Friday 11 November 2016

Gulam, Bayi wachukua fomu kutetea nafasi zao za uongozi TOC


Rais wa TOC, Gulam Rashid (kushoto) akimuonesha kitu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnaye alipotembelea katika ofisi ya TOC hivi karibuni. Kulia ni Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi.

Na Mwandishi Wetu
RAIS na Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Gulam Rashid na Filbert Bayi wamechukua fomu kutetea nafasi zao katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Dodoma Desemba 10.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana, zilisema Bayi amechukua na kurudisha fomu.

Viongozi hao wawili ambao jana walitarajia kwenda Qatar kuhudhuria Mkutano Mkuu wa mwaka wa Kamati za Olimpiki za Taifa (ANOC) utakaofanyika wiki ijayo Doha, wamelazimika kuchukua kwani watakuwa huko hadi Novemba 17.

Mwisho kwa kuchukua na kurudisha fomu kwa wanaotaka kuwania uongozi TOC ni Novemba 15 kwani siku hiyo watakuwa hawajarejea nchini.

Akizungumza kwa simu jana, Bayi hakukubali wala kukataa lakini alisema kuwa jana alikuwa na kazi nyingi ofisini kwake kabla ya kuondoka kwenda Qatar.

Taarifa zingine zinasema kuwa Mkurugenzi msaidizi wa zamani wa Kurugenzi ya Michezo katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Yassoda ni miongoni mwa waliochukua fomu za kutaka kuwania ujumbe TOC.

Yassoda ni miongoni mwa wakufunzi wa TOC, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akitoa mafunzo kwa vyama mbalimbali vya michezo nchini.

Wengine ambao tayari wamechukua fomu kutaka kuwania ujumbe ni pamoja na Muharami Mchume, Irine Mwasanga, Noorelain Sharif, Noel Kihunsi na Zakia Mrisho anayewania ujumbe wa wale waliowahi kushiriki Michezo ya Olimpiki (Olympians).

Mkutano huo wa Qatar pamoja na mambo mengine, utasikiliza sera za majiji yanayotaka kuandaa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2024 na ile ya walemavu ya Paralimpiki.

Zaidi ya wajumbe 1,000 kutoka mataifa 206 wanatarajia kuhudhuria mkutano huo wa mwaka.

No comments:

Post a Comment