Sunday 25 August 2019

DStv Yafyeka Bei za Vifurushi Vyake!

Wateja kuendelea kushuhudia burudani kabambe kwa bei ‘mtelezo’!
Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania, Jacqueline Woiso (kulia) akimkabidhi zawadi mchezaji wazamani wa Simba, Dua Said wakati wa hafla ya uzinduzi wa Ligi Kuu za Ulaya, katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
 Na Mwandishi Wetu
DStv Tanzania imethibitisha rasmi kupunguza kwa kiasi kikubwa ada ya mwezi ya vifurushi vyake kuanzia Septemba mosi mwaka huu.

Mabadiliko hayo yanakuja muda mfupi tu baada ya kuanza kwa msimu wa soka, ambapo ligi kubwa maarufu diniani zimeanza, hivyo kuwawezesha wateja wa DStv kushuhudia ligi hizo kwa bei nafuu kabisa.

Akithibisha punguzo hilo la bei, Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania, Jacqueline Woiso amesema kuwa muda wote wamekuwa wakisikiliza maoni ya wateja wao na moja ya mambo wateja waliyoshauri ni kupunguzwa kwa bei za vifurushi.

“Wateja ndiyo moyo wa biashara yetu na muda wote tunawasikiliza na kutekeleza maoni yao pale inapowezekana. Kwa msingi huu, tumeamua kupunguza bei ili wateja wetu waendelee kufurahia burudani kabambe kwa bei nafuu zaidi, “ alisema Jacqueline.
Mchezaji wazamani wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, Edibily Lunyamila akizungumza hivi karibuni. Kulia ni mchezaji mwenzake wazamani wa Yanga na timu ya taifa, Sekilojo Chambu.
Amezitaja bei hizo mpya kuwa kifurushi cha DStv Premium kutakuwa na punguzo la Sh 40,000 kutoka bei ya sasa ya Sh 169,000 hadi 129,000; Kifurushi cha DStv Compact+ punguzo la Sh 25,000 kutoka 109,000 hadi 84,000;  Kifurushi cha DStv Compact punguzo la Sh 25,000 kutoka 69,000 hadi  44,000; na kifurushi cha DStv Family punguzo la Sh 10,000 kutoka 39,000 hadi 29,000.

Kuhusu vifurushi maalum, Jacqueline amesema kifurushi chenye nyongeza maalum ya chaneli za Asia - DStv Premium+Asia Addon kitapungua kwa shilingi 40,000 kutoka 220,050 hadi 170,050 wakati kile chenye chaneli za ziada za Kifaransa DStv Premium+French addon nacho pia kitapungua kwa 40,000 kutoka 259,000 hadi 2019,000.
Mkurugenzi huyo amewahakikishia wateja wa DStv kuwa kushuka huko kwa bei hakutasababisha mabadiliko wa chaneli katika vifurushi hivyo mteja ataendelea kupata chaneli zile zile alizokuwa akipata awali ila sasa atakuwa analipa bei ndogo zaidi.

Friday 16 August 2019

Mabalozi Tanzania Nje Wamwagia Sifa Terminal 3

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Julius Ndyamukama akitoa maelezo kwa mabalozi wanaowakilisha Tanzania nje ya nchi wakati walipotembelea Jengo la Tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam leo. Kulia kwa Ndyamukama ni Mtendaji Mkuu wa Tanroad, Patrick Mfugale. 

Na Mwandishi Wetu
MABALOZI 42 wanaowakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani wamelimwagia sifa Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA).

Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dk Wilbroad Slaa akizungumza kwa niaba ya wenzake baada ya kutembelea jengo hilo jana, alisema jengo hilo ni kioo cha nchi  na ndipo wageni wengi wa nje ya nchi ndio wanafikia, ni kivutio kizuri.

 “Hapa (JNIA) ni kioo cha nchi. Tukiharibu mambo kwa kutoweka kaunta nzuri, tunaharibu taswira ya nchi. Hii ndiyo Dubai (Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) yetu. Lazima izingatie viwango vya kimataifa, “alisema Slaa huku akisisitiza kutoogopa kujifunza kutoka nje.

