Wednesday, 27 May 2015

Tanzania mwenyeji fainali Mataifa ya Afrika 2019Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Soka la Afrika (CAF) limeipa Tanzania uenyeji wa kuandaa fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wenye umri chini ya iaka 17 zitakazofanyika mwaka 2019.

Uamuzi huo ulifikiwa wakati wa Mkutano wa Kamati ya Utendaji ya CAF uliofanyika jijini Zurich, Uswisi juzi jioni.

Kamati ya Utendaji ya CAF imekubali ombi la Shirikisho la Soka Tanzania la kuwa mwenyeji wa fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 mwaka 2019, ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya CAF.

Tanzania iliwasilisha ombi hilo kwa msaada wa serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo chini ya waziri wake, Fenella Mukangara.

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi alisema ni heshima kubwa kwa Tanzania kuandaa mashindano hayo ya Afrika.
Kuandaa mashindano ya vijana ya Afrika ni hatua kubwa katika maendeleo ya soka na itafungua milango kuandaa fainali za wakubwa za Mataifa ya Afrika za Afcon mbeleni, alisema Malinzi.

Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa fainali za Afrika, ambapo imejihakikisha nafasi ya kushiriki fainali hizo kama mwenyeji baada ya kusota kwa miaka mingi ikisaka kufuzu.

TFF ilisema kuwa katika kuandaa kikosi bora cha kushiriki fainali hizo, Tanzania, mwezi ujao itaandaa mashindano ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 13 na wachezaji bora wa mashindano haya wataunda kikosi cha mwanzo cha taifa kuelekea fainali hizo za mwaka 2019.

TFF inamshukuru sana Rais Jakaya Kikwete na Mukangara Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kufanikisha maamuzi haya, na inaamini ushirikiano huu wa Serikali na wadau wengine utafanikisha mashindano haya mwaka 2019.

 Kupitia mashindano haya ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 13 huko jijini Mwanza yatasaidia kuunda kikosi imara tena cha ushindano cha U17 mwaka 2019,aliongeza Malinzi katika ukurasa wake rasmi wa Twitter.

Malinzi tayari ameelezea mipango kabambe ya TFF ya kuunda kikosi imara kwa ajili ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 zitakazofanyika Madagascar mwaka 2017.

Kwa sasa, TFF inaendesha program za vijana wenye umri chini ya miaka 13 na 15 kwa ajili ya kupata timu imara za taifa za vijana kwa ajili ya kufuzu kwa fainali hizo za Madagascar 2017, na zile za vijana za Afrika za mwaka 2019.

Timu hizo zitakuwa zikipiga kambi na kucheza mechi kadhaa za kirafi ndani na nje ya nchi zikiwemo nchi za Malawi, Zambia, Zimbabwe, Botswana na Afrika Kusini.

Katika mkutano huo wa CAF, Niger imepewa uenyeji wa kuandaa fainali za vijana wenye umri chini ya miaka 20 zitakaofanyika mwaka 2019.

No comments:

Post a Comment