Saturday 20 June 2015

Taifa Stars yafungwa na Uganda, kocha akaribia kutupiwa virago



 *Aondolewa chini ya ulinzi mkali wa polisi akihofia kupigwa

Na Mwandishi Wetu Zanzibar
SAFARI ya Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imeiva baada ya leo usiku timu yake kupokea kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa majirani zao wa Uganda katika mchezo wa kufuzu kwa fainali za Chan 2016.

Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani (Chan), zitafanyika mwakani nchini Rwanda na Tanzania imecheza na Uganda `The Cranes kujaribu kusaka nafasi hiyo katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilimpa kocha Mart Nooij mtihani wa mwisho na endapo atashindwa kuipeleka Taifa Stars, basi atafute njia ya kuondoka baada ya wapenzi wa soka nchini kuchoshwa na ipigo ya timu hiyo.

Wiki iliyopita, Taifa Stars ilipokea kichapo cha idadi kama hiyo cha mabao kutoka kwa Misri katika mchezo wa kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika mwaka 2017 nchini Gabon.

Kocha wa rtimu ya taifa ya Tanzania (kushoto) akisindikizwa na polisi mara baada ya filimbi ya mwisho timu yake ilipocheza na Uganda Cranes kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar Polisi hao walikuwa wakimlinda asiadhibiwe na wapenzi wa soka wenye hasira.
Hakuna ubishi kuwa baada ya kichapo hicho cha leo kocha huyo Mholanzi atajiongeza kabla TFF haijamuonesha njia ya kutokea baada ya mchezo wa pili utakaofanyika Kampala Uganda wiki mbili zijazo.

Mwaka jana Tanzania ilifungwa 1-0 na Uganda katika mchezo kama huo wa Chan uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa kabla ya kutolewa na kuiacha The Cranes ikisonga mbele.

Mabao ya The Cranes katika mchezo huo ulioanza saa 2;30 usiku ili kuwawezesha wapenzi wa soka kufuturu ndio waende uwanjani yalifungwa na Sekisambo Erisa mabao mawili na Miya Farouk.

Kabla ya kuanza mchezo huo, Taifa Stars ilipata pigo baada ya mchezaji wake Oscar Joshua kuugua gafla na kuukosa mchezo huo.

Kwa mara ya mwisho Stars ilifuzu kwa fainali hizo za Chan mwaka 2009 zilipofanyika kwa mara ya kwanza nchini Iory Coast na ilitolewa katika hatua ya makundi ikiwa chini ya Mbrazil Marcio Maximo.

Wakati huohuo kocha wa timu hiyo ilibidi asindikizwe na polisi mara baada ya filimbi ya mwisho ili kumzuia asipate kichapo kutoka kwa mashabiki wenye hasira waliotaka kumpifa.


No comments:

Post a Comment