Tunauhakika wa kwenda kufanya vizuri kwani timu imeanza mazoezi tayari ingawa muda ni mdogo, ila ninaamini tutafanya vizuri,” amesema Tenga.

USC inatetea vikombe vinne walivyoshinda mwaka 2014, ambavyo ni Darts – wanaume (washindi wa kwanza); mpira wa miguu (washindi wa pili); na Kamba – wanaume na baiskeli - wanawake (washindi wa tatu).
Katibu Mkuu wa Klabu ya Uchukuzi (USC), Mbura Tenga (katikati) jana akijumuika na wachezaji wa klabu hiyo kwenye viwanja vilivyopo jirani na jengo la Aviation kufanya mazoezi ya kujianda na Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (Shimiwi), iliyopangwa kufanyika mkoani Dodoma kuanzia Septemba 25, 2018.
Ratiba iliyotolewa na Shimiwi inaonesha katika ufunguzi mabingwa watetezi katika mchezo wa kuvuta Kamba wanaume timu ya Ofisi ya Rais Ikulu itavutana na MSD; nao wanawake wa RAS Iringa ambao ni mabingwa watetezi watavutana na Viwanda; huku katika mpira wa miguu Wizara ya Elimu watakutana na Ukaguzi.
     Wachezaji wa mpira wa miguu wa Klabu ya Uchukuzi (USC) wakijifua kwenye viwanja jirani na Jengo la Mamlaka ya Mawasiliano ya Anga wakijiandaa na Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (Shimiwi), inayotarajiwa kufanyika mkoani Dodoma kuanzia Septemba 25 hadi Oktoba 6, 2018.  
Michezo hiyo ambayo pamoja na kuunganisha wafanyakazi wa umma wa maeneo mbalimbali pia huleta burudani kwa wakazi wa eneo husika.


No comments:

Post a Comment