Wednesday 18 May 2016

GEITA GOLD MINE (GGM) NA TACAIDS WAUNGANA KUPAMBANA NA UKIMWI


 
Rais Mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa akikabidhi mfano wa hundi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa  Tume ya Kupambana na Ukimwi, Dk. Fatma Mrisho. Wengine ni Mkurugenzi Mkuu wa GGM, Terry Mulpeter wakati wa uzinduzi rasmi wa Kili Challange kwa mwaka jana.

KWA Kipindi kirefu sasa Tanzania imeendelea kuwa na watu wengi wanaoishi na Virusi vya UKIMWI pamoja na wagonjwa wa UKIMWI.Kwa mujibu wa takwimu kutoka Tume ya Kupambana na UKIMWI nchini (TACAIDS) inakadiriwa kuwa watu milioni 1.6 nchini wanaishi na VVU na Ukimwi. Ugonjwa huu umewaathiri zaidi vijana na watoto yatima zaidi ya milioni 1.3.

Bado ipo changamoto miongoni mwa jamii kuhusu elimu ya ugonjwa huo kwa kuwa kuna vituo vichache sana vya taarifa juu ya janga hilo.Jamii bado ina unyanyapaa kwa Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI pamoja na UKIMWI.

Hali hii ndiyo inayosababisha tuchelewe kukabiliana na janga hili.Waathirika wa tatizo hili wamekuwa woga kwa hofu ya unyanyapaa miongoni mwa jamii.Usiri huu na elimu ndogo ya kukabiliana na ugonjwa huu ikiwemo matumizi sahihi ya kinga na dawa za kupunguza makali yake vimezidi kufanya hali izidi kuwa mbaya

Katika kukabiliana na changamoto hiyo na kuisaidia serikali kufikia lengo namba tatu la Malengo endelevu ya Maendeleo ya Umoja wa mataifa  ya kuwa na jamii yenye afya bora ifikapo 2030,Mgodi wa Dhahabu wa Geita(GGM) kwa kushirikiana na Tume ya Kupambana na UKIMWI nchini (TACAIDS) umendelea tena kuchangisha fedha ili kupambana na UKIMWI kupitia Kampeni yake ya KILI CHALLENGE.
 
KILI CHALLENGE ni kampeni iliyoanza mwaka 2002 ambayo hufanywa kila mwaka kwa wadau mbalimbali kupanda mlima Kilimanjaro na kuchangisha fedha kwa ajili ya kutunisha mfuko wa mapambano dhidi ya Virusi vya UKIMWI pamoja na UKIMWI.
 
Mwaka 2015 pekee Kampeni hii ilifanikiwa kukusanya takribani shilingi za Kitanzania Bilioni Moja. Fedha hizo zitatolewa kwa wadau mbalimbali wanaojishughulisha na mapambano ya Ukimwi katika uzinduzi wa upandaji Mlima kwa mwaka huu pale Hyatt Hotel, Dar es Salaam Ijumaa tarehe 20 Mei. 

Mgeni rasmi katika Hafla hiyo atakuwa makamu wa Raisi Mhe. Samia Suluhu.

Makamu wa Rais wa miradi endelevu wa Anglogold Ashanti (GGM) Bw. Simon Shayo amesema kuwa Kampeni ya Kili Challenge mwaka huu itakuwa na utofauti mkubwa kwa kuwa inafanyika chini ya Serikali mpya.

Kwa miaka 15 iliyopita tumeshirikiana vizuri na Serikali zote pamoja na wadhamini mbalimbali ambao wamekuwa wakituunga mkono kutuchangia fedha ili kupambana na tatizo hili.
 
Tunaamini kuwa Serikali mpya chini ya Rais  Dkt John Pombe Magufuli ambayo imekuwa ikifanya jitihada nyingi kununua dawa na kuboresha huduma za Afya itatuunga mkono katika Kampeni yetu mwaka huu.Anaeleza Bwana Shayo.

Zaidi ya Asasi 30 zimeweza kunufaika na Mfuko huu katika kipindi cha miaka 15 iliyopita. Baadhi ya asasi hizi ni pamoja na TACAIDS, Benjamin Mkapa Foundation, Geita Hospital na nyinginezo.

Shayo amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza kwa wingi kuchangia fedha katika Kampeni hiyo ili kusaidia kupunguza ongezeko la maelfu ya watoto yatima wanaohitaji misaada baada ya wazazi wao kufariki.

Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dk. Fatma Mrisho amesema, Tukifanikiwa kushiriki kikamilifu katika Kampeni hii tutafanikiwa pia kusaidia wajane wasiokuwa na kipato pamoja na wazee wanaolazimika kuwalea wajukuu walioachwa na watoto ambao walifariki kutokana kwa ugonjwa huo 

Kilimanjaro Challenge imebakia kuwa Asasi pekee inayoleta kwa pamoja serikali na Makampuni binafsi kwa ajili ya mapambano dhidi ya VVU & Ukimwi kwa jamii ya Kitanzania na dunia kwa ujumla ili kuwapa matumaini ya kuhakikisha jamii inabaki bila kuathiriwa na ugonjwa huo katika miaka ijayo.

Mpango huo pia unalenga kuisaidia Serikali kukabiliana na VVU & Ukimwi sambamba na kutoa nafasi kwa watalii wa ndani kuupanda mlima Kilimanjaro.

KUHUSU Kili Challenge:
Kwa maelezo zaidi tembelea tovuti ya www.anglogoldashanti.com  na www.geitakilichallenge.com

Kwa maelezo zaidi wasiliana na:-
Tenga B Tenga Manager, Public Relations & Communications
Email: ttenga@anglogoldashanti.com  Tel: +255 282 160 135 | +255 689 103 619

No comments:

Post a Comment