Tuesday 1 November 2016

Thomas Mashali kuagwa leo mchana Leaders Club na kuzikwa makaburi ya Kinondoni Dar es Salaam



Na Mwandishi Wetu
MWILI wa bondia wa ndondi za kulipwa nchini, Thomas Mashali aliyeuawa Kimara jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia Jumatatu, utazikwa leo kwenye makaburi ya Kinondoni.

Baba mzazi wa marehemu, Malifedha Mashali alisema kuwa mwili wa mtoto wake huyo aliyeuawa kwa kupigwa na watu wasiojulikana, utazikwa katika makaburi ya Kinondoni Mwembejini.

Alisema mipango mingine ya mahali utakapoagiwa mwili huo na utakapoombewa, bado ilikuwa inaendelea na alikuwa hajajua shughuli hizo zitafanyikia wapi.

Mzee Mashali alisema kuwa mwili wa mtoto wake utaagwa katika viwanja vya Leaders Club Kinondoni kuanzia saa 7 mchana kabla ya kwenda kupumzishwa katika nyumba yake ya mileleni katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
 
Mashali alikuwa akishikilia mikanda ya WBO na UBO kabla ya kifo chake, ambapo amekufa huku akiacha mataji kibao ya ngumi ya hapa nchini na yale ya kimataifa.

Wadau wengi wa michezo walitoa masikitiko yao kuhusu kifo hicho cha Mashali huku wengi wao wakisema kuwa bondia huyo alikuwa na kipaji cha aina yake katika ndondi.

Mashali alizaliwa Dar es Salaam mwaka 1989 na alianza kupigana ngumi za kulipwa Novemba 27, 2009 alipopigana na kumtwanga Hamadu Mwalimu katika pambano lililofanyika katika ukumbi wa Texas, Manzese.

No comments:

Post a Comment