Monday, 2 April 2018

Zawadi Zaongezwa Ngorongoro Marathon 2018


Na Mwandishi Wetu
WAANDAAJI wa Ngorongoro Marathon 2018 wameongeza zawadi kwa washindi wa mbio hizo, zitakazofanyika Aprili 21, imeelezwa.

Mkurugenzi wake, Meta Petro alisema juzi kwa njia ya simu kuwa, sasa wameandaa zawadi kuanzia mshindi wa kwanza hadi wa 15 katika mbio za kilometa 21 wakati awali wanariadha wanne bora ndio walikuwa wakipewa zawadi.
 
Petro alisema kuwa lengo lao ni kuhakikisha wanatoa zawadi hadi kwa mwanariadha akayemaliza katika nafasi ya 50 ili kuhakikisha mbio hizo zinakuwa na ushindani wa hali ya juu zaidi kutoka kwa washiriki.

Alisema zawadi hizo zitatolewa kwa washindi wakike na kiume huku katika mbio za kilometa tano, ambazo katika mbio nyingi huwa ni za kujifurahisha na hazina zawadi, wenyewe watatoa zawadi hadi kwa washindi 15 wa kwanza.

Akielezea maboresho hayo, Petro alisema kuwa, kwa upande wa watoto wadogo, ambao watachuana katika mbio za kilometa 2.5, zawadi zimeongezwa hadi kwa mtu atakayemaliza katika nafasi ya 15 badala ya wale wanne wa kwanza.

Alisema kuwa kwa uoande wa kilometa 21 kwa wanaume na wanawake, mshindi wa kwanza ataondoka na Sh milioni 1, wakati wa pili Sh 500,000 wa nne Sh 100,000, watano Sh 80,000, wa sita Sh 70,000, wa saba Sh 60,000, wa nane 50,000, wa tisa Sh 40,000 na wa 10 Sh 30,000.
 
Washindi wa 11 na 12 kila mmoja atapewa Sh 30,000 wakati wa 13 hadi 15 kila mmoja ataondoka nakifuta jasho cha Sh 20,000.

Alisema kuwa kwa upande wa kilometa tano, mshindi wa kwanza ataondoka na Sh 200,000 wakati wa pili atapewa 100,000 huku yule atakayemaliza watatu atapata Sh 50,000 huku wa nne Sh 30,000 na watano Sh 20,000, na wa sita hadi wa 15 kila mmoja atapewa Sh 10,000.
 
Kwa watoto, mshindi wa kwanza atapewa Sh 50,000 wakati yule wa pili ataondoka na Sh 40,000 huku wa tatu atabeba Sh 30,000, wa nne na tano kila moja atapata Sh 20,000, wa sita Sh 15,000, wa saba hadi wa 12 kila moja atajiondokea na Sh 10,000, wa 13 hadi wa 15 kila moja atapewa Sh 5,000.

Mbio hizo zinadhaminiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro  (NCAA) pamoja na Bonite Bottlers, ambapo Petro amezitaka taasisi binafsi pamoja na zile za Serikali na watu binafsi kujitokeza kudhamini mbio hizo zenye kauli mbiu ya `Kimbiza Jangili’.

No comments:

Post a Comment