Monday 24 June 2019

Serikali Yaweka Mikakati Viwanja vya Ndege

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Issac Kamwelwe leo akifungua Jukwaa la Pili la Kitaifa la Usafiri wa Anga linalofanyika kwa siku mbili kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imesema imeweka mipango kabambe ya kuboresha viwanja vidogo vya ndege (Airstrips), ili viweze kutumika kirahisi na ndege ndogo zinazosafirisha Watalii kutembelea mbuga mbalimbali za wanyama na vivutio vilivyopo nchini.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Issac Kamwelwe katika Jukwaa la Pili la Kitaifa la Usafiri wa Anga linaloendelea kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), ambapo tayari imeundwa kamati kutembelea viwanja hivyo, ambavyo amesema vipo zaidi ya 600 vikiwemo vya makampuni binafsi.

“Hivi viwanja ndivyo vinavyoingiza Watalii ndani ya mbuga na vivutio vingine baada ya kushuka pale KIA (Kilimanjaro International Airport) na hapa Dar es Salaam Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), sasa hivi vinatakiwa viwe katika ubora mzuri utakaofanya Watalii kujiona wapo sehemu nzuri na salama,” amesisitiza Mhandisi Kamwelwe.
Wadau mbalimbali wa masuala ya usafiri wa anga leo kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC),  wakiwa kwenye picha ya pamoja na mgeni rasmi wa Jukwaa la Pili la Kitaifa la Usafiri wa Anga, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Issac Kamwelwe.

Hata hivyo, Mhandisi Kamwelwe amesema Idara ya Uhandisi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), itaimarishwa zaidi ili iweze kufanya marekebisho kwenye viwanja hivi, ikiwezekana kununuliwa vifaa ili kufanya kazi kwa ufanisi.

Pia amesema tayari Serikali imeweza kusimamia vyema mradi wa ujenzi wa Jengo la Tatu la abiria la JNIA, ambao umekamilika na limeongeza uwezo wa kuhudumia abiria, ambapo itahudumia abiria milioni sita kwa mwaka badala ya milioni 2 waliokuwa wakihudumia na Terminal 2.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Vedastus Fabian (kushoto) akiwasikiliza Maafisa Naomi Mbilinyi na Gladston Mlay (kulia), kutoka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), katika maonesho yanayokwenda sambamba na Jukwaa la Pili la Kimataifa la Usafiri wa Anga linalofanyika kwa siku mbili mfululizo kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC). 
“Ninawataka wafanyabiashara na wadau wengine wote kuchangamkia fursa za kibiashara zilizopo kwenye jengo letu hili la kisasa, ambapo sasa nimetaarifiwa wapo katika hatua za kuwapata watoa huduma ndio maana ninasema mjitokeze kwa wingi kuomba,” amesema Mhandisi Kamwelwe.
Dkt Bartholomew Rufunjo (kulia) leo akipata maelezo mbalimbali kuhusiana na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kutoka kwa Mhandisi Astelius John (kushoto), kwenye maonesho yanayokwenda sambamba na Jukwaa la Pili la Kitaifa la Usafiri wa Anga yanayofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC). Wengine pichani ni Afisa Masoko wa TAA, Pendo Mwakilasa akizungumza na Mtendaji Mkuu wa VIA Aviation Ltd, Suzan Mashibe.

Akizungumzia viwanja vingine amesema baada ya kukamilika kwa upanuzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Songwe na Mwanza vitawekwa katika daraja la Kimataifa, kutokana na kuwa na miundombinu ya kisasa, ambapo kwa upande wa Mwanza ujenzi wa jengo la mizigo upo katika hatua ya mwisho kukamilika.

  1. Mhandisi Astelius John na Afisa Masoko, Pendo Mwakilasa wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (kushoto), leo wakiwaeleza masuala mbalimbali ya viwanja vya ndege wadau waliotembelea meza ya maonesho yanayokwenda sambamba na Jukwaa la Pili la Kitaifa la Usafiri wa Anga yanayofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).
Kwa sasa kiwanja cha ndege cha Songwe kipo daraja 3C na yakikamilika maboresho ya miundombinu kitakuwa daraja la 4D na Mwanza ni daraja 4C.

No comments:

Post a Comment