Sunday 30 September 2018

“TAA KUIFUNGUA TANZANIA KWA ULIMWENGU”


1.        Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (kushoto) akiongea na waandishi kuhusiana na viwanja vya ndege kuchagiza uingiaji wa watalii nchini. Kulia na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Prof. Audax Mabula. 

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imejipanga kupitia kaulimbiu yake `kuifungua Tanzania kwa ulimwengu' kupitia sekta ya Utalii nchini, kwa kuimarisha usafiri wa anga ili kuhakikisha watalii wote wanafikia vivutio vyote vya utalii kwa haraka zaidi.

Hayo yamebainishwa juzi na Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela alipokuwa akizumgumza na waandishi wa habari siku ya ushiriki wa Mamlaka katika Tamasha la Urithi Wetu linaloanza leo Jumatatu (Oktoba Mosi, 2018) kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

"Viwanja vyetu vya ndege ndio milango mikuu wa watalii kupita, hivyo tupo hapa kuwaambia wananchi, wadau pamoja na Jumuiya za Kimataifa kwamba sasa kuna fursa ya kutanganza vivutio vya kitalii kupitia viwanja vyetu vya ndege kwa kuwa vinatumika kwa usafiri wa anga lakini pia tunaweza kuvitumia kibiashara kwa kutangaza vivutio vyetu" alisema Bw. Mayongela.

Bw Mayongela pia amewapa wito Watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii kutangaza vivutio vilivyopo kupitia Viwanja vya ndege lakini pia kuwaeleza wadau kwa njia mbalimbali zilizopo Tanzania ili watalii wanapowasili waweze kupata picha halisi ya maeneo ya kutembelea akiwa nchini.

Aidha Bw. Mayongela ameongeza kwamba Mamlaka ina mtandao mkubwa na inasimamia viwanja 58 vilivyopo chini ya serikali, ambavyo vipo kila sehemu penye vivutio vya utalii na wamejiimarisha kuhakikisha huduma bora ya usafiri wa anga.

"Sehemu ya Kaskazini mwa nchi yetu ambapo ndio kuna vivutio vingi, vipo viwanja vya ndege vya kutosha, tuna Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA), Kiwanja cha Lake Manyara ambacho kimejengwa kwa mkakati wa kutumika kwa watalii na kinafanya vizuri sana kwa kuingiza watalii wengi, vilevile tuna mpango wa kujenga kiwanja kipya katika Mkoa wa Manyara,” alibainisha Bw. Mayongela.

Akizungumzia miundombinu ya Viwanja vya Ndege kwa Kanda ya Kusini ameeleza kwamba serikali imejitoa kufanya maboresho ya kiwanja cha Mtwara kwa lengo moja kuu la kuvutia watalii wengi zaidi ili waweze kushuhudia vivutio vya utalii vilivyopo maeneo hayo.

“Serikali inaboresha kwa kufanya upanuzi na ukarabati mkubwa wa Kiwanja Cha Ndege cha Mtwara, pamoja na sababu za kiuchumi lakini pia lengo ni kuvutia watalii wengi zaidi ili waweze kushuhudia vivutio vilivyopo, sio hivyo tu lakini pia Kilwa masoko tuna kiwanja, Lindi tuna kiwanja, Nachingwea mpaka Masasi kote tuna viwanja” Alisema Bw. Mayongela.

Akizungumzia upande wa nyanda za juu Kusini Bw. Mayongela amebainisha kwamba baada ya ukarabati mkubwa kukamilika kutakuwa na kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Songwe, Njombe mpaka Iringa kutakuwa na viwanja vizuri vya ndege ili kuhakikisha kwamba vivutio vilivyopo Tanzania vinafikika kwa urahisi.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Prof Audax Mabula ameeleza kwamba Tamasha la Urithi Wetu lililobuniwa na Wizara ya Maliasili na Utalii lina madhumuni makuu mawili ikiwemo ya kuwezesha kuonyesha fursa zote zinazoizunguka tasnia hii.

“Madhumuni makuu ni kuendeleza, kutambua na kuhifadhi urithi wetu wa utamaduni kwa ajili ya kizazi kilichopo na kinacho kuja lakini pili ni kubadili urithi wetu wa utamaduni kuwa zao la utalii hayo ndio malengo makuu mawili” alisema Prof Mabula.

