Wednesday, 25 May 2016

TUGHE Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Makao Makuu, TAA HQ, yapata viongozi wapya


Viongozi wapya wa Tughe tawi la Makao Makuu ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, TAA.

Na Mwandishi Wetu
TAWI la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) la Makao Makuu ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA-HQ), limepata viongozi wake wapya katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Transit uliopo katika jengo la Kiwanja cha Ndege cha Zamani (TBI).

TAA ni wakala wa Serikali iliyoanzishwa tarehe 29 Novemba 1999 kwa Tangazo la Serikali Na.404 la mwaka 1999 chini ya kifungu cha 3 cha Sheria Na. 30 ya mwaka 1997 ya Wakala wa Serikali. Wakala hii ilirithi majukumu ya iliyokuwa Idara ya Viwanja vya Ndege (Directorate of Aerodromes) chini ya Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, ulizinduliwa rasmi mnamo tarehe 3 Desemba 1999.

Viongozi hao wamepatikana baada ya uliokuwepo kumaliza muda wao, na  waliochaguliwa katika uchaguzi huo uliosimamiwa na Katibu Mkuu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Gaudence Kadyango,  ni pamoja na Mwenyekiti Bw. Nasib Elias aliyezoa kura zote 28, baada ya kutokuwa na mpinzani, huku katibu mkuu akichaguliwa Bi. Aziza Kipande aliyepata kura 15 akimshinda Bi. Caroline Mntambo aliyepata kura 13.

Wajumbe watatu ambao ni Bi. Mwanaisha Omari, Bw. Joel Mwakamele na Bi. Frida Omari walipitishwa bila kupingwa na wajumbe waliotoka idara mbalimbali za TAA HQ.

Naye Bi. Irene Sikumbili alipata kura zote 14 za wanawake na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake na Katibu Mkuu wake ni Bi. Mwanahawa Mdee aliyepata kura 11 akimshinda Bi. Kipande aliyepata kura tatu.

Walioshinda katika nafasi  ya ujumbe katika kamati hiyo ni Bi. Glory Mollel na Bi. Pendo Pascal; wakati Bi. Mntambo ameukwaa uhazini na Bi. Magreth Mushi ni mwakilishi wa vijana, huku hakukuwa na mwakilishi wa walemavu kutokana na kutokuwa na mlemavu.

Naye mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu Bw. Abdi Mkwizu aliwapongeza viongozi wateule wa TUGHE na kuwaahidi ushirikiano mzuri kutoka upande wa mwajiri.

Katika kutoa neno la shukrani kwa wajumbe, Mwenyekiti Bw. Elias aliwashukuru wajumbe wote kwa kuonesha imani yao ya dhati kwake na kuwaahidi kuendeleza mshikamano na mahusiano mema yaliyojengwa na uongozi uliomaliza muda wake baina ya wafanyakazi na mwajiri, lakini pia baina ya wafanyakazi wenyewe.

Bw. Elias pia ameahidi kuhakikisha wafanyakazi ambao si wanachama wa TUGHE wanajiunga na chama hicho  kwani kina manufaa makubwa kwao yakiwemo ya kutetewa pindi mfanyakazi anapokuwa kwenye matatizo na mwajiri wake .

Naye msimamizi, Bw. Kadyango ambaye aliukabidhi uongozi mpya Katiba, aliwashukuru wajumbe wote kwa kumaliza zoezi la uchaguzi kwa amani na kusisitiza kuwa na ushirikiano mzuri na mwajiri, kudumisha uhusiano mwema kazini kati ya waajiri na waajiriwa, kudumisha uhusiano mwema baina ya wafanyakazi wao kwa wao, kusimamia uboreshaji wa maslahi ya wafanyakazi na hali bora za kazi, ili kufikia malengo.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA SHERIA NA MAHUSIANO TAA

No comments:

Post a Comment