Monday, 21 March 2016

Vijana Temeke walivyomkaribisha mkuu mpya wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kwa jogging kuanzia Uwanja wa Taifa hadi viwanja vya Buliaga Temeke
Na Mwandishi Wetu
KLABU za mbio za pole pole `jogging wilayani Temeke zimemkaribisha rasmi Mkuu mpya wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda na kumtaka awasaidie kujikwamua kiuchumi.

Makonda akizungumza katika hafla hiyo alizitaka klabu hizo za jogging wilayani Temeke kuwatimua viongozi wasioeleweka, ambao wamekuwa wakichelewesha maendeleo yao.

Hafla hiyo ya kumkaribisha  Mkuu mpya wa Mkoa wa Dar es Salaam ilifanyika kwenye Viwanja vya Buliyaga Temeke.

Alisema kuwa hataki kuona viongozi wa klabu za jogging kazi yao kubwa  kupita kwa wanasiasa kuomba pesa kutumia  majina ya vijana. 

Alisema kuwa kiongozi kama huyo atakuwa anawachelewesha katika mipango yao ya maendeleo, hivyo msimvumilie na badala yake mumuondoe haraka.

Aidha, Makonda alisema kuwa vijana wengi hawataki kufanya safari ya mapambano na hivyo kushindwa kufanikiwa kwani hawana nidhamu, hawana bidii na wala hawamuweki Mungu mbele. 

Alisema kuwa yuko tayari kuwasaidia vijana wa Temeke ili waweze kuondokana na umasikini, mradi tu wakubali kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na kumuweka Mungu mbele.

Makonda alisema kuwa Aprili 10 atakutana na vijana wote wa jogging mkoa wa Dar es  Salaam pamoja na wanamichezo wote na wasanii ili kuzungumzia fursa za kujikwamua kiuchumi.

Pia Makonda alisema kuwa atatoa Sh  milioni 2 kwa kikundi cha jogging ambacho kitakuwa na mipango mizuri ya kujikwamua kiuchumi.

Naye msanii maarufu wa mashairi nchini, Mrisho Mpoto ambaye ndiye mratibu wa hafla hiyo alisema kuwa anguko la vijana wa Temeke liko mikononi mwa Makonda, ambapo alimtaka kuhakikisha vijana hao wanajikwamua katika umasikini.

Alisema kuwa chini ya Makonda wanataka kuiona kesho mpya ya Temeke, ambayo itatoa fursa kwa vijana kujikwamua kiuchumi tofauti na zamani.

Jumla ya klabu 66 za jogging kutoka wilaya ya Temeke vikiwa na jumla ya washiriki 2,000 walishiriki katika hafla hiyo, ambapo walianza kwa kukimbia na Makonda kwa kilomita saba kuanzia Uwanja wa Taifa hadi Viwanja vya Buliaga Temeke.

Msanii mahiri wa mashairi, Mrisho Mpoto (kulia) akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kabla ya kuanza mbio za pole `Jogging' zilizoanzia Uwanja wa Taifa hadi Temeke.
Baada ya kushiriki mbio za pole na baadae kufanya mazoezi na kuwahutubia vijana kwenye viwanja vya Buliaga Temeke, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alikunywa chai kwa `mbilimbi' pamoja na viongozi wa jogging wa Temeke.No comments:

Post a Comment