Saturday, 27 January 2018

TAA Yarudishiwa Kiwanja cha Ndege cha Kahama

 Naibu Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elias Kwandikwa (wanne kulia), Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Zainab Telack (Mwenye ushungi) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (watatu kulia), jana wakikagua miundombinu ya Kiwanja cha Ndege cha Kahama kabla ya makabidhiano ya kurudishwa serikalini na Kampuni ya Madini ya ACACIA.
Na Mwandishi Wetu, Kahama
KAMPUNI ya madini ya ACACIA yenye kumiliki migodi ya dhahabu ya Buzwagi na Bulyahulu imekirudisha serikalini Kiwanja cha Ndege cha Kahama kwa ajili ya kuchochea maendeleo kwa ujumla.

Awali mwaka 2005 kiwanja hicho kilikabidhiwa kwa makabidhiano maalum kati ya serikali na iliyokuwa kampuni ya madini ya Barrick walioomba ili kurahisisha shughuli zao za migodini ikiwemo ya kutumia ndege kusafirisha wafanyakazi wao na vifaa.
 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Zainabu Telack akihutubia wananchi waliofika kushughudia makabidhiano ya Kiwanja cha Ndege cha Kahama yaliyofanyika jana baina ya Kampuni ya Madini ya ACACIA na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).
Katika makabidhiano hayo yaliyofanyika jana mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Zainab Telack na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elias Kwandikwa, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela aliiomba serikali kusaidia kurefusha barabara ya kutua na kuruka kwa ndege kutoka Km. 1.5 hadi kufikia Km 2, ili kufanikisha utuaji wa ndege kubwa ikiwemo ya Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) aina ya Bombardier Q400.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (watatu kulia), akisaini nyaraka za makubaliano ya kurudishwa Kiwanja cha Ndege cha Kahama kwa serikali kutoka kwa Kampuni ya Madini  ya ACACIA, ambapo wa pili kulia ni Meneja wa migodi ya dhahabu ya Buzwagi na Bulyahulu, Bw. Benedict Busuzu na wakwanza kulia ni Mwanasheria wa ACACIA, Bi Diana Wamuza, huku Naibu Waziri Sekta ya Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa (mwenye miwani) na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Zainab Telack wakishughudia.
“Tunashukuru wenzetu wa ACACIA kwa kurudisha tena serikalini kiwanja hiki, lakini bado tunaimani tutaendeleza ushirikiano baina yetu, lakini ombi langu kwa serikali ni kuongeza urefu wa barabara ya kutua na kuruka kwa ndege ili ndege kubwa zaidi ziweze kutua ninaimani zitachochea shughuli za kilimo, biashara na madini na uchumi wananchi utaimarika zaidi,” alisema Bw. Mayongela.
 Mwanasheria wa ACACIA, Bi. Diana Wamuza (wa kwanza kulia) akishughudiana makabidhiano ya nyaraka za kurudishwa kwa Kiwanja cha ndege cha Kahama uliofanywa jana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Meneja wa migodi ya dhahabu ya Buzwagi na Bulyahulu, Bw. Benedict Busuzu.
Naye Naibu Waziri, Mhe. Kwandikwa alisema serikali itahakikisha inasaidiana na wadau mbalimbali ili waweze kurefusha barabara ya kutua na kuruka kwa ndege, ili kufanikisha utuaji wa ndege kubwa za abiria na mizigo, ambazo zitachochea maendeleo ya Wilaya ya Kahama na Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla.

Hatahivyo, Mhe. Kwandikwa aliwataka ACACIA kuweka katika mipango yao ya kusaidia ujenzi wa upanuzi na urefushaji wa Kiwanja cha ndege cha Kahama, ili kiweze kutumika kwa lengo la kutua kwa ndege kubwa, ambapo itachochea sera ya kukuza viwanda.
Naibu Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elias Kwandikwa akizungumza mara baada ya makabidhiano ya kurudishwa serikalini Kiwanja cha Ndege cha Kahama kutoka kwa Kampuni ya Migodi ya ACACIA, uliofanyika jana mkoani Shinyanga.  Mwenye ushungi ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Zainab Telack na wa kwanza kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela.
“Tunamaeneo mengi sana hapa Shinyanga, tunawaita wawekezaji waje kuwekeza kwa wingi katika ujenzi wa viwanda, kilimo, madini na biashara nyingine, sasa usafiri wa uhakika upo ukizingatia tunaviwanja viwili vya ndege kikiwemo hiki cha Kahama na kile cha Shinyanga, na malighafi, umeme na maji vipo vya kutosha hivyo waje tu kuwekeza,” alisisitiza Mhe. Kwandikwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa, Bi. Telack alisema sasa mkoa wake utainuka kwa kuwa umepata fursa ya kuongezewa kiwanja cha pili cha ndege cha Kahama, ambapo sasa wananchi wataweza kusafirisha mazao ya kilimo na kufanya biashara na mikoa mingine kutokana na usafiri wa ndege ni wa haraka na uhakika.

