Tuesday, 5 May 2015

Ratiba makundi Ligi ya Mabingwa Afrika yapangwa 
CAIRO, Misri
KLABU tatu za Algeria zimepangwa katika kundi moja la michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya michuano hiyo kutokea kitu kama hicho.

Mabingwa watetezi Entente Setif watakutana na wenzao wa USM Alger na MC Eulma katika mechi za Kundi B, huku timu ya Al Merreikh ya Sudan ikikamilisha kundi hilo.

Nchi 12 za juu katika bara la Afrika kawaida hutoa timu mbili kila moja, lakini imekuwa tofauti kwa Algeria baada ya Entente Setif kushinda taji hilo mwaka jana, nchi hiyo ikapata nafasi nadra ya kuingiza timu tatu katika michuano hiyo msimu huu.

Ratiba hiyo ya makundi ilipangwa katika Makao Makuu ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) yaliyopo jijini hapa jana.

TP Mazembe Englebert ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ndio timu pekee iliyofuzu kwa hatua hiyo kutoka nje ya nchi za Afrika Kaskazini zinazozungumza Kiarabu, ikipangwa katika Kundi A.

Timu zingine zilizomo katika kundi hilo ni pamoja na Smouha (Misri), Moghreb Tetouan (Morocco) na Al Hilal (Sudan).

Mechi za hatua hiyo ya makundi zitaanza mwishoni mwa Juni huku timu mbili za kwanza kutoka kila kundi zitafuzu kucheza nusu fainali ya mechi mbili za nyumbani na ugenini Septemba na Oktoba.

Fainali ambayo itachezwa Oktoba na Novemba nayo itapigwa kwa mtindo wa mechi mbili za nyumbani na ugenini.

Ratiba kamili:

Kundi A: Smouha (Misri), Moghreb Tetouan (Morocco), TP Mazembe Englebert (DR Kongo) na Al Hilal (Sudan).

Kundi B: Entente Setif (Algeria, mabingwa watetezi), USM Alger (Algeria), Al Merreikh (Sudan), MC Eulma (Algeria)


No comments:

Post a Comment