Sunday, 27 November 2016

Mwenye uchungu na michezo nchini Gidabuday ashinda ukatibu Mkuu riadha Tanzania (RT)


Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Riadha Tanzania (RT), Meta Petro (kulia) na Katibu Mkuu wa Kamati ya Utendaji ya TOC,, ambaye pia mjumbe wa RT, Filbert Bayi wakipiga kura leo kwenye Uwanja wa Taifa.

Na Mwandishi Wetu

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania umefanyika leo kukishuhudia mwanariadha wa zamani, Wilhelm Gidabuday akirithi mikoba ya Katibu Mkuu wa zamani Suleiman Nyambui aliyeko nchini Brunei.

Nyambui kwa sasa ndiye kocha mkuu wa timu ya taifa ya riadha ya Brunei.

Aidha katika uchaguzi huo Anthony Mtaka aliitetea nafasi yake ya Urais wa shirikisho hilo kwa mara nyingine tena kwa kura 73 kati ya kura 74.

Gidabuday alipata kura 38 akiwapita Michael Washa (24) na Gidamis Shahanga (11) huku kura moja ikiharibika katika nafasi hiyo.

Katika nafasi nyingine, William Kalaghe alichukua nafasi ya Makamu wa Rais Utawala kwa kura 59 dhidi ya 15 zilizokwenda kwa Zainab Mbilo huku Dk. Ahmed Ndee alichukua nafasi ya Makamu wa Rais Ufundi kwa kura 74 dhidi ya kura nne za hapana.

Ombeni Zavalla aliyekuwa akikaimu Katibu Mkuu wa RT katika uchaguzi huo alipita bila kupingwa katika nafasi ya Katibu Mkuu Msaidizi kwa kura zote 74 na Gabriel Liginyani akipata nafasi ya Mweka  Hazina wa shirikisho hilo kwa kura 69 kati ya 74. 

Wengine waliopata nafasi ya Ujumbe wa RT ni Lwiza John, Meta Petro, Robert Kalyahe, Dk. Nassoro Matuzya, Rehema Killo, Zakaria Barie, Mwinga Mwanjala, Tullo Chambo, Christian Matembo na Yohana Misese.

 
Katibu Mkuu wa BMT afunguka 

Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Mohamed Kiganja aliweka bayana  RT ndio chama pekee cha michezo nchini kinachoongozwa na Mkuu wa Mkoa, kwetu sisi (BMT) ni utajiri, hii ni dalili nzurihivyo ukiboronga unapoteza nafasi zote mbili, na kuongeza

Migogoro kwenye vyama inakimbiza wawekezaji na wafadhili, sio vema pindi mambo ya ndani yanapokuwa hayaendi sawasawa kukimbilia kwenye vyombo vya habari, alisema Kiganja.

 
Gidabuday asutwa, ajitetea

Mjumbe wa BMT na Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa na Usuluhishi ya baraza hilo Jamal Lwambo alimsuta Gidabuday kwa kauli zake ngumu alizowahi kuzitoa awali.

Katibu Mkuu mpya uliwahi kusema kwa RT wasiporudi na medali ungefanya nini ...sasa kama ulivyokuwa ukiisuta RT ukiwa bado hujaikamata nafasi hiyo watu wamekurudisha kundini wana matumaini makubwa kwako, na kuongeza

Kipindi mlichopata ni kifupi sana..hatutarajii kuona migogoro bali tunarajia kuona timu inatengenezwa vizuri ili kuleta heshima ya Tanzania, alisema Lwambo.

Kwa upande wake Gidabuday alisema, Challenge zangu kwa RT nilipokuwa nje ya shirikisho ndizo zilizonifanya nigombee nafasi hii lakini nawashukuru sana RT kwani hawakunijengea chuki kwa kuwakosoa bali walinitazama kwa upande wa uzuri.

Aliongeza, Kwa umbo mimi ni mwembamba natoa ahadi tena kama ukiniona mwakani wakati kama huu nina kitambi basi uje uniulize kulikoni, alisema Gidabuday.

Tullo Chambo atetea nafasi yake

Afisa Habari wa RT na mjumbe wa shirikisho hilo Tullo Chambo alisema, Kwa kweli kinyanganyiro mwaka huu kilikuwa kigumu ukilinganisha na msimu uliopita wakati tukiingia, lakini naamini uongozi huu kwa mara nyingine utajitahidi kufanya makubwa kuinua riadha.


No comments:

Post a Comment