“Ninakuomba Naibu Waziri najua hili lipo kwenye wizara yako, utusaidie kuharakisha kumalizika kwa kiwanja cha ndege cha Shinyanga, maana hiki hapa tayari kipo ili na sisi tuweze kupata wawekezaji katika viwanda mfano Wachina wasiende kuwekeza mkoani Pwani pekee bali waje na huku, tunaimani tutachochea maendeleo sio ya mkoa wetu tu ila kwa Taifa kwa ujumla,” alisema Bi. Telack.

Kwa upande wa Meneja wa migodi ya dhahabu ya Buzwagi na Bulyahulu, Bw. Benedict Busuzu alisema wanajivunia tukio la kurudisha kiwanja cha ndege cha Kahama kwa serikali, ili sasa kiweze kutumika na Watanzania wote katika kuchochea ukuaji wa viwanda.


Hata hivyo, Bw. Busuzu ameahidi wataendelea kutoa huduma mbalimbali kwenye kiwanja hicho kama ilivyokuwa awali, na wataendeleza ushirikiano mzuri ulipo kati yao na TAA.

Friday, 26 January 2018

Kambi ya Riadha Kuanza Jumatatu Kilimanjaro

Na Mwandishi Wetu
KAMBI ya timu ya taifa ya riadha kwa ajili ya mashindano mbalimbali ya kimataifa, inatarajia kuanza Jumatatu West Kilimanjaro wilayani Siha.

Kambi hiyo ambayo awali ilitakiwa kuanza Januari 15, ilishindwa kuanza kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya taratibu.

Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday alisema jana kuwa sasa kambi hiyo itaanza rasmi Jumatatu, Januari 29, ambapo wanariadha 15 na makocha wanne watakuwepo.

Alisema kuwa wanariadha hao ni wale watakaoshiriki mashindano tofauti ya kimataifa, ikiwemo mashindao ya dunia ya nusu marathon, Jumuiya ya Madola pamoja London Marathon

Alisema kuwa mashindano ya dunia ya nusu marathon yatafanyika Valencia, Hispania Machi 24 kabla ya kufanyika Michezo ya Juuiya ya Madola kuanzia Aprili 4 hadi 15.

Alisema kuwa mashindano watakaoshiriki wanaridha hao ni yale ya London Marathon, ambayo mbali na Alphonce Simbu pia RT itapeleka wanariadha wengine kwa ajili ya mbio hizo.


Aidha, Gidabuday amesma kuwa makocha Zacharie Barie na Lwiza John ndio wataongoza na timu ya riadha katika Michezo ya Jumuiya ya Madola.

Kyle Edmund atolewa Australian Open 2018

MELBOURNE, Australia
MUINGEREZA Kyle Edmund amesema kuwa "amepata uzoefu wa kushindana katika mashindano makubwa ya tenisi baada ya kutolewa katika nusu fainali ya Australian Open.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 alishindwa kusonga mbele baada ya kuchapwa kwa 6-2 7-6 (7-4) 6-2 na mchezaji wa Croatia anayeshikilia nafasi ya sita kwa ubora Marin Cilic mjini hapa.

Hatahivyo, Edmund aligoma kulaumu maumivu ya nyonga, ambayo yalihitaji matibabu, lakini alicheza mashindano hayo na kutinga nusu fainali.
"Hatimaye nimetoka baada ya wiki nzimaya kufanya vizuri katika mashindano haya, “alisema Edmund.

"Aina hii ya mashindano inakupa uzoefu zaidi. Kwa mara nyingine tena unapata jaribio, ni kama mwaka, nahitaji kama hii zaidi,”

Cilic, 29, alitawala mchezo wa nusu fainali baada ya kuokoa pointi kibao hadi mapumziko.

Mourinho bado yupo yupo Man United hadi 2020

LONDON, England
KOCHA wa Manchester United Jose Mourinho ameongeza mkataba utakaomuweka katika klabu hiyo hadi mwaka 2020, ukiwa na nafasi ya kuongeza mwaka mmoja zaidi.
Mkataba wa awali wa kocha huyo mwenye miaka 54 Old Trafford unatakiwa kumalizika mwaka 2019.

Mourinho alisema “amefurahi” kuwa Man United “wananiamini kuwa kocha sahihi kwa ajili ya klabu kubwa….”

