Tuesday, 1 November 2016

Kilimanjaro Health Marathon kufanyika Desemba 4 Mjini MoshiNa Mwandishi Wetu
MBIO za tatu za Kilimanjaro Health Marathon 2016 zitafanyika mjini hapa Desemba 4, imeelezwa.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Moshi, Mkurugenzi wa Community Vission & Better Future, Luka Ndalima alisema mbio  hizo zitakuwa za kilometa 10, 5 na tatu.

Alisema zinatarajia kuanza na kumalizikia katika viwanja vya Majengo Mjini Moshi.

Ndalima alisema lengo la mbio hizo za kila mwaka ni kutoa elimu ya afya katika Siku ya Ukimwi Duniani pamoja na ile ya Walemavu, ambazo zote hufanyika Desemba.

Siku ya Ukimwi Duniani hufanyika Desemba mosi wakati ile ya walemavu nayo hufanyika mwezi huo huo, hivyo tumeamua kuzisherehekea pamoja Desemba 4, wikiendi ya kwanza ya mwezi Desemba," alisema Ndalima.

Alisema kuwa pia mbio hizo zinatumika kutoa elimu ya afya na kuwataka kutowaficha ndani walemavu na badala yao wawatoe na kuwapatia elimu kama watoto wengine.

Alisema mafunzo watakayotoa ni kuwaelimisha watu kuhusu kujikinga na maambukizo mapya ya Ukimwi hasa kwa upande wa vijana.

Alisema mwaka jana walishiriki jumla ya wakimbiaji 1,200 huku watu wazima wakiwa 800 na watoto ni 400, ambapo mwaka huu wanatarajia kupata washiriki wengi zaidi.

No comments:

Post a Comment