TAA wametoa msaada wa fulana 100 kwa ajili ya washiriki wa tamasha la Urithi Wetu, ambalo litafikia tamati Oktoba 6, 2018 kwa kufungwa na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa.

 Imeandaliwa na Idara ya Uhusiano Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA)

Friday 28 September 2018

TAA Yaunga Mkono Tamasha la Urithi Wetu, Yatoa Fulana 100


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Bw. Richard Mayongela (kushoto) akimkabidhi moja kati ya fulana 100, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Prof. Audax Mabula (kulia), zilizotolewa na TAA kwa ajili ya Tamasha la Urithi Wetu kwa mkoa wa Dar es Salaam litakaloanza Oktoba Mosi, 2018, katika Kijiji cha Makumbusho ya Taifa, jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), katika kuunga mkono Tamasha la Urithi Wetu, imekabidhi fulana 100 katika hafla iliyofanyika Makumbusho ya Taifa Jijini Dar es Salaam leo.

Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Richard Mayongela alisema leo kuwa, wanaunga mkono tamasha hilo kwani linatangaza utalii wa nchini  na alikabidhi fulana hizo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Makumbusho ya Taifa, Professor Audax Mabula katika hafla hiyo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Prof. Audax Mabula (Kulia) leo akizungumza na waandishi wa habari juu ya uzinduzi wa Tamasha la Urithi Wetu kwa mkoa wa Dar es Salaam, katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa, jijini Dar es Salaam. kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela.

 Tamasha hilo ambalo lilizindulia mjini Dodoma mwezi huu, litafanyika jijini Dar es Salaam Oktoba Mosi katika Makumbusho ya Taifa, ambapo watu kibao wanatarajia kuhudhuria kabla ya kufanyika Zanzibar na baadae mikoa mingine.

Pia TAA imetangazwa kuwa mshirika wa tamasha hilo kwa ajili ya kutangaza utalii wan chi hiyo, ambapo mamlaka hiyo imeahidi kutangaza tamasha hilo katika viwanja vyake nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Bw. Richard Mayongela (katikati), Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Prof. Audax Mabula (kulia) na Mratibu wa Tamasha la Urithi Wetu Dk. Emannuel Bwasiri (kushoto) kwa pamoja wakionesha aina tatu za tisheti kati ya 100 zilizotolewa na TAA, kwa ajili ya Tamasha la Urithi Wetu kwa mkoa wa Dar es Salaam, katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa, jijini Dar es Salaam.

Mayongela aliongeza kusema kuwa wameamua kujihusisha na tamasha hilo kwa kuwa viwanja vya ndege ni njia kubwa ya watalii kungia nchini, hivyo ni muhimu kujihusisha na tamasha hilo, ambalo lilizinduliwa na  Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Kama mchango wetu katika tamasha hili, TAA inawapa waandaaji wa Tamasha la Urithi nafasi ya kujitangaza katika viwanja vyetu vyote vya ndege ili kusaidia kuutagaza utalii na kufanikisha kuingia kwa watalii nchini, “alisema Mayongela.

Tamasha hilo ambalo litakuwa likifanyika kila mwaka, linaandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, ambalo lilizinduliwa rasmi Septemba 15 mjini Dodoma na likiwa na lengo la kuongeza idadi ya watalii nchini kutoka milioni 1.3 mwaka jana ma kuongezeka zaidi.

Aidha, marais watatu wazamani wa Tanzania ni miongoni mwa watu walioalikwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kuhudhuria tamasha hilo la Oktoba Mosi.