"Najihisi mtu mwenye bahati kufanya kazi na kundi la vijana wa ajabu, “aliongeza.
"Mkataba wangu wa awali ulikuwa ni wa miaka mitatu, sasa tumefanya uamuzi wa wazi kwa kila mmoja sio miaka mitatu, ni minne au mitano, nani anajua, zaidi.”

Mourinho, aliteuliwa kuwa kocha wa Man United kuchukua nafasi ya Louis van Gaal Mei mwaka 2016, ambapo alishinda Kombe la EFL na lile la Ligi ya Ulaya katika msimu wake wa kwanza.

Msimu huu Man United wako katika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya England, wakiwa nyuma ya Manchester City, huku timu hiyo ikiwa bado iko katika mbio za Ligi ya Mabingwa na Kombe la FA.

"Tumeweka viwango vya juu, tukishinda mataji matatu katika msimu mmoja, lakini hicho ni kiwango nilichotarajia, “alisema kocha huyo Mreno.

Woodward alimpongeza Mourinho kwa kazi yake nzuri na weledi”, wakati akitimiza lengo la klabu kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi na wenye viwango”.

Akizungumza mapema juzi katika mkutano na waandishi wa habari, kabla ya kuingia mkataba huo mpya, Mourinho aliipongeza klabuhiyo kwa kumsajili Alexis Sanchez kutoka Arsenal.

Alisema mchezaji huyo wa kimataifa wa Chile amejiunga kutoka klabu ya ajabu na kwenda katika klabu kubwa huku ikishuhudia kiungo wa Armenia Henrikh Mkhitaryan akitua upande mwingine.


Mourinho alisema ni usajili mkubwa kwa kila mtu na kuthibitisha Sanchez atakuwa katika kikosi cha United kilichotarajia kucheza Kombe la FA jana dhidi ya Yeovil.

Coutinho aanza kuichezea Barcelona, aingia akitokea benchi wakati wakiifunga Espanyol 2-0

BARCELONA, Hispania
PHILIPPE Coutinho ameanza kuichezea Barcelona wakati timu hiyo ikiifunga Espanyol na kutinga nusu fainali ya Kombe la Hispania usiku wa kuamkia leo.

Mchezaji huyo aliyesajiliwa kwa ada ya pauni milioni 142 akitokea Liverpool aliingia akitokea benchi zikiwa zimebaki dakika 22 kabla ya mchezo haujamalizika wakati tayari Barcawakiwa mbele kwa mabao 2-0.

Barcelona imesonga mbele kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-1 baada ya mchezo wa kwanza kufungwa 1-0.

Coutinho nusura angesaidia kupatikana kwa bao, lakini kipa Pau Lopez aliokoa shuti la Luis Suarez, ambaye awali aliifungia Barca bao la kuongoza dhidi ya wapinzani wao wa jiji.

Lionel Messi alifunga bao safi la pili wakati akitimiza mabao 4,000 kwenye uwanja huo wa Nou Camp.

Sevilla, Valencia na Leganes – ambayo iliitoa Real Madrid Jumatano, ni timu zingine zilizopo katika nne bora.

Kabla ya mchezo huo, beki wa Argentina Javier Mascherano alitoka nje ya uwanja kuaga, baada ya kukamilisha uhamisho wa kwenda kucheza China katika klabu ya Hebei China Fortune.


Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 ambaye aliwahi kuichezea West Ham na Liverpool alitumia miaka nane katika klabu ya Barca, akishinda mataji 18 yakiwemo manne ya La Liga na mawili ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Monday, 22 January 2018

Mwanasoka Gearge Weah aapishwa Monrovia leo

George Weah akiapishwa kuwa Rais mpya wa Liberia leo mjini Monrovia.

Simba Yaichapa Kagera 2-0 na kurejea kileleni

Na Mwandishi Wetu
MABAO mawili yaliyofungwa na Said Ndemla na John Bocco ‘Adebayor’  dhidi ya Kagera Sugar, leo yameirudisha Simba kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, na kuishusha nafasi ya pili Azam iliyokuwa imekaa nafasi hiyo kwa muda baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons jana.

Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha pointi 32, katika michezo 14 na wanatarajiwa kumaliza mzunguko wa kwanza wikiendi inayokuja kwa kukabiliana na Majimaji Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Katika dakika 45 za kipindi cha kwanza, timu zote mbili zilishambuliana kwa zamu na kupoteza nafasi kadhaa walizozipata, huku wachezaji wawili wa Kagera Sugar, Juma Nyosso na Mohamed Fakhi wakioneshwa kadi za njano kutokana na kucheza rafu mbaya kwa wachezaji wa Simba.

