Monday 1 August 2016

TIMU YA TANZANIA ITAKAYOSHIRIKI MICHEZO YA OLIMPIKI YA RIO YATAKIWA KURUDI NA MEDALI


Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura (kushoto) akikabidhi bendera ya taifa kwa timu Tanzania itakayoshiriki Michezo ya 31 ya Olimpiki Rio, Brazil katika hafla iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Kulia kabisa ni Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Gulam Rashid.

Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imeitaka timu ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya 31 ya Olimpiki kuhakikisha inarejea na medali kutoka katika michezo hiyo nchini Brazil.

Michezo hiyo itaanza Ijumaa hadi Agosti 21, ambapo timu hiyo yenye wachezaji wa riadha (4), kuogelea (2) na judo (1), iliagwa jana na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Anastazia Wambura kwenye Uwanja wa Taifa.

Wanariadha, Alphonce Felix (kushoto) na Said Makula wakiteta kabla ya kuanza hafla ya kukabidhi bendera timu ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya Olimpiki. Wawili hao ni miononi mwa wachezaji saba wa Tanzania watakaoshiriki michezo hiyo ya Rio, Brazil.
Wabura katika hafla hiyo alisema kuwa anatambua changamoto kibao walizopitia wanamichezo hao wakati wa maandalizi ya kushiriki michezo hiyo mikubwa inayoshirikisha zaidi ya mchezo mmoja duniani.

Pia, naibu waziri huyo aliwapongeza wanamichezo wote waliofuzu na wale wanaoshiriki michezo hiyo kwa upndeleo kwa jitihada zao walizofanya wakati wakijiandaa kwa michezo hiyo.


Daktari wa timu ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya Olimpiki 2016, Nassoro Matuzya akisalimiana na Kocha Mkuu wa timu ya riadha, Frrancis John kabla timu hiyo haijakabidhiwa bendera tayari kwa safari ya Rio, Brazil.
Aliwataka wachezaji hao kupambana ili kupeperusha vizuri bendera ya Tanzania na kutangaza utamaduni wa Tanzania zikiwemo ngoma za asili.

Pia aliwapongeza wadhamini mbalimbali, ambapo aliwataka kudhamini na michezo mingine ambayo haipewi kipaumbele.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura akiinia katika hafla ya kukabidhi bendera kwa timu ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya Olimpiki. Kushoto ni Katibu wa wizara hiyo, Profesa Elisante Ole Gabriel, na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja.
Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Elisante Ole Gabriel aliwataka Bodi ya Utalii (TTB) kuwapeleka wanamichezo hao katika mbuga za wanyama watakaporejea kutoka Brazil.

Wanariadha wanaounda timu hiyo ni Alphonce Felix, Said Makula, Fabian Joseph na mwanadada pekee katika riadha, Sarah Ramadhani, ambao wote watashiriki marathon.

Waogeleaji ni Magdalena Moshi na Hilal Hemed Hilal wakati mchezaji pekee wa judo ni Andrew Thomas.

Makocha watakaoongozana na timu hizo ni Francis John (riadha), Alexander Mwaipasi (kuogelea) na Zaid Hamisi (judo) wakati daktari wa timu ni Nassoro Matuzya.

Waogeleaji na mchezaji huyo wa judo na makocha wao wanaoondoka leo kwa ndege mbili tofauti, huku mwanariadha wakike ataondoka Agosti 10 na wale wakiume wataondoka Agosti 15.

Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi akizunggumza na Kaimu Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT), Ombeni Zavalla.
Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi alisema timu hiyo inaondoka kwa awamu kutokana na ratiba za ndege.

Timu ya judo itaondoka kwa ndege ya Afrika Kusini na kundi la pili litakuwa la kuogelea, ambalo litaondoka saa tisa alasiri na Emirates.

Mkurugenzi Mkuu wa MultiChoice Tanzania, Maharage Chande akizungumza wakati wa hafla hiyo ya kuiaga timu ya Tanzania ya Olimpiki kwenye Uwanja wa Taifa.
Nahodha wa timu hiyo, Felix alisema timu ya riadha imejioandaa vizuri baada ya kufanya mazoezi kwa muda mrefu, ambapo aliahidi kurudi na medali.



Jenerali Mstaafu Mrisho Sarakikya (kushoto) akiwa na kiongozi wa mpira wa meza na mjumbe wa TOC.






Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura akimkabidhi Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Gulan Rashid vipeperushi vya Bodi ya Utalii kwa ajili ya kutangaza utalii watakapokuwa Brazil katika Michezo ya Olimpiki.






Baadhi ya wachezaji wa timu ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya Olimpiki wakichukua msosi walipoandaliwa chakula cha mchana katika hoteli ya Lamada.
Wachezaji wa timu ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya Olimpiki wakipata mlo katika hoteli ya Lamada jijini Dar es Salaam.




 

1 comment:

  1. Medali huwa zinatabirika hasa ktk riadha kwa sababu mshindi ni yule aliyemaliza ndani ya MUDA MFUPI. Mchezaji makini anajijua huwa anamaliza mbio za mita elf 10 kwa dakika ngapi. Halafu analinganisha na rikodi ya dunia au ya olimpiki iliyopita. Kwa hiyo wachezaji na viongozi TAYARI wanajua km medalist IPO AMANI HALIPO.

    ReplyDelete