Komba akiwaonesha mabalozi wanaowakilisha Tanzania nje ya nchi walipotembelea Jengo la Tatu la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).

Alaa alitakiwa kutoa shukrani kwa niaba ya wenzake na Mkuu wa Msafara huo wa mabalozi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ramadhan Mwinyi.
Dk. Slaa aliishukuru serikali kwa kuwapa mabalozi hao fursa ya kutembelea jengo hilo kujionea kazi nzuri ya serikali ya awamu ya tano iliyomalizia ujenzi wa jengo hilo.

Alisema kiwanja cha ndege ni sehemu ya kuingilia nchini na kama kina huduma na vifaa bora, kama ulivyo huo wa JNIA Terminal 3 utashawishi watu wengi kuingia nchini kupitia lango hilo.

Jengo hilo lina uwezo wa kupokea abiria milioni 6 kwa mwaka wakati lile la Terminal 2 lina uwezo wa kuchukua watu milioni 2 tu, hivyo ni hatua kubwa imepigwa kuhakikisha wasafiri wanahudumiwa kwa haraka na kwa muda mfupi, tofauti na huko nyuma.
Awali, akizungumza wakati akiwakaribisha mabalozi hao ambao wako nchini kuhudhuria mkutano wa Sadc Mkurugenzi Mkuu wa Viwanja vya Ndege nchini, Julius Ndyamukama alisema tayari makampuni 29 kati ya 41 ya usafi yanaendelea na huduma mengi yao yakiwa ni ya wazawa.

Mabalozi hao walitembezwa kuanzia sehemu ya mwanzo ya ukaguzi, sehemu ya uhamiaji, kuondokea abiria, daraja la kuingilia ndani ya ndege, sehemu ya kufikia abiria na sehemu ya mizigo kabla ya kutoka nje ya kiwanja hicho.
Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Dk Asha Rose Migilo alimwambia mwandishi wetu kuwa kutokana na kazi nzuri wanayofanya mabalozi nje ya nchi, watu wengi wakiwemo watalii wanataka kutembelea Tanzania, hivyo kiwanja hicho kinaendana na wakati.
Alisema uwezo wake wa kuchukuwa watu wengi kwa wakati mmoja, huduma kiwanja hicho kina hadhi ya hali ya juu na itasaidia sana kupokea watu hao na kuwapokea bila tatizo.

Wednesday 14 August 2019

Bodystreet Kumdhamini Masomo Ujerumani Mchezaji Tanzanite


Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi akifanya mazoezi katika Gym ya Bodystreet iliyopo jirani na Makao Makuu ya Airtel Morocco jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Bodystreet, Emma Lehner Lyayuka akifuatilia mazoezi hayo leo.

Na Mwandishi Wetu
GYM ya kisasa nchini ya Bodystreet imempatia ofa ya masomo nchini Ujerumani mchezaji bora wa mashindano ya Kombe la Cosafa 2019 kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 iliyomalizika wiki iliyopita nchini Afrika Kusini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mtendaji Mkuu na muanzilishi wa Bodystreet hapa nchini, Emma Lehner Lyayuka alisema kuwa wameamua kumpatia Enekia Kasonga ofa ya masomo nchini Ujerumani.

Pia mbali na kusoma masomo hayo ya michezo, pia atakuwa akicheza soka katika timu ya wanawake ya FFC Wacker München  ya Munich, Ujerumani katika kipindi chote atakachokuwa akisoma.

Kasonga ambaye anaichezea Alliance Queens ya Mwanza, alikuwa mchezaji bora katika mchezo wa Tanzania (Tanzanite) dhidi ya Afrika Kusini, ambapo Tanzania ilishinda 2-0 na yeye alifunga bao moja. Pia alifunga jumla ya mabao manne katika mashindano hayo.
Pia mchezaji huyo alifunga bao pekee la Tanzania wakati ilipofungwa 2-1 na Zambia katika hatua ya makundi na kuifanya kumaliza ya pili na kutinga nusu fainali.

