Wednesday 10 June 2015

Vodacom kumwaga mapesa kwa washindi wa Ligi Kuu Tanzania Bara



Na Mwandishi Wetu
MSHAMBULIAJI mpya wa Free State Stars ya Afrika Kusini, Mrisho Ngassa ni miongoni mwa wachezaji wanaowania tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 2014/2015.
Mchezaji mwingine ni mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliomalizika hivi karibuni, Simon Msuva pamoja na mchezaji wa Simba Mohamed Hussein au Tshabalala.

Ngassa na Msuva wote walikuwemo kwenye kikosi cha Yanga SC kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliomalizika Mei mwaka huu.

Ngassa alisaini mkataba wa miaka minne na Free State Stars Mei mwaka huu kama mchezaji huru, baada ya kumaliza mkataba wake Yanga SC.

Watatu hao, mmoja wao leo atatajwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu katika taafrija itakayofanyika ukumbi wa JB Belmonte (Kilimanjaro) uliopo katika jengo la Golden Jubilee Tower (PSPF), mtaa wa Ohio, Dar es Salaam kuanzia saa 12:00 jioni.

Kipa chipukizi, Mohamed Yusuph wa Tanzania Prisons atachuana na Said Mohamed wa Mtibwa Sugar na Shaaban Kado wa Coastal Union kuwania tuzo ya kipa bora.

Aliyekuwa Kocha wa Simba SC, Mserbia Goran Kopunovic atachuana na Mholanzi Hans Van Der Pluijm wa Yanga SC na Mbwana Makata aliyekuwa Prisons kuwania tuzo ya kocha bora wa ligi hiyo.

Israel Nkongo atachuana na Jonesia Rukyaa na Samuel Mpenzu kuwania tuzo ya Refa Bora, wakati Mgambo JKT, Mtibwa Sugar na Simba SC zitagombea tuzo ya timu yenye Nidhamu.

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kwa kushirikiana na wadhamini wa Ligi Kuu, Vodacom wanatarajia kutoa zawadi kwa washindi wa ligi hiyo kesho JB Belmonte.

Mgeni rasmi katika halfa hiyo ya utoaji zawadi kwa wachezaji, makocha, na timu washindi atakua ni Juma Nkamia, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

Pamoja na tuzo binafsi, Vodacom ambao ni wadhamini wa Ligi Kuu tangu mwaka 2002, watatoa zawadi kwa bingwa, mshindi wa pili, mshindi wa tatu na mshindi wa nne.

WANAOWANIA TUZO ZA LIGI KUU 2014/2015

Mchezaji Bora; Mohamed Hussein (Simba SC), Mrisho Ngassa (Yanga SC), Simon Msuva (Yanga SC).

Kipa Bora; Mohamed Yusuph (Tanzania Prisons), Said Mohamed (Mtibwa Sugar) na Shaaban Kado (Coastal union).

Kocha Bora; Goran Kopunovic (Simba SC), Hans Van Der Pluijm (Yanga SC na Mbwana Makata (Tanzania Prisons)

Refa Bora; Israel Nkongo, Jonesia Rukyaa na Samuel Mpenzu.
Timu yenye Nidhamu; Mgambo JKT, Mtibwa Sugar na Simba SC.

No comments:

Post a Comment