Kipindi cha pili Simba waliingia kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 69, lililofungwa na Ndemla aliyemalizia pasi murua ya Shiza Kichuya na kupiga shuti, ambalo kipa wa Kagera Sugar, Juma Kaseja alibaki akiukodolea macho ukitinga nyavuni kwake.

Kagera Sugar walijitahidi kupambana kutafuta bao la kusawazisha kupitia kwa washambuliaji wake, Atupele Green na Pastory Athanas, lakini safu ya ulinzi ya Simba ilikuwa makini kuondosha hatari zote langoni mwao.

Dakika ya 79 Bocco, aliifungia Simba bao la pili na kuihakikishia timu hiyo ushindi akimalizia krosi nzuri iliyotokana na jitihada kubwa za beki Shomar Kapombe aliyeingia dakika ya 71 kuchukua nafasi ya Nicholaus Gyan.

Hiyo ilikuwa ni mechi ya kwanza kwa Kapombe tangu aliposajiliwa na Simba, akitokea Azam FC, na kabla ya kupiga krosi hiyo alifanya kazi kubwa ya kumtambuka beki wa Kagera Sugar Adeyum Mohamed.

Chirstopher Edward wa Kagera ambaye aliigia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Athanas mara kadhaa alimjaribu kipa Aishi Manula wa Simba, lakini lengo lake lilishindikana kutokana na kipa huyo kuwa imara kwa kudaka mashuti yote ya wapinzani wao.

Mshambuliaji Emmanuel Okwi ambaye katika mchezo uliopita dhidi ya Singida United alifunga mabao mawili akitokea benchi, jana hakuweza kufurukutwa baada ya kuwekwa chini ya ulinzi mkali na Juma Nyosso  ingawa dakika za mwishoni mwa mchezo huo alikaribia kufunga bao, lakini Kaseja alifanya kazi nzuri kwa kuuwahi mpira.


Wakati huo huo; timu ya Singida United nayo ililazimishwa sare kwa kutoka sare ya kufungana 1-1 na Majimaji FC katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Sunday, 21 January 2018

George Weah Apiga Bao Akijiandaa Kuapishwa Kuwa Rais wa Liberia

Rais Mteule wa Liberia, George Weah (kushoto) akimiliki mpira wakati wa mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Jeshi uliofanyika jana. Weah anatarajia kuapishwa kesho mjini Monrovia kwa rais rasmi wa nchi hio.
MONROVIA, Liberia
GEORGE Weah alifunga bao la kipindi cha kwanza na kuiongoza timu ya Weah All Stars kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya timu ya Jeshi la Liberia katika mchezo wa kuelekea kuapishwa kwa rais mpya wa nchi hiyo mjini hapa.

Weah anaapishwa rasmi kesho kuwa rais mpya wa Liberia baada ya kushinda uchaguzi hivi karibuni.

Mchezo huo ulikuwa sehemu ya program ya hafla ya kuapishwa kwa Weah mwenye umri wa miaka 51, ambaye ni mchezaji soka nyota wazamani, ambaye Desemba alichaguliwa kuwa rais wan chi hiyo.
"Asili ya mchezo ni kushinda, “alisema Weah alipozungumza na BBC Sport baada ya mchezo huo wa maonesho.

Weah alikuwa amevaa jezi namba 14 ya asili, akiwakubusha watazamaji ugwiji wake wa soka wakati akivaa jezi namba hiyo ya timu ya taifa ya Liberia, ambako aliifungia Lone Stars mabao ya kukumbukwa.

"Hii ni namba yangu, nambayo nilipewa na taifa, hivyo nimeivaa, “alisema.

Mchezo huo ulichezwa chini ya ulinzi mkali tena wakati wa jua kali, ambapo mamia ya watu walifurika kwenye uwanja huo uliopo katika kambi ya jeshi kumshuhudia mchezaji bora wa dunia wa mwaka.
Huku bandi ya jeshi ikitumbuiza pembeni ya uwanja, Weah aliamsha hisia za mashabiki pale alipowapita wachezaji wa timu pinzani.

Bao lake lilipatikana katikakipindi cha kwanza kwa mkwaju wa adhabu baada ya shuti lake kubadili mwelekeo na kujaa kushoto ya lango.

"Tumekuja kushinda, hii sio ndoto, “alisema, akitembea pembeni ya mkuu wa majeshi, Meja Jeneral Daniel Ziankahn.

"Wachezaji wa jeshi wanaweza kukimbia, wana nguvu zaidi yetu, lakini tulipiga mpira vizuri na tulijipanga vizuri pia.

