Tuesday 29 March 2016

Wenger atamba kuendelea kuifundisha Arsenal msimu ujao, awaponda wanamkosoa na kutaka atimuliwe



Kocha Arsene Wenger.

LONDON, England
ARSENE Wenger anasema kuwa "hana wasiwasi" kuwa ataendelea kuifundisha Arsenal mwanzoni mwa msimu ujao.

Wenger amebakisha mwaka mmoja katika mkataba wake na kumekuwa na uvumi mkubwa kuhusu hatma ya kocha huyo Mfaransa katika klabu hiyo kufutia matokeo mabovu katika wiki za hivi karibuni.

Kimsimamo, Arsenal kwa sasa iko katika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu, pointi 11 nyuma ya vinara wa ligi hiyo Leicester City.

Kikosi cha Wenger pia kilitupwa nje ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya pamoja nay ale ya Kombe la FA mwezi huu, matokeo yaliyosababisha baadhi ya mashabiki wa timu hiyo kuja juu.

Mashabiki hao wamechukulizwa na mwenendo mbovu wa timu hiyo,ambapo wamemtaka kocha huyo kuachia ngazi ili timu hiyo ipate mafanikio.

Hatahivyo, kocha huyo mwenye umri wa miaka 66, ambaye ameifudisha Arsenal kwa misimu 20, anasisitiza kuwa ana uhakika kwa asilimia 100 ataiwezesha timu hiyo kufanya vizuri msimu ujao.

Alipoulizwa kama ataendelea kuwa kocha wa Arsenal msimu ujao, Wenger alisema: "Sina wasiwasi kwasababu nimejitoa kuisaidia timu kufanya vizuri. Kama ninafanya kitu, nakifanya kwa asilimia 100. Wakati wote hujitoa kuiwezesha timu kufanya vizuri.

Guinea ya Ikweta ya kwanza kutupwa nje mbio za Mataifa ya Afrika Gabon 2017


Mchezaji wa Libya, Sadik (kushoto) akigombea mpira na mchezaji wa São Tomé na Príncipe, Sousa Pontes wakati wa mchezo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Gabon 2017 katika mchezo uliochezwa Cairo, Misri jana.

CAIRO, Misri
GUINEA ya Ikweta ambao mwaka jana walikuwa wenyeji wa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon), wamekuwa wa kwanza kutupwa nje ya mbio za kufuzu kwa fainali zile za Gabon 2017.

Timu hiyo imetupwa nje baada ya kupokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Mali.

Mustapha Yatabare ndiye aliyekuwa shujaa wa Mali baada ya kupachika bao katika dakika ya 89 katika mchezo uliofanyika Malabo na kuifanya timu yake kushika uongozi wa Kundi C, ikiwa pointi mbili juu ya Benin.

Guinea ya Ikweta, ambayo ilitinga nusu fainali ilipoandaa masindano hayo mwaka 2015, sasa wanashika mkia katika kundi lake hilo ikiwa na pointi moja huku zikiwa zimebaki mechi mbili kabla ya kumalizika mbio hizo za makundi.

Sudan Kusini ni ya tatu, wakiwa na pointi tatu, na wamebaki na nafasi finyu ya kufuzu kama moja ya timu bora zilizoshika nafasi ya pili.

Kwingineko, Zimbabwe iliisambaratisha Swaziland kwa mabao 4-0 katika mchezo wa kufuzu kwa fainali hizo kutoka katika Kundi L.

Wenyeji, walioambulia sare ya bao 1-1 na Swaziland katika mchezo wa Ijumaa, walitawala mchezo huo wa marudiano uliofanyika jijini Harare, Zimbabwe na kushika uongozi wa kundi wakiwa pointi tatu zaidi ya timu iliyopo katika nafasi ya pili.

Knowledge Musona ndiye aliyekuwa wa kwanza kufunga bao katika dakika ya 53 kwa penalti huku Costa Nhamoinesu akiifanya timu hiyo kuwa mbele kwa mabao 2-0 dakika sita baadae.

Evans Rusike aliongeza ushindi huo wa Zimbabwe huku Khama Billiat akikamilisha ushindi huo baada ya kufunga bao la nne.

