Na Mwandishi Wetu
PASAKA imekuwa chungu kwa Yanga baada ya kutupwa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho
la Azam dhidi ya Singida United kwa kuchapwa mikwaju ya penalti 4-2.
Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida, ilimalizikakwa timu hizo kufungana bao 1-1 katika muda wa kawaida na ndipo ilipoamuliwa ipigwe
mikwajua ya penalti na Yanga kulala kwa matokeo hayo.
Papy Tshishimbi
na Emanuel Martin ndio waliokosa penalti
hizo kwa upande wa Yanga, huku nahodha Kelvin Yondani na Gadiel Michael wakipata
mikwaju yao.
Kipa wa Yanga,
Youthe Rostand alipangua mkwaju wa Malik Antil, lakini akashindwa kufanya hivyo
kwa mikwaju iliyopigwa na Shafiq Batambuze, Tafadzwa Kutinyu, Kenny Ally na
Elinyeswia Sumbi au Msingida.
Katika mchezo huo
uliokuwa mgumu kwa timu zote mbili kutokana na kila upande kuwa na uhitaji wa
kutinga hatua inayofuata, kipa upande ulitawala katika kila kipindi, Yanga
ikitawala kipindi cha kwanza na Singida cha pili.
Yanga ilikuwa ya
kwanza kupata bao la kuongoza katika dakika ya 23 bao lililofungwa kwa kichwa
na winga Yusuph Mhilu baada ya kutumia kona safi iliyopigwa na Ibrahim Ajib.
Hali ya uwanja
kujaa maji ilisababisha timu zote kucheza mpira wa pasi ndefu ambazo hata hivyo haikuwa na faida kwa timu zote
mbili ingawa kwa Singida ilionekana kuwanufaisha kwa mipira ya kona ambazo hata
hivyo hazikuwa na faida kwao.
Bao la Yanga
lilidumu mpaka mapumziko na Singida ilisawazisha dakika ya kwanza ya kipindi
cha pili kupitia kwa kiungo Kenny Ally baada ya kupokea pasi safi
kutoka kwa Kigi Makasi.
Baada ya hapo
Yanga ilionekana kutulia na kutafuta bao ambalo lingeweza kuwavusha katika
hatua nyingine hata hivyo pamoja na kufanya mabadiliko kadhaa hawakufanikiwa na
kadri muda ulivyokuwa ukienda Singida walionekana kuimarika zaidi na kujipanga
kuongeza bao.
Singida ilitaka
kudhihirisha uimara wake kufuatia mashambulizi mfululizo waliyokuwa wakifanya
langoni mwa Yanga,ingawa umahiri wa
Yondani na Andre Vincent uliwapa faida Yanga baada ya kutulia dakika
zote 90.
Dakika ya 78
Yanga ilianza kutulia tena baada ya kufanikiwa kudhibiti mashambulizi wa
wapinzani wao ambapo dakika tano baadaye Juma Abdul alitolewa na nafasi yake
kuchukuliwa Hassan Kessy, hata hivyo bado ngoma ilikuwa ngumu mpaka dakika 90.
Kwa matokeo hayo
Singida itacheza hatua ya nusu fainali na JKT Tanzania wakati Stand United
iliyoitoa Njombe FC itaumana na Mtibwa Sugar iliyoitoa Azam, katika nusu fainali nyingine.
No comments:
Post a Comment