"Tulitumia udhaifu wao, kwa upande wa ufundi na kwa kweli kifundi tulikuwa wazuri zaidi yao, “aliongeza Weah.
Timu ya Weah All Star iliundwa na wachezaji wenzake wazamani wa timu ya taifa, ambao walimuunga mkono katika mbio za kusaka urais.

Mmoja wao alikuwa mshambuliaji wazamani wa Arsenal Christopher Wreh, ambaye alicheza pamoja na George Weah katika klabu yake ya kwanza Ulaya, AS Monaco.

"Ni siku maalum kwa sababu baada ya leo itakuwa ngumu sana kukutana naye (Weah), “alisema Wreh alipozungumz na BBC Sport.


"Leo najivunia kuwa wote kati yetu tumemzunguka akielekea kuwa rais wa Liberia, “alisema.

Wababe wa Yanga Wachapwa na Vibonde Stand

Na Mwandishi Wetu, Mwanza
WACHOVU wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Stand United ya Shinyanga (pichani)  imewazima wababe wa Yanga, Mbao FC baada ya kuwafunga bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.

Mbao FC wiki iliyopita ilitoa kipigo kwa mabingwa watetezi Yanga baada ya kushinda mabao 2-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, lakini wamejikuta wakishindwa kuibuka na pointi tatu au moja dhidi ya vibonde Stand United, ambao kabla ya mchezo huo walikuwa wakikalia mkia na pointi zao 10.

Ushindi huo umeibena Stand United hadi kufikia nafasi ya 11 kati ya timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo.
Ushindi huo unaifanya Stand United ifikishe pointi 13 baada ya kucheza mechi 14 na kusogea juu hadi nafasi ya 11 kutoka mkiani kwenye ligi ya timu 16.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Jacob Adongo aliyesaidiwa na Hellen Mduma na Martin Mwalyaje, Stand United walipata bao lao dakika ya 40 likifungwa na Vitalis Mayanga kwa penalti baada ya kipa wa Mbao, Ivan Rugumandiye kumkamata miguu Landry Ndikumana baada ya wote kuanguka wakati wanawania mpira ndani ya boksi.


Katika mchezo mwingine leo, Mtibwa Sugar imelazimishwa suluhu na Njombe Mji FC kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro. 

Saturday, 20 January 2018

Kiganja Alipohitimu Chuo cha Diplomacia

Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa, BMT, Mohamed Kiganja (kushoto), katika mahafali ya Chuo cha Diplomacia Kurasini jijini Dar es Salaam jana. Kiganja amehitumu Post Graduate ya Uhusiano wa Kimataifa.
 





Chelsea Yatoa Kipigo Kizito EPL cha Mabao 4-0

Beki wa Brighton, Markus Suttner (kushoto) akiwania mpira na kiungo wa Chelsea, Eden Hazard wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya England kwenye Uwanja wa  American Express Community huko Brighton, kusini ya England jana. Chelsea ilishinda mabao 4-0. (Picha na AFP).
LONDON, England
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya England, Chelsea jana walitoa kichapo kikali kwa Brighton & Hove Albion baada ya kuitandika mabao 4-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Community.

Kwa ushindi huo, Chelsea imefikisha pointi 50 na kuwa katika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 20.

Liverpool endapo itashindamchezo wake wa leo dhidi ya Swansea City kwenye Uwanja wa Liberty, nayo itafikisha pointi 50, lakini zitakuwa zikishindana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.


Mabao ya Chelsea jana yalifungwa na Eden Hazard mawili huku mengine yakiwekwa kimiani na Willian na Moses.

Shimiwi Kuandaa Bonanza Kubwa Dodoma

Uongozi mpya wa Shirikisho la Michezo la Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) mara baada ya kutangazwa na msimamizi wa uchaguzi uliofanyika hivi karibuni kwenye hoteli ya Mount Uluguru mkoani Morogoro.
Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Michezo la Wizara na Idara za Serikali (Shimiwi) linatarajia kuandaa bonanza kubwa la kwanza la michezo mkoani Dodoma litakalofanyika mwezi ujao.

Katibu Mkuu wa Shimiwi, Moshi Makuka alisema jana kuwa, bonanza hilo la michezo ni kwa ajili ya kulitambulisha shirikisho hilo mkoani humo, hasa ukizingatia ndio Makao Makuu ya nchi na wafanyakazi wengi wa Serikali wako huko sasa.
Makuka alisema kuwa baada ya Dodoma, bonanza hilo litahamia jijini Dar es Salaam, ambako wafanyakazi wa Serikali watashiriki katika michezo mbalimbali.

Alisema kuwa kamati yao ya utendaji ilikutana hivi karibuni, ambapo pamoja na mambo mengine ilijadili pia utekelezaji wa akizo la Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan la kufanya mazoezi kila wiki ya pili ya kila mwezi, ili kuweka fiti afya za wafanyakazi.

