Wednesday, 10 August 2016

Real Madrid ndio mabingwa wapya wa Uefa Super CupBeki wa Real Madrid Dani Carvajal (katikati) akishangilia na wachezaji wenzake baada ya kufunga bao la tatu na kufanya timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Sevilla  katika mchezo wa Uefa Super Cup juzi kwenye Uwanja wa Lerkendal Stadion, Trondheim.
MADRID, Hispania
BEKI Dani Carvajal alifunga bao safi dakika moja kabla ya kumalizika kwa kipindi cha nyongeza wakati Real Madrid ikiwafunga wapinzani wao Sevilla katika mchezo mkali wa Super Cup.
Real Madrid, ambao ni mabingwa wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya walikuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza wakati Marco Anensio alipofunga kwa shuti la mbali.


Sevilla ambao ni mabingwa wa Ligi ya Ulaya, walisawazisha kupitia kwa Franco Vazquez na penalti ya Yevhen Konoplyanka iliwapatia uongozi baada ya Sergio Ramos kumchezea vibaya Vitolo.

Ramos alifanya matokeo kuwa 2-2 na kulazimisha mchezo huo kwenda muda wa nyongeza kabla Carvajal kuifungia Real Madrid bao la ushindi.

Mchezaji huyo wa zamani wa Bayer Leverkusen alifunga baada ya kukimbia katika eneo la penalti na kumpatia Zinedine Zidane taji lake la pili tangu aanze kuifundisha Real Januari mwaka huu.

Sevilla, ambao waliifunga Liverpool katika fainali ya msimu uliopita wa Ligi ya Ulaya, ilicheza fainali zote tatu zilizopita za Super Cups na kupoteza zote.

Jorge Sampaoli, aliyeichukua baada ya Unai Emery kuteuliwa kuwa kocha wa Paris St-Germain, alionekana kama angeweza kuibuka na ushindi kabla ya Ramos hajafunga kwa kichwa na kufanya ubao wa matangazo kuwa 2-2 dakika tatu kabla ya mchezo kumalizika.

Bao hilo lilisababisha mchezo huo kuongezewa dakika 30 za ziada, ambazo Real Madrid walizitumia vizuri na kuibuka na ushindi.

Real iliwakosa wachezaji wake muhimu, pamoja na Cristiano Ronaldo ambaye aliumia wakati akiichezea Ureno katika fainali ya Kombe la Mataifa ya Ulaya ya Euro 2016, wakati Gareth Bale na Mjerumani Toni Kroos aliongeza mapumziko yake yaliyohusisha mashindano hayo.

"Tulipambana katika kipindi chote cha pili, lakini Madrid hawakukata tamaa na bao lao la dakika ya 90 lilituwezesha sisi kuwa mabingwa", alisema Carvajal, mwenye umri wa miaka 24.
"Leo (juzi) tuliwakosa wachezaji wetu kibao lakini tuna kikosi imara cha wachezaji waliokulia katika timu hii.

Real Madrid, ambayo haijatwaa taji la La Liga tangu mwaka 2012, itaanza kampeni zake za msimu wa mwaka 2016-17 kwa kucheza ugenini dhidi ya Real Sociedad Agosti 21, wakati Sevilla watakuwa nyumbani wakiikaribisha Espanyol mapema siku hiyo.

No comments:

Post a Comment