Thursday 6 June 2019

Ronaldo Aipeleka Ureno Fainali Ligi Mataifa ya Ulaya 2019


LISBON, Ureno
KOCHA wa timu ya taifa ya Ureno, Fernando Santos amemuelezea Cristiano Ronaldo (pichani) ni  "mchezaji wa ajabu" baada ya kuifungia timu yake mabao matatu au hat-trick na kuiwezesha kutinga fainali ya mashindano ya Ligi ya Mataifa ya Ulaya dhidi ya Uswisi.

Ureno iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 huku mabao yake yote yakifungwa na Ronaldo na sasa inasubiri kucheza fainali keshokutwa Jumapili ama na England au Uholanzi, ambazo zilitarajia kucheza jana katika nusu fainali ya pili.

Ronaldo alifunga mabao hayo katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Estadio do Dragao.

Ronaldo, mwenye umri wa miaka 34, aliifungia Ureno bao la kuongoza kwa mkwajui wa mpira wa adhabu katika kipindi cha kwanza, ambao ulijaa wavuni kupitia kona ya chini ya lango upande wa kulia na kumpita kipa wa Uswisi, Yann Sommer.

Hatahivyo, Uswisi walisawazisha katika kipindi cha pili kwa penalti ya utata kupitia kwa Ricardo Rodriguez baada ya mwamuzi kudai kuwa mchezaji mmoja wa Ureno aliunawa mpira wakati sio kweli licha ya kuwasiliana na mwamuzi msaidizi wa VAR.

Licha ya kuwasiliana na mwamuzi msaidizi wa VAR, lakini mwamuzi Brych alitoa penalti hiyo na kuiwezesha Uswisi kupata bao la kusawazisha.

Wenyeji waliendelea kufanya kweli licha ya mchezo huo kuonekana kama ungeongezwa muda kwani matokeo yaliendelea kuwa sare ya 1-1.

Hatahivyo, Ronaldo alidhihirisha makali yake baada ya kuujaza wavuni mpira wa kona iliyochongwa na Bernardo Silva, kabla hajafunga bao jingine sekunde 102 baadae.

Watu wengi wakiwemo makocha waliowahi kuifundisha Ureno na timu zingine ambao baadhi yao sasa ni wachambuzi wa soka, wamemuelezea Ronaldo kama mchezaji wa àjabu’ kutokana na uwezo wake licha ya umri wake kusogea.

Kocha wazamani wa Ronald wakati akiwa Sporting Lisbon, Santos anasema kuwa mchezaji huyo ana kipaji kikubwa katika soka.

"Nilikuwa kocha wake mwaka 2003 na niliona wapi anakoelekea. Nilijua kuwa ni mtu wa ajabu…”

Ureno sasa Jumapili itacheza fainali ya Ligi ya Mataifa ya Ulaya dhidi ya Uholanzi,  ambao jana usiku waliifunga England kwa mabao 3-1 katika mchezo uliochezwa hadi muda wa ziada baada ya timu hizo kutoka sare ya 1-1 katika dakika 90 za kawaida.

Kabla ya mchezo huo, Ronaldo alicheza mechi mbili tu katika timu ya Ureno kati ya nane za kimataifa, na hakutoa mchango wowote katika mechi zote za kufuzu kwa ajili ya kufuzu kwa nusu fainali.

No comments:

Post a Comment