Pia walijadili jinsi ya kukiendeleza kiwanja chao cha Bunju B jijini Dar es Salaam, ambapo mbali na kujenga uwanja wa michezo, pia kutakuwa na hosteli na kumbi kwa ajili ya shughuli mbalimbali, ambazo zitawaingizia kipato.

Aidha, kikao hicho kiliunda kamati mbalimbali ikiwemo ya habari na mawasiliano kwa ajili ya kulitangaza shirikisho hilo kwa wadau mbalimbali.

Alisema waandishi wa habari za michezo wa Kituo cha Televisheni cha Taifa (TBC), Jane John na Jessey John  na  Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bahati Mollel ni miongoni mwa wanaounda kamati hiyo.
Makuka alisema wanataaluma hao wa habari, ambao pamoja na kuwa ni wachezaji katika timu za wizara zao, wamekuwa pia wakitoa michango mikubwa katika kutangaza na kuandika habari za Shimiwi.

Wengine waundao kama hiyo ni pamoja na Itika Mwankenja (Mwenyekiti), Elias Malima (katibu) na wajumbe ni James Katubuka na David Kitila.
Kamati ya Utendaji inaundwa na Daniel Mwalusamba (Menyekiti), Ally Katembo (Makamu Mwenyekiti), Makuka (Katibu Mkuu), Alex Temba (Katibu Msaidizi), William Mkombozi (Mhazini), Frank Kibona (Mhazini Msaidizi).

Wajumbe ni Appolo Kayungi, Damian Manembe, Seleman Kifyoga, Assumpta Mwilanga na Aloyce Ngonyani, huku wajumbe wa viti maalum ni Mariam Kihange na Mwajuma Kisengo.

Wanaounda Kamati ya Mipango ni Mwalusamba (Mwenyekiti), Mkombozi (Katibu) na wajumbe ni Makuka, Ngonyani, Kihange na John Jambele; huku kamati ya Ufundi inaundwa na Kayungi (Mwenyekiti), Manembe (Katibu) na wajumbe ni Kisengo na Joyce Benjamin; Kamati ya Nidhamu wapo Katembo (Mwenyekiti), Temba (Katibu) na wajumbe ni Marcel Katemba na Mwilanga.

Kamati ya usajili itaongozwa na Temba (Mwenyekiti), Kibona (Katibu) na James Emmanuel (Mjumbe); nayo Sekretarieti ya Uendeshaji inaundwa na Kihange (mwenyekiti), Kifyoga (Katibu), na wajumbe ni  Bahati Magambo, Buya Ndalija, Justo Mwandelile, Ahmed Chitagu, Peter Lihanjala, Gracia Kyelula, Peter Onono, Modesta Kaunda, Amina Kakozi, Ismail Ismail, Sophia Mkama na James Emmanuel.
Nayo Kamati ya Huduma za tiba itaongozwa na Joakim Mwaipaja (Mwenyekiti), Magreth Mtaki (Katibu), na Wajumbe ni Richard Yomba, Haji Masasi, Jafari Chikoko na Gration Kaizirege.

Friday, 19 January 2018

Tigo yatangaza Zawadi Nono za Kili Marathon 2018

Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Mawasiliano ya simu za Mkononi ya Tigo Kanda ya Kaskazini, Henry Kinabo akizungumza wakati wa uzinduzi wa Msimu wa 16 wa Mbio za Kimataifa za Kilimanjaro Marathon 2018,Uzinduzi uliofanyika katika Hoteli ya Kibo Palace Homes mjini Moshi juzi, Mashindano ambayo Kampuni ya Tigo inadhamini Mbio za Nusu Marathon,Km 21. Pichani (mwenye kofia) Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira na wadau mbalimbali. (Na Mpigapicha Wetu).
Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Simu za mkononi ya Tigo imesema kuwa itadhamini tena mbio za nusu marathon za Kilimanjaro zitakazofanyika Machi 4 mjini Moshi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mbio hizo juzi, Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Mawasiliano ya simu za Mkononi ya Tigo Kanda ya Kaskazini, Henry Kinabo alisema wanadhamini tena mbio hizo kwa mwaka wanne mfululizo.

Kinabo alisema wanaunga mkono mbio hizo, ambazo zinasaidia kuibua na kuviendeleza vipaji vya vijana na kuhakikisha Watanzania wanaishi katika maisha ya kiafya kwa kushiriki katika mchezo huo wa riadha.

Alitaja zawadi, ambazo zitatolewa kwa washindi wa kwanza kwa upande wa wanawake na wanaume, kila mmoja ataondoka na kitita cha sh milioni 2.

