Friday, 8 May 2015

Gerrard amenifanya kuwa kocha bora-MourinhoLONDON, England
KOCHA wa Chelsea Jose Mourinho anasema kuwa nahodha wa Liverpool Steven Gerrard amemfanya yeye kuwa "kocha bora", kabla ya timu hizo kukutana Jumapili kwa mara ya mwisho katika msimu huu wa Ligi Kuu ya England.

Mabingwa hao wapya wa England Jumapili wanawakaribisha Liverpool katika moja ya mechi za mwisho za Gerrard mwenye umri wa miaka 34 katika klabu hiyo yenye maskani yake Anfield. Mchezo huo unatarajia kuanza saa 11:00 jioni.

"Adui yangu, alinifanya kuwa kocha bora kwa sababu ilikuwa vigumu kumsimamisha, " alisema Mourinho, huku akiongeza kuwa alijaribu mara tatu kumsajili mchezaji huyo.

"Nasikitika sana hii ni mara ya mwisho nitakabiliana naye."

Gerrard alikaribia kusaini Chelsea wakati Mourinho alipoifundisha klabu hiyo kwa mara ya kwanza mwaka 2005, na kocha huyo Mreno alibainisha kuwa pia alimtaka mchezaji huyo akiwa Inter Milan na hata alipokuwa akifundisha Real Madrid.
 
Alisema kuwa amechelewa kumsajili mchezaji huyo kwa sasa kwani tayari klabu ya LA Galaxy ya Marekani imemuwahi: "Nimechelewa kumsajili. Hawezi kucheza dhidi ya Liverpool. Amefanya mambo makubwa akiwa Liverpool. Alikataa kabisa kuchezea klabu nyingine kubwa, ligi nyingine kubwa, aliamua kuichezea Liverpool pekee.

"Nani alijua kama siku moja nitacheza dhidi ya Steven kama kocha wa Liverpool?"

Endapo angemshawishi Gerrard kujiunga na the Blues, Mourinho alisema angekuwa amefanikiwa mchezaji huyo kumchezesha na Frank Lampard kitu ambacho makocha wengi wa England wanadaiwa kushindwa kukifanya.

No comments:

Post a Comment