Wednesday 24 June 2015

Mkwasa atangaza Taifa Stars mpya na kuwatema saba


Kocha Mkuu mpya wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. Kulia ni msaidizi wake, Hemed Morocco.

 Na Seba Nyanga
KOCHA wa timu ya  Soka ya Taifa,  Taifa Stars, Charles Mkwasa amesema watajitahidi kufanya vizuri katika mchezo wa marudiano kufuzu  kwa fainali ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan)   dhidi Uganda, huku akisisitiza kuwa mashabiki wasitarajie miujiza.
 
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mkwasa alisema kwa muda mfupi waliokabidhiwa timu, hawataweza kufanya mabadiliko makubwa, lakini watajitahidi kwa uwezo wao kuleta matumaini mapya.

Aidha, Mkwassa amefanya mabadiliko kwenye timu ya taifa pamoja na benchi la ufundi, ambapo mbali na kuita wachezaji 26, amemteua kocha wa zamani wa timu hiyo, Abdallah Kibadeni kuwa mshauri wa timu.

Katika timu yake Mkwasa amewapumzisha wachezaji saba waliotumika kwa muda mrefu na kuwaita watatu wapya ambao hawakuwahi kuitwa kwenye timu iliyopita.

Mkwasa aliteuliwa juzi kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Tanzania, akirithi mikoba ya Mholanzi  Mart Nooij aliyefukuzwa mwishoni mwa wiki kufuatia kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Uganda katika mchezo wa Chan.

Alisema wachezaji walioteuliwa wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanajitunza na kujiheshimu ndani na nje ya uwanja, huku akisema  atashirikiana na benchi jipya la ufundi kujenga timu imara bila upendeleo.

Wachezaji  waliowekwa kando ni pamoja na Amri Kiemba, Deogratias Munishi, Salim Mbonde, Erasto Nyoni, Kevin Friday, Oscar Joshua na Hassan Dilunga.

Sura mpya ambazo hazikuwahi kuitwa ni Mudathir Khamis (KMKM), Michael Aidan(Ruvu Shooting) na Ame Ally (Mtibwa Sugar).

Walioitwa kwa jumla ni Mohamed Hussein Tshabalala(Simba) , Deus Kaseke (Mbeya City), Ramadhan Singano (Simba),  Mwadini Ally (Azam), Shomari Kapombe (Azam), Nadir Haroub Cannavaro (Yanga), Kelvin Yondani (Yanga), na Hassan Isihaka (Simba).

Wengine ni  Aggrey Morris (Azam),  Jonas Mkude (Simba), Abdi Banda (Simba), Salum Telela (Yanga), Frank Domayo (Azam), Saimon Msuva (Yanga), Said Ndemla (Simba), Atupele Green (Kagera Sugar), Rashid Mandawa (Kagera) Ramadhan Singano Messi (Simba). John Bocco (Azam), Sugar) na Ame Ally (Mtibwa Sugar),
Wachezaji wa akiba ni Juma Abdul (Yanga), Mudathir Yahya (Azam) na Samwel Kamuntu (JKT Ruvu).

Wachezaji hao wote watazungumza na makocha kesho kwenye hoteli ya Tansoma na keshokutwa wataanza mazoezi rasmi kwenye uwanja wa Boko Veteran kujiandaa na mchezo wa marudiano dhidi ya Uganda.

Katika hatua nyingine, Mkwasa alitangaza benchi la ufundi la Taifa Stars chini ya usaidizi wa Hemed Morocco wakati kocha wa makipa ni Peter Manyika, mshauri wa timu Abdallah Kibadeni, mtunza vifaa Hussein Swedi Gaga huku mratibu wa timu akiwa ni Alhaj Ahemd Mgoyi na meneja wa timu ni Juma Mgunda.

Alisema kamati ya tiba ya TFF itapendekeza majina ya daktari wa timu na mchua misuli watakaoungana na kambi ya Taifa Stars.

No comments:

Post a Comment