Lyayuka alisema kuwa walimuona Enekia katika mchezo wa Tanzanite na Afrika Kusini wa Kombe la Cosafa na walivutiwa sana jinsi alivyokuwa akicheza na kuisaidia Tanzania kutwaa ubingwa wa mashindano hayo kwa mwaka huu.

Alisema wanafanya mawasiliano na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili kukamilisha taratibu mbalimbali za kumuwezesha mchezaji huyo kwenda kusoma Ujerumani mafunzo ya kuanzia miezi mitatu hadi mwaka.

Wakati wa kutangaza ofa hiyo, Bodystreet waliwaonesha waandishi wa habari vifaa vya teknolojia ya kisasa vya kufanyia mazoezi, ambavyo ni vya kwanza kuwepo nchini.

Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Filbert Bayi alifanyishwa mazoezi kupitia vifaa hivyo, ambapo alikiri kuwa vinabana muda na mtu anafanyishwa mazoezi katika viungo vyote.

Bayi alisema kuwa gym hiyo inasaidia sana kubana muda kwani mtu hatumii muda mwingi, lakini mwili mzima unafanyishwa mazoezi kutokana na kizibao anachokivaa wakati wa mazoezi.
Juhudi za kuwapata viongozi wa Alliance na TFF ili kuzungumzia ofa hiyo jana hazikufanikiwa baada ya baadhi yao simu zao kutopatikana kabisa na wengine ziliita bila majibu.

Thursday 8 August 2019

TAA Yawahakikishia SADC Huduma Bora

Raia wenye Asili ya Asia, kuanzia kulia Cuco Donny, Dorony Mnarty na Zohra
Lukmanji leo wakimsikiliza Kaimu Meneja Biashara wa Kiwanja cha Ndege cha 
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bi. Herieth Nyalusi (kushoto), 
walipotembelea maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo 
Kusini Mwa Afrika (SADC) katika Banda la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania 
(TAA), kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. Maonesho hayo 
yamefungwa leo na Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein.
Kaimu Meneja Biashara, Bi. Herieth Nyalusi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (wa kwanza kulia), akitoa  maelezo mbalimbali kwa Bw. Mohamed Issa alipotembelea maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) katika Banda la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) waliopo kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. Maonesho hayo yamefungwa leo na Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein.
 Mzee Iluganyuma (kulia) leo akimsikiliza Kaimu Meneja Biashara wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) Bi. Herieth Nyalusi alipotembelea maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) katika Banda la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) waliopo kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. Maonesho hayo yamefungwa leo na Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein.
Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bahati Mollel akitoa maelezo mbalimbali kwa Wilson Ishengoma (kulia) na watoto wake walipotembelea Banda la maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kwenye viwanja vya Karimjee. Maonesho hayo yamefungwa leo na Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein.


Friday 2 August 2019

DStv Yazindua `Soka Mwaa...Mwiii..’!

Mkurugenzi Mtendaji wa Multchoice-Tanzania, Jacquline Woiso (kulia) akimkabidhi zawadi mchezaji wazamani wa Simba, Dua Said wakati wa hafla ya uzinduzi wa Msimu Mpya wa Ligi za Ulaya, jijini Dar es Salaam leo. 

Na Mwandishi Wetu
WACHEAJI nyota wazamani wa Tanzania leo walipamba uzinduzi wa msimu mpya wa mechi za Ligi mbalimbali za Ulaya, ambazo zitaoneshwa na DStv katika hafla hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya nyota hao waliowahi kutamba katika soka la Bongo ni pamoja na Edibily Lunyamila, Sekilojo Chambua, Fikiri Magoso, Dua Said na wengineo, ambao waliipongeza channel hiyo kuonesha ligi hizo.

