Viongozi wapya wa Tughe tawi la Makao Makuu ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, TAA. |
Na Mwandishi Wetu
TAWI la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya
(TUGHE) la Makao Makuu ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA-HQ),
limepata viongozi wake wapya katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni kwenye
ukumbi wa Transit uliopo katika jengo la Kiwanja cha Ndege cha Zamani (TBI).
TAA ni wakala wa Serikali iliyoanzishwa tarehe 29
Novemba 1999 kwa Tangazo la Serikali Na.404 la mwaka 1999 chini ya kifungu cha
3 cha Sheria Na. 30 ya mwaka 1997 ya Wakala wa Serikali. Wakala hii ilirithi
majukumu ya iliyokuwa Idara ya Viwanja vya Ndege (Directorate of Aerodromes)
chini ya Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, ulizinduliwa rasmi mnamo tarehe 3
Desemba 1999.
Viongozi hao wamepatikana baada ya uliokuwepo
kumaliza muda wao, na waliochaguliwa katika
uchaguzi huo uliosimamiwa na Katibu Mkuu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Gaudence
Kadyango, ni pamoja na Mwenyekiti Bw. Nasib
Elias aliyezoa kura zote 28, baada ya kutokuwa na mpinzani, huku katibu mkuu akichaguliwa
Bi. Aziza Kipande aliyepata kura 15 akimshinda Bi. Caroline Mntambo aliyepata
kura 13.
Wajumbe watatu ambao ni Bi. Mwanaisha Omari, Bw. Joel
Mwakamele na Bi. Frida Omari walipitishwa bila kupingwa na wajumbe waliotoka
idara mbalimbali za TAA HQ.
Naye Bi. Irene Sikumbili alipata kura zote 14 za
wanawake na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake na Katibu Mkuu
wake ni Bi. Mwanahawa Mdee aliyepata kura 11 akimshinda Bi. Kipande aliyepata
kura tatu.
Walioshinda katika nafasi ya ujumbe katika kamati hiyo ni Bi. Glory Mollel
na Bi. Pendo Pascal; wakati Bi. Mntambo ameukwaa uhazini na Bi. Magreth Mushi
ni mwakilishi wa vijana, huku hakukuwa na mwakilishi wa walemavu kutokana na
kutokuwa na mlemavu.
Naye mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu Bw. Abdi Mkwizu aliwapongeza
viongozi wateule wa TUGHE na kuwaahidi ushirikiano mzuri kutoka upande wa
mwajiri.
Katika kutoa neno la shukrani kwa wajumbe, Mwenyekiti
Bw. Elias aliwashukuru wajumbe wote kwa kuonesha imani yao ya dhati kwake na
kuwaahidi kuendeleza mshikamano na mahusiano mema yaliyojengwa na uongozi
uliomaliza muda wake baina ya wafanyakazi na mwajiri, lakini pia baina ya
wafanyakazi wenyewe.
Bw. Elias pia ameahidi kuhakikisha wafanyakazi ambao
si wanachama wa TUGHE wanajiunga na chama hicho kwani kina manufaa makubwa kwao yakiwemo ya
kutetewa pindi mfanyakazi anapokuwa kwenye matatizo na mwajiri wake .
Naye msimamizi, Bw. Kadyango ambaye aliukabidhi
uongozi mpya Katiba, aliwashukuru wajumbe wote kwa kumaliza zoezi la uchaguzi
kwa amani na kusisitiza kuwa na ushirikiano mzuri na mwajiri, kudumisha
uhusiano mwema kazini kati ya waajiri na waajiriwa, kudumisha uhusiano mwema
baina ya wafanyakazi wao kwa wao, kusimamia uboreshaji wa maslahi ya wafanyakazi
na hali bora za kazi, ili kufikia malengo.
IMETOLEWA
NA KITENGO CHA SHERIA NA MAHUSIANO TAA
No comments:
Post a Comment