Wednesday 17 June 2015

Thadeo azindua Airtel Tanzania Rising Stars


Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini Leonard Thadeo akipiga mpira kuashiria kuanza kwa mashindano ya Airtel Rising Stars.

Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania jana ilizindua rasmi msimu wa tano wa mashindano ya soka kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars ambayo yataanza kutimua vumbi Agosti 8 katika ngazi ya awali na kuhitimishwa kwa fainali za Taifa Dar es Salaam kuanzia Septemba 11 – 21 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye hafla ya uzinduzi huo jana Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania Beatrice Singano alisema kampuni ya Airtel Tanzania  ina nia thabiti ya kusaidia maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu hapa nchini na kujivunia mafanikio yaliyotokana na michuano hiyo kwa miaka minne iliyopita.

 “Tunaona fahari kwamba michuano ya Airtel Rising Stars imeweza kuibua vipaji vya wachezaji ambao baadhi yao wamechaguliwa kujiunga na timu za taifa za vijana chini ya umri wa miaka 20”, alisema Singano.

Kumbukumbu za TFF zinaonyesha kwamba timu ya taifa ya wanawake imeundwa na wachezaji wengi kutoka Airtel Rising Stars ambayo madhumuni yake makubwa ni kuibua na kuendeleza vipaji vya soka kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17. 

Singano pia ametangaza kampuni ya Airtel kuingia mkataba na nahodha wa Ivory Coast na kiungo wa Manchester City Yaya Toure katika kampeni mpya iitwayo  “It’s Now” yenye lengo la kulea na kukuza vipaji barani Afrika kupitia Nyanja mbalimbali kama vile michezo, ikijumuisha mashindano ya Airtel Rising Stars kwa vijana chini ya umri wa miaka 17.

Alisema sehemu nyingine ambazo kampeni hii itazigusa ni mtindo wa maisha na muziki, ambapo wateja watapata ufumbuzi wa masuala mbalimbali ya kiteknolojia ili kuona fursa zinazowazunguka.

Huu ni mwaka wa tano mfululizo kwa michuano ya Airtel Rising Stars kufanyika hapa nchini Tanzania ambayo huanzia ngazi ya chini hadi Taifa. Singano alilipongeza Shirikisho la Mpira wa miguu Tanzania (TFF) pamoja na serikali kupitia Wizara ya Michezo kwa kuiunga mkono kwa dhati michuano ya Airtel Rising Stars tangu ilipoanzishwa nchini mwaka 2011.

Mkurugenzi wa Idara ya michezo katika wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Leonard Thadeo ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema serikali inatambua mchango wa Airtel katika kuibua vipaji vya wanasoka chipukizi. 

“Inatuwia vigumu kuwekeza kikamilifu katika michezo kwa sababu ya kuelemewa na majukumu mengine muhimu ya kijamii ndio maana tunahamasisha sekata binafsi kujitokeza kusaidia na Airtel wanafanya kazi nzuri,” alisema Thadeo.     

Mwaka huu michuano ya ARS itajumuisha mikoa ya Ilala, Kinondoni,Temeke Mbeya, Mwanza na Morogoro kwa upande wa wavulana na huku upande wa wasichana ukiwakilishwa na mikoa ya Ilala,Kinondoni, Temeke, Mbeya na Arusha.

Kwa upande wake, Rais wa TFF Jamal Malinzi aliipongeza Airtel Tanzania kwa kuwekeza kwenye soka la vijana. “Nawapongeza sana kampuni ya Airtel Tanzania kwa mpango wake huu wa kuwekeza kwenye soka la vijana ambao kwa kweli ndio msingi wa maendeleo wa mpira wa miguu hapa Tanzania na duniani kote”, alisema.

No comments:

Post a Comment