Pazia la Ligi Kuu ya England msimu wa mwaka 2019/2020 linafunguliwa rasmi kesho Jumapili kwa mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Manchester City na Liverpool utakaoneshwa moja kwa moja na DStv.

Kwa mujibu wa  Mkuu wa Masoko wa Kampuni ya Multchoice, Ronald Shelukindo, DStv wataanza kuonesha kipute hicho cha Ngao ya Jamii na baadae kuendelea na ligi zingine zote kubwa Ulaya, zikiwemo za Hispania (La Liga), Italia (Serie A) na zinginezo.

Alisema: “ Soka Mwaa…Mwiii…Ndani ya DStv, yaani wananchi watapata soka mwanzo mwisho mechi kibao.”

 Alisema pia DStv itaendelea kurusha hewani Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na Ligi ya Ulaya pamoja na ligi zingine kubwa, ambazo zinafuatiliwa na watu wengi.
Wachezaji wazamani wa Tanzania (mstari wa nyuma waliosimama) wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Multchoice-Tanzania, Jacquline Woiso (watatu kushoto mstari wa mbele) pamoja na wachambuzi wa soka katika hafla jijini leo.
Shelukindo alisema DStv itahakikisha wateja wake wote wanaendelea kuliona soka katika muonekano bora zaidi, huku wakipata matangazo hayo ya Ligi Kuu ya England kwa lugha ya Kiswahili.

“Kampeni yetu ya sasa tunasema ni ‘Soka Mwanzo Mwisho’ na tunamaanisha kwani kwa wateja wetu wa DStv, burudani ya soka haitawatindikia kamwe! 

Ni wapi unaweza kuona mechi zote 380 za ligi ya Uingereza, mechi  380, za Ligi Kuu ya Hispania, mechi 380 za Ligi Kuu ya Italia bila kusahau mechi  za ligi ya mabingwa Ulaya na nyingine nyingi?  Bila shaka ni DStv pekee. Ndiyo sababu tunasema kwetu DStv ni Soka Mwanzo Mwisho!”
Mchezaji wazamani wa Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars, Edibily Lunyamila akzungumza wakati wa hafla hiyo leo. Kulia ni mchezaji mwenzake wazamani wa Yanga na Taifa Stars, Sekilojo Chambua. 
Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na wadau wa soka nchini wakiwemo wasanii mbalimbali, wachezaji wazamani na watangazaji wanaotangaza Ligi Kuu ya England kwa Kiswahil, ambao ni Salama Jabir, Edo Kumwembe, Maulid Kitenge, Ibrahim Masoud (Maestro), Abuubakar Lyongo na Oscar Oscar.

Thursday 1 August 2019

Jengo la 3 la abiria JNIA kuongeza chachu ya Uchumi


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na viongozi mbalimbali akikata utepe kuashiria kufungua rasmi Jengo la Tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Agosti 1, 2019
Na Mwandishi Wetu
JENGO la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB III) litaongeza chachu ya kukua kwa uchumi wa nchi, imeelezwa.

Hayo yamesemwa leo na Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipozindua jengo hilo, ambalo sasa limeanza kutumika kwa safari za nje ya nchi baada ya kukamilika kwake.

Rais Magufuli amesema mbali na jengo hilo litatoa ajira mbalimbali kwa wazawa, pia litaruhusu wananchi kuwekeza katika huduma mbalimbali ndani na nje ya jengo hilo, ambapo ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhakikisha Wazawa wanapewa kipaumbele katika uwekezaji katika jengo hilo.
Rais Dk John Pombe Magufuli na Viongozi wa dini, Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeiry bin  Ally na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Muadhama Polycarp Kardinali Pengo na viongozi wengine wakifunua pazia kama ishara ya ufunguzi rasmi wa Jengo la Tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam leo Alhamisi Agosti 1, 2019
“Serikali inaimarisha usafiri wa anga kwa kununua ndege pamoja na kuimarisha miundombinu ya viwanja vya ndege, ambapo serikali inampango wa kukarabati na kujenga viwanja 15 nchini kikiwepo cha Kimataifga cha Msalato Dodoma, ili kuendelea kuufanya usafiri huu uendelee kuwa wa haraka na salama, ambapo utachangia kukuza pato la taifa kwa watumiaji wake, ambao kwa sasa abiria wameongezeka kwa asilimia 12 kwa mwaka,” amesema Mhe. Rais.

