Thursday 6 June 2019

Taifa Stars Yaenda Misri na Matumaini Kedekede


Naibu Waziri, Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Juliana Shonza akikabidhi Bendera ya Taifa kwa Nahodha wa Timu ya Taifa Stars, Mbwana Samatta jijini Dar es Salaam leo Alhamisi. Kulia ni Mkurugenzi wa Michezo, Dk Yussuf Singo. Timu hiyo inatarajia kuondoka kesho Ijumaa kwenda Misri kwa ajili ya michuano ya michuano ya mataifa Africa (Afcon).

Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars,  inatarajiwa kuondoka leo kuelekea nchini Misri ikiwa na kikosi cha wachezaji 32 kwa ajili ya maandalizi ya fainali za Afrika, huku ikibeba matumaini ya kufanya vizuri.

Kabla ya kuanza kwa fainali hizo Juni 21, mwaka huu nchini humo, timu hiyo itaweka kambi ya wiki mbili na kucheza mechi mbili za kirafiki za kujipima nguvu dhidi ya Misri na Zimbabwe au Nigeria.

Akizungumza jana wakati anakabidhiwa bendera na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza,  Nahodha wa kikosi hicho Mbwana Samatta alisema wanaenda kupambana ili kuleta sifa kwa Tanzania.

“Kwa niaba ya wachezaji tunashukuru kwa kuwa nasi hapa na kututakia heri, nafikiri haya ni mashindano makubwa kila mmoja anafahamu, tunaenda kupambana kuleta kitu kitakachoipa sifa serikali hii ya Rais John Magufuli, na tunawaomba muendelee kuwa nasi bega kwa bega kipindi chote cha mashindano,”alisema.

Kocha Mkuu Emmanuel Amunike alisema wanaenda Misri wakiwa na malengo ya kufanya vizuri na kwamba anaamini kujituma kwa wachezaji wake kunaweza kubadilisha historia nyingine, kwani kwenye mpira lolote linaweza kutokea.

“Tangu tumeanza safari hii Agosti mwaka jana hadi hapa tulipofika kumetokana na juhudi za wachezaji, leo tunaenda Misri tukiwa na ahadi na malengo ya kufanya vizuri, lolote linawezekana kama ambavyo baada ya miaka 39 imetokea,”alisema.

Alisema watu wa Tanzania wanastahili kuona mafanikio zaidi kwasababu kuna wachezaji wengi wenye vipaji.

Kocha huyo alimshukuru Waziri Shonza kwa kuwatembelea akisema kuwa wamefurahi ujio wake kwa kuwa umewapa hamasa kama timu.

Awali, Shonza aliwatakia kila la heri wachezaji hao na kusema kuwa ana matumaini watafanya vizuri na kurudi na ushindi.

Alisema macho ya Watanzania yapo kwao hivyo, waende wakapambane, waonyeshe nidhamu na kushikamana ili kuandika historia nyingine nzuri.

“Twende Misri tukashinde na serikali ya awamu ya tano iko pamoja nanyi, tunaomba msituangushe bali mkawe wazalendo mkapigane kufa au kupona kupata matokeo mazuri,”alisema.

No comments:

Post a Comment