Huku washindi wa pili kila mmoja tazawadiwa sh milioni 1 huku mshindi watatu ataondoka n ash 650,000, wanne sh 500,000, mshindi wa sita sh 325,000 wakati wasabi atapewa sh 250,000.


Alisema kuwa mshindi wanane ataondoka na kiasi cha sh 150,000, huku mshindi wa tisa atapewa sh 125,000 na wa 10 atabeba sh 100,000.

Simba yaikandamiza Singida United 4-0 Taifa

Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi (kushoto) akishangilia na mchezajui mwenzake wa timu hiyp, Asante Kwasi moja yamabao aliyofunga katika mchezo huo dhihi nya Singida United ya Singida. Simba ilishinda mabao 4-3, katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu
SIMBA ya Dar es Salaam, jana ilijikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuifunga Singida United kwa mabao 4-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.

Simba ilianza kuandika bao katika dakika ya tatu tangu kuanza kwa mchezo baada ya Shizza Kichuya kufunga baada ya kutuliza mpira na kuujaza wavuni kwa juu.

Dakika nne baadae, Nicolas Gyan nusura afunge, lakini akiwa katika nafasi nzuri,alipiga mpira nje.

Asante Kwasi akiichezea Simba kwa mara ya kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu tangu ajiunge nayo katika dirisha dogo la usajili akitokea Lipuli ya Iringa, alifunga katika dakika ya 24.

Wachezaji wa Singida walifikiri mfungaji atakuwa ameotea na kusita kumzuia na kupatikana kwa bao hilo.

Dakika ya 76 Emmanuel Okwi aliyeingia kipindi cha pili, aliifungia Simba bao la tatu na kuifanya timu hiyo kuzidi kuwa na uhakika wa kutoka na pointi zote tatu.

 Okwi ambaye alirejea juzi kutoka kwao Uganda, ambako alikaa zaidi ya muda alioruhusiwa, alifunga bao la nne baada ya kupata pasi kutoka kwa Ndemla baada ya kumkwepa kipa.

Kwa ushindi huo, Simba sasa imefikisha pointi 29 baada ya michezo 13 na kuiacha Azam FC ikisa ya pilina pointi zake 27 huku Yanga ikibaki katika nafasi ya tano kwa pointi zake 22.

Azam jana ilikalia kwa muda kiti cha uongozi wa ligi baada ya kutoka sare ya 1-1 na Majimaji ya Songea katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Majimaji, huku Yanga juzi ikilazimishwa suluhu na Mwadui ya Shinyanga kwenye Uwanja wa Taifa.

Kocha moya wa Simba, Mfaransa Pierre Lechantre akifuatilia mpambano wa Ligi Kuu ya Tanzania katika ya Simba na Singida United kwenye Uwanja wa Taifa. 
Ushindi huo ulishuhudiwa na kocha mpya wa Simba, Mfaransa Pierre Lechantre aliyekuwa jukwaani wakati timu hiyo ikitoa kipigo hicho.

Kwa mujibu wa taarifa ya Simba, klabu hiyo wakati wowote itaingia mkataba na kocha huyo aliyeipatia Cameroon ubingwa wa Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2000.

Vikosi vilikuwa, Simba: Aishi Manula, Nicholas Gyan, Asante Kwasi, Juuko Murdhid, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, James Kotei/Mohamed Ibrahim, Mwinyi Kazimoto, John Bocco, Shiza Kichuya na Mzamiru Yassin/Emmanuel Okwi.


Singida: Peter Manyika, Micahel Rusheshagonga, Shafik Batambuzi, Kenned Wilson, Maliki Antiri, Mudathir Yahya, Deus Kaseke, Tafwadza Kutinyu/Yusuph Kagoma, Lubinda Mundia/Kenny Ally, Kambale Salita na Kiggi Makasi/Elinywesia Sumbi.

Thursday, 18 January 2018

Kocha Aliyeipa Ubingwa Cameroon Atua Simba

Na Mwandishi Wetu
UONGOZI wa Simba SC umeamua kuachana na kocha Hubert Velud na kumchukua Mfaransa mwenzake, Pierre Lechantre.

Taarifa ya klabu ya Simba leo kwa vyombo vya Habari imesema kwamba, kocha huyo mzoefu ataanza kazi mara moja na atasaidiwa na kocha Mrundi, Masoud Juma ambaye amekuwa akiiongoza timu tangu Desemba mwaka jana alipoondolewa Mcameoon, Joseph Omog.