Amesema anaimani idadi ya abiria wa ndege wataongezeka zaidi kutokana na utalii unakwenca sambamba na usafiri wa anga, kutokana na Watalii wengi huja nchini kwa kutumia usafiri wa anga.

Hatahivyo, ameipongeza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, pamoja na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kwa kufanikisha kukamilika kwa mradi huo mkubwa wa jengo hilo, ambao mwaka 2016 ulisuasua kutokana na kukosekana kwa fedha za kuendelea na mradi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo na Wafanyakazi wa Benki ya NMB, ambao wanatoa huduma ya kubadilisha fedha ndani ya Jengo la Tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, ambalo amezindulia leo Agosti 1, 2019
Amewataka Watanzania kulipa kodi ili serikali iweze kukamilisha mapema kwa wakati miradi mikubwa, ambayo itakuja kuwanufaisha na kuwapa heshima kubwa.

“Miradi inawezekana kwani fedha nyingi zilikuwa zikitumiwa na mafisadi, hivyo nawataka tulipe kodi ili kufanikisha miradi yote, na tuachane na dhana ya wafadhili ambao wamekuwa na masharti,” amesema Mhe. Rais.

Hatahivyo, amewataka watumiaji wote wa Jengo hili kuhakikisha wanalitunza na wasiliharibu kutokana na kujengwa kwa fedha nyingi za Watanzania.

Katika hatua nyingine amempongeza Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Jakaya Kikwete aliyeanzisha ujenzi wa mradi wa Jengo la Tatu la abiria, na pia amewashukuru viongozi wa Dini nchini kuendelea kuliombea taifa.

Naye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema kutokana na ongezeko la mara kwa mara la abiria, sasa Jengo la pili la abiria (JNIA-TBII) linaboreshwa na kukarabatiwa ili liweze kuhudumia abiria mara mbili ya sasa ambao ni Milioni 1.5 kwa mwaka.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli (aliyenoosha kidole) wakati wakipata maelezo mbalimbali kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), ,Mhandisi Julius Ndyamukama (kulia) mara baada ya kuzindua rasmi Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, leo Agosti 1, 2019
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patric Mfugale, ambao ndio walikuwa wasimamizi wa mradi huu wa kimkakati amesema jengo hili limekuja wakati muafaka kutokana na wananchi kuwa na mwamko wa kupanda ndege, ambapo kumekuwa na ongezeko la abiria, ambapo kwa sasa kati ya ndege 23 za nje tayari 18 zimeanza kutumia jengo hili.   

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mhandisi Julius Ndyamukama amesema TAA wapo tayari kuendesha huduma kwenye jengo hilo, ambapo wamefanya majaribio kadhaa ya ndege, ambapo tarehe 17 Julai, 2019 walianza na ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), iliyokuwa ikizindua safari yake ya kwanza kwenda nchini India.

Kwa upande wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai amesema jengo hili la kisasa linaitoa Tanzania kimasomaso, kutokana na ukubwa na ubora wake.

“Nipo hapa kuwawakilisha Wabunge, ambapo tunaona fedha tunazopitisha zinatumika kihalali na tutaendelea kumuunga mkono Mhe. Rais katika jitihada zake za kuendeleza na kuanzisha miradi mbalimbali,” amesema Mhe. Spika.

Naye Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma ame wataka wananchi kuhakikisha wanatatua migogoro yao ya ardhi inayohusisha ujenzi wa miradi mbalimbali nje ya mahakama, ili kufanikisha miradi hiyo kumalizika kwa wakati.