Friday, 18 November 2016

Kumekucha tamasha la michezo la Karatu 2016 kufanyika Desemba 17
Mratibu wa Tamasha la Michezo la Karatu, Meta Petro (kulia) akikagua washiriki wa mbio za baiskeli kabla hazijaanza.

Na Mwandishi Wetu
TAMASHA la Michezo la Karatu mwaka huu litafikia kileleni chake Desemba 17, imeelezwa.

Mratibu wa tamasha hilo la kila mwaka, Meta Petro alisema jana kwa njia ya simu kuwa, mashindano ya mchezo wa mpira yatafanyika kwa siku mbili kuanzia Desemba 12 na 16.

Alisema kuwa timu zitakazofuzu kwa nusu fainali zitacheza Desemba 13 kabla ya kutifuana katika fainali Desemba 15 kwa zile zitakazopenya hatua iliyotangulia.

Petro alisema kuwa fainali ya mchezo wa mpira wa wavu itakuwa Desemba 16 huku fainali za riadha, mbio za baiskeli zikifanyika Desemba 17 siku ya ufungaji wa mashindano hayo.

Alisema mwaka huu tamasha hilo linatarajia kuwa kubwa na lenye msisimko na wakitarajia wachezaji kutoka mikoa mbalimbali watashiriki.

Mbali na michezo hiyo ya soka, riadha, baiskeli na wavu, pia tamasha hilo hushirikisha ngoma za asili pamoja na nyimbo na sarakasi.

No comments:

Post a Comment