Taarifa hiyo imesema Lichantre amekuja na msaidizi mmoja, kocha wa viungo, Mmorocco Mohammed Aymen Hbibi na jioni ya leo ataishuhudia Simba ikicheza na Singida United kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Pierre Lechantre aliyezaliwa Aprili 2, mwaka 1950 mjini Lille, Nord, Ufaransa ni kocha aliyeipa Cameroon ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2000 na kabla ya kuanza kufundisha alikuwa mchezani pia.

Aprili 27 mwaka 2012, Lechantre alitambulishwa kuwa kocha Mkuu wa Senegal, lakini akashindwa kufikia makubaliano ya mwisho na Shirikisho la Soka la nchi hiyo.

Akiwa mchezaji katika nafasi ya ushambuliaji, Lechantre amechezea klabu za Paris FC (1986–1989), Red Star 93 (1983–1986), Stade de Reims (1981–1983), Olympique de Marseille (1980–81) na RC Lens (1979–80).

Zingine ni Stade Lavallois (1976–1979), AS Monaco (1975–76), FC Sochaux (1970–1975) na Lille OSC (1964–1970).

Na akiwa kocha amefundisha timu za taifa za Kongo (2016), Cameroon (1999-2001), klabu za Al-Ittihad Tripoli ya Libya kuanzia 2014 hadi 2015 na Al Arabi ya Qatar kuanzia Machi hadi September 2013.

Zingine alizowahi kuzifundisha ni pamoja na CS Sfaxien ya Tunisia kuanzia Juni hadi Desemba 2010, Club Africain ya Tunisia kuanzia Juni 10 mwaka 2009 hadi Aprili 2010 na Al Rayyan ya Qatar.

Amefundisha pia timu ya taifa ya Mali kuanzia Machi hadi Oktoba 2005, Al-Siliya Sports Club ya Qatar kuanzia Novemba 2003, Al-Ahli ya Jeddah kuanzia Agosti hadi Oktoba mwaka 2003, Qatar kuanzia Juni 2002, Le Perreux (1992–1995) na Paris FC (1987–1992).

Amewahi pia kuwa Mshauri wa Ufundi wa Val de Marne kuanzia Julai 7 mwaka 1995 hadi Januari 1999.

Na ujio wa kocha huyu unazima mpango wa kocha wa zamani wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Etoile du Sahel ya Tunisia, Mfaransa, Hubert Velud kujiunga na Simba.

Habari za ndani zinasema kwamba, Velud ni pendekezo la Mjumbe Mteule wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Mohammed Nassor ‘Mohaamed Kigoma’ ambaye alipambana mno klabu imchukue mwalimu huyo, lakini akakutana na upinzani mkali kutoka kwa Kaimu Rais, Salim Abdallah ‘’.

Wednesday, 17 January 2018

Okwi kuiongoza Simba Kuikabili Singida, Aomba Radhi Benchi la Ufundi na Viongozi kwa Utoro

Na Mwandishi Wetu
WAKATI Simba ikishuka dimbani leo kucheza na Singida United, mshambuliaji wake, Emmanuel Okwi ameomba radhi wachezaji wenzake, viongozi na benchi la ufundi baada ya kukosekana kwenye kikosi hicho kwa muda mrefu bila sababu za msingi.

Akizungumza jana Kocha wa Simba, Masoud Djuma alisema amemsamehe Emmanuel Okwi, kwani aliomba radhi kwake, kwa uongozi na wachezaji wenzake na juzi alianza rasmi mazoezi na timu.

“Unajua binadamu hakuna aliyekamilika cha lazima ni muunganiko wa pamoja, tukianza kunyoosheana vidole nguvu inapungua cha lazima ni kurudisha nidhamu kwenye timu. Hakuna mchezaji au mtu yeyote ambaye yuko juu ya timu, hata rais wa timu hayuko juu ya timu, timu inakuja kwanza halafu mtu baadaye,” alisema Masoud.

Pia Masoud amemuombea radhi Emanuel Okwi kwa mashabiki, akiwataka kuungana ili timu ifanye vizuri katika mchezo wa leo dhidi ya Singida United na michezo ijayo.

Simba ambayo ilikuwa imeweka kambi mkoani Morogoro,  ilirejea Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wa leo dhidi Singida United utakaochezwa kwenye wa Taifa.

Mchezo huo unachezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam baada ya serikali kuruhusu kutumika kwa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara na zile za kimataifa zilizo chini ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).


Okwi amekuwa na tabia ya kuchelewa kurudi kundini mara anaporuhusiwa kwenda kwao Uganda kutatua matatizo ya kifamilia au anapoitwa katika timu yao ya taifa, The Cranes, ambapo amekuwa akilalamikia na uongozi pamoja na benchi la ufundi kwa kuvuruga ratiba ya mazoezi.