Musona aliiambia BBC Sport: "Najisikia furaha sana. Timu yangu imekusanya pointi zote tatu nyumbani, sasa tunaongoza kundi letu na sasa tuna nafasi kubwa ya kufuzu.
Ni muhimu kuondoka na pointi zote tatu kutoka katika mchezo wetu uhao nyumbani (dhidi ya Malawi utakaofanyika Juni 3). 
Swaziland wanabaki wakiwa na pointi zao tano, tatu juu ya Malawi na Guinea ambao walitarajia kucheza jana.
Kila mshindi wa kundi na timu mbili zilizoshika nafasi bora za pili zitafuzu kwa fainali zijazo za Mataifa ya Afrika zitakazopigwa Gabon.

Katika Kundi B Jamhuri ya Afrika ya Kati ikiwa nyuma kwa bao moja, iliibuka na kuifunga Madagascar kwa mabao 2-1.
Faneva Andriatsima alikuwa wa kwanza kuwafungia wageni bao katika dakika ya 35 na kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 1-0.

Lakini mabao mawili yaliyofungwa ndani ya dakika 12, ambayo yalifungwa na Salif Keita katika dakika ya 53 na baadae Limane Moussa alipachika la ushindi.

Matokeo hayo yanaiweka Afrika ya Kati kileleni mwa msimamo wa kundi lao wakiwazidi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa pointi moja.

Libya walipata pointi za kwanza katika Kundi F baada ya kushinda mabao 4-0 dhidi ya Sao Tome e Principe.
Katika mchezo uliopigwa Misri kutokana na sabbau za kiusalama, Mohamed Zubya wa Libya alifunga hat-trick katika kipindi cha pili.

Maandalizi Ngorongoro Marathon 2016 yapamba moto, Waziri Maghembe athibitisha kuzindua mbio hizo Aprili 16



Baadhi ya wanariadha wakichuana katika mbio za Ngorongoro Marathoni 2012 na mbio hizo zimeendelea kukuwa kila mwaka na kushirikisha washiriki kibao kutoka ndani na nje ya nchi.

  Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Jumanne Maghembe amethibitisha kuanzisha msimu wa tisa wa mbio za Ngorongoro Marathon zitakazofanyika Aprili 16.

Mmoja wa waratibu wa mbio hizo, John Mbando alisema kuwa, Maghembe amethibitisha kuwa mgeni rasmi wa mbio hizo za kila mwaka.
 
Mwanariadha wa kimataifa wa Tanzania, Fabian Joseph akimaliza mbio za Ngorongoro Marathon 2012 kwenye Uwanja wa Mazingira Bora mjini Karatu
Mbio za mwaka huu zinatarajia kuwa na msisimko mkubwa na zitashirikisha zaidi ya wanariadha 2,000 kutoka nje na ndani ya Tanzania.

Mbando alisema kuwa mbio hizo zitaanzia katika lango kuu la kuingilia na kutokea katika Hifadhi ya Ngorongoro na kumalizia kwenye viwanja vya Mazingira Bora mjini Karatu mkoani Arusha.
Kampuni mbalimbali zimekuwa zikijitokeza kudhamini mbio hizo. Pichani Tigo walipodhamini mbio za mwaka 2013.
 Mbali na kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasomesha watoto wa kimaasai, pia mbio hizo zinasaidia kupiga vita ugonjwa hatari wa malaria kwa kuwaelimisha watu na kutoa vyandarua.

Mshindi wa kwanza katika mbio za kilometa 21 kwa upande wa wanawake na wanaume, kila mmoja ataondoka na sh. 2,000,000 huku mshindi wa pili ataondoka na sh. 1,000,000 na watatu sh. 500,000.

Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu akisalimiana na mmoja wa waratibu wa Ngorongoro Marathon 2013. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka ambaye pia ni Rais wa Riadha Tanzania (RT) wakati huo Mtaka alikuwa mkuu wa wilaya ya Mvomero.
Zaidi ya sh. Milioni 6 zimetengwa kwa ajili ya zawadi za washindi, ambapo pia kutakuwa na mbio za kilomita tano na zile za wanafunzi wa shule za msingi na sekondari za kilomita 2.5.

