Saturday 15 September 2018

Benitez Hajutii Kuondoka Kwa Mitrovic


LONDON, England
RAFAEL  Benitez amesisitiza kuwa hajutii kumruhusu mshambuliaji,  Aleksandar Mitrovic  kuondoka kwenye klabu ya  Newcastle United na kutua Fulham.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Serbia mwenye umri wa miaka 23, alijiunga na Fulham kwa ada ya uhamisho ya pauni milioni 27, amefunga mabao sita kwenye mechi tano zilizopita kwenye klabu yake na timu ya taifa, yakiwemo mabao manne kwenye Ligi Kuu ya England.
Kinyume chake, Newcastle imefunga mabao matatu kwenye mechi zake nne za Ligi Kuu ya England, huku kocha Benitez akiziba pengo la mshambuliaji huyo kwa kumleta mshambuliaji Salomon Rondon kwa mkopo wa muda mrefu kutoka West Brom, huku Dwight Gayle akienda upande mwingine na Benitez akimsajili Yoshinori Muto kutoka Mainz kwa ada ya uhamisho ya pauni milioni 9.5.
Kuuzwa kwa  Mitrovic kumeibua maswali kwa mashabiki wa Newcastle, lakini Benitez  haonekani kujutia hilo.
Alipoulizwa kiwango cha  Mitrovic msimu huu Benitez alijibu: "Anafanya vizuri, alifanya vizuri na Serbia, lakini Rondon anafanya vizuri na Venezuela.
"Kila mchezaji ana mazingira yake na anaweza akafanya vizuri kwenye timu moja lakini hasifanye vizuri timu nyingine.
"Tunatakiwa kufanya maamuzi kwa kuangalia kinachohitajika na tulijua nini tunahitaji, hiko hivyo, sasa tunatakiwa kusonga mbele.
"Haitabadili uamuzi wangu. Natakiwa kusonga mbele na Ayoze Perez, Joselu, Yoshinori Mutuo na Rondon, hiko hivyo."

No comments:

Post a Comment