Baada ya Dar es Salaam, Prtofesa Mabula alisema kuwa tamasha hilo litatua Jijini Arusha kwenye Uwanja wa Sheikh  Amri  Abeid  na Karatu, ambako ni njia kuu ya kuingilia katika Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro na Serengeti kuanzia Oktoba 8  hadi  13 

Saturday 22 September 2018

Waziri Ummy Avipongeza Viwanja vya Ndege Kudhibiti Ebola

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akiwa pamoja na Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Adiele Onyeze wakati wa matembezi ya uelimishaji kuhusu gonjwa la Ebola leo jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu
WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeipongeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kwa kuchukua hatua za haraka za kudhibiti ugonjwa wa Ebola usiingie nchini, imeelezwa.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Ummy Mwalimu katika hotuba yake kwa wananchi walioshiriki Matembezi ya Hiyari ya kuelimisha na kuhamasisha Jamii kuzuia ugonjwa huo usiingie nchini yaliyoanzia kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja na kuishia Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, ambapo imesharipotiwa ugonjwa huo umeingia nchi jirani ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.
Meneja Rasilimali Watu na Utawala  wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, TAA, Abdi  Mkwizu (mwenye fulana ya bluu) wakati wa matembezi hayo leo. 
Mhe. Mwalimu amesema TAA inafanya jambo jema kwa kuhakikisha wasafiri wote wanaoingia nchini kupitia viwanja vya ndege wanafanyiwa ukaguzi na kutoa taarifa za afya zao kwa wale ambao watabainika kuwa na joto la mwili lisilokuwa la kawaida.

“Nawapongeza sana tena sana Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania kwa kuhakikisha nchi inakuwa salama bila kupata maambukizi ya ugonjwa huu wa Ebola, imeripotiwa sasa huu ugonjwa upo Kivu Kaskazini, ambapo ni karibu na nchini na Wavuvi wanakuwa na muingiliano kwa kutoka huko na kuja nchini,” amesema Mhe. Mwalimu.
Hatahivyo, amesema pamoja na ugonjwa huo kutoingia nchini, lakini kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), tayari imeripotiwa wananchi 111 wa Kongo wamepata maambukizi na kati yao 75 sawa na asilimia 67 wamefariki, hivyo inakisiwa endapo Tanzania ikiwa na wagonjwa 100 anaweza kusababisha vifo vya watu 50.    

"Ebola bado haujaingia nchini Tanzania, lakini ni kweli kwamba tupo katika hatari kubwa zaidi kupata ugonjwa huu, hii inatokana na mlipuko wa ugonjwa huu kuwepo katika eneo la Kivu Kaskazini na imesharipotiwa kuua watu na sisi hatupo mbali na eneo la Kivu, hivyo tusikubali ugonjwa huu kuingia nchini na tutoe elimu juu ya ugonjwa huu,” amesisitiza Mhe. Waziri Ummy Mwalimu.
 
Aidha, Mhe. Mwalimu aliwaomba Viongozi wa Dini kutumia majukwaa yao katika mahubiri yao kutoa tahadhari kwa wananchi kuhusiana na ugonjwa huu wa Ebola, ambapo pia awaomba wasanii wa muziki na viongozi wa Siasa nchini kutumia majukwaa yao ili kufikisha taarifa kwa wananchi juu ya ugonjwa huu.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa TAA, Bw. Lawrence Thobias aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Bw. Richard Mayongela amesema viwanja vya ndege vimekuwa na mikakati ya muda mrefu kwa kushirikiana na Wataalamu wa Afya ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza ukiwemo Ebola.
Bw. Thobias amesema sasa viwanja vyote hususan vilivyopo katika mipaka ya nchi zimefungwa mashine maalum (thermos scanner) za kutambua joto la mwili wa binadamu, na ikibainika limezidi nyuzi joto 38, abiria huyo anapelekwa katika chumba maalum na kufanyiwa mahojiano ya kina juu ya afya yake na pia abiria wanaowasili na ndege zinazofanya safari nchi jirani na Kongo nao hunawa mikono kwa dawa maalum kabla ya kutoka nje ili kuendelea na safari zao.

“Kwa upande wetu tumeweka mikakati kamambe ili huu ugonjwa usiweze kuingia nchini, mbali na abiria kunawa kwa dawa maalum anapoingia tu ndani ya mlango wa wasafiri wanaotoka nje ya nchi, pia kuna mashine maalum (thermo scanners) ambazo zinaonesha joto la mwili wa kila abiria anapoingia kwenye lango hilo, na kimetekwa chumba maalum cha mahojiano kwa wale wanaobainika kuwa na joto la juu, na pia katika hospitali ya Temeke napo kipo chumba maalum endapo atabainika mgonjwa aliyepