Bingwa wa mchezo wa baiskeli kwa wanaume,
Chaptele Muhumba (aliyenyoosha mkono) wa Uchukuzi akiwa na wasindikizaji wake
mara baada ya kumaliza mbio za kilometa 20 zilizoanzia eneo la Mizani Ndolela
mkoani Iringa leo, ikiwa ni michezo wa kombe la Mei Mosi inayoendelea mkoani
hapa. Mshindi alitumia dakika 32:18. (Picha Zote na Bahati Mollel wa TAA).
Na Bahati Mollel-TAA, Iringa
TIMU
ya Uchukuzi imetwaa ubingwa wa mchezo wa baiskeli wa kilometa 20 kwa wanawake
na wanaume baada ya wachezaji wake Chaptele Muhumba na Scolastica Hasiri
kuibuka washindi, katika michuano ya Kombe la Mei Mosi inayoendelea mkoani
Iringa.
Mbio
hizo zilizoanzia eneo la mizani Ndolela na kuishia FFU, ambapo Muhumba
alimaliza baada ya kutumia muda wa dakika 32:18; huku Scolastica akimaliza kwa
dakika 53:44.
Ushindi
wa pili kwa wanaume ulichukuliwa na Nehemia Jonnas wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) aliyemaliza kwa muda wa dakika 41:44 na mshindi wa tatu ni
Stanley Umbe wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa dakika 46:51.
Aliyeshika nafasi ya nne ni Roman Steven wa MUHAS aliyetumia saa 1:12.40 na wa
mwisho ni John Fataki wa Ikulu.
Kwa
upande wa wanawake mshindi wa pili Happy Mwanga wa Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco) alitumia muda wa saa 1:23.33 na wa tatu ni Severina Mnyaga wa MUHAS alitumia
muda wa saa 1:38.00.
Katika
mchezo wa netiboli, timu ya Ikulu iliwaadhibu Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco) kwa kuwafunga magoli 70-4 katika mchezo uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki
(RUCU).
Washindi
walikwenda mapumziko wakiwa mbele kwa magoli 33-2. Mfungaji Fatuma Machenga wa
Ikulu ndio aliyefunga magoli yote 70, huku kwa upande wa Tanesco yamefungwa na
Imelda Hango.
- Mlinzi Jacky Sanga (WD) wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) akijitahidi kuzuia mpira uliorushwa na Fatuma Fusi (WA) wa Ikulu katika mchezo wa netiboli wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika leo kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCU) mkoani Iringa. Ikulu wameshinda kwa magoli 70-4.
Katika
mchezo wa soka nao ulifanyika leo kwenye uwanja wa Samora, mabingwa watetezi
timu ya Geita Gold Mine (GGM) wameendelea kugawana pointi na wapinzani wao
ambapo wamelazimishwa sare na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya bao 1-1.
GGM
ndio walikuwa wa kwanza kupachika bao katika dakika ya 27 lililofungwa na
Mohamed Salum, lakini TRA wakasawazisha kwa njia ya penalti kupitia kwa
Boniface Emmanuel katika dakika ya 52.
Wakati
huohuo, michuano hiyo ya Mei Mosi yenye kaulimbiu “Tanzania ya Viwanda Swadakta… kwa Ukuzaji wa Ajira Sambamba na Uhamasishaji wa Michezo Kazini”,
inafunguliwa rasmi kesho tarehe 23
April, 2018 na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, ambapo zaidi ya timu
12 zinashiriki katika michezo ya netiboli, soka, karata, bao, draft, baiskeli
na riadha.
No comments:
Post a Comment