Mbio za mwaka huu zinadhaminiwa na Maji ya Kilimanjaro pamoja na Zara Tours na Zara Charity za zingine.
Kabla ya kuanza kwa mbio za Ngorongoro 2013 katika lango kuu la kuingilia na kutokea katika Hifadhi ya Ngorongoro

Nyalandu akimkabidhi zawadi mshindi wa mbio za Ngorongoro 2013 Dickson Marwa. Kushoto ni Alphonce Felix mshindi wa pili wa mbio hizo.
Wanariadha wakichuana katika mbio za Ngorongoro 2013.

Kujitoa kwa Chad kwaiweka pabaya Taifa Stars, kwaiingizia hasara ya mil. 200 TFF



Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Samatta akiwa mazoezini kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Taifa ya Chad ‘Les Sao imejiondoa katika michuano ya kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika (AFCON) itakayofanyika mwaka 2017 nchini Gabon.

Kujitoa ghafla kwa Chad kumeliingizia hasara ya kiasi cha sh. milioni 200 Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya maandalizi mbalimbali.

Taarifa ya kujitoa kwa Chad ilitolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) jana baada ya Les Sao kuandika barua ya kujitoka katika mashindano hayo ikiwa katika kundi G pamoja na timu za Tanzania, Nigeria na Misri.

Chad ilitarajiwa kucheza leo dhidi ya Taifa Stars katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, ikiwa ni mchezo wa marudiano wa kundi G baada ya kucheza mchezo wa awali jijini NDjamena katikati ya wiki iliyopita.

Katika mchezo wa awali uliochezwa Uwanja wa Idriss Mahamat Ouya, Taifa Stars iliibuka na ushindi wa bao 1- 0 , bao lililofungwa na nahodha, Mbwana Samatta dakika ya 30 ya mchezo.

Kufuatia kujitoa kwa Chad, matokeo ya michezo yote iliyoihusisha timu hiyo yanafutwa, na msimamo wa Kundi G kwa sasa unaongozwa na Misri yenye pointi nne, Nigeria pointi mbili na Tanzania pointi moja.

Awali, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John  Magufuli aliitakia heri timu ya Taifa yaTanzania (Taifa Stars) ambayo leo ingecheza na Chad. 

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Gerson Msigwa alisema katika taarifa yake ya jana kuwa, Rais Magufuli aliwataka wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa TFF kutambua kuwa Watanzania wana matumaini makubwa kuwa timu yao itafanya vizuri katika mchezo huo.

Endapo Stars ingecheza na kushinda jana, basi ingefikisha pointi saba na kuipita Nigeria na kama ingeshinda kwa mabao mengi, ingeweza kushikilia kwa muda uongozi wa kundi hilo.

Hata hivyo kujitoa kwa Chadi kumekuwa pigo kwa Stars kwa kuwa sasa inabaki kuwa ya tatu.

Awali, msemaji wa TFF, Baraka Kizuguto alisema hawakuwa na taarifa zozote za kuwasili kwa Chad na wala hawakuwa na taarifa kama timu hiyo imeshindwa kuja nchini kutokana na ukata kama baadhi ya watu walivyodai.

Hadi sasa hatuna taarifa zao na hatujapata taarifa kama Chad wamejitoa kwa sababu ya ukata, ebu muulize vizuri aliyekupa taarifa hizo, alisema Kizuguto jana mchana.

Licha ya Chad, kujitoa lakini kocha wa Stars Boniface Mkwasa, alisema kikosi chake kilikuwa tayari kwa ajili ya mchezo huo wa leo na lengo lao kubwa ni kuendeleza ushindi walioupata ugenini Chad Jumatano iliyopita.

Kocha huyo alisema awali walikuwa na majeruhi wawili beki Kelvin Yondani na kiungo Mwinyi Kazimoto, lakini juzi walianza mazoezi hivyo angewatumia sambamba na mshambuliaji Abdillah Yusuf, aliyejiunga kwa mara ya kwanza na timu hiyo akitokea klabu ya  daraja la pili ya Mansfield ya England.

Rais wa TFF, Jamal Malinzi alikuwa amemtangaza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa kuwa mgeni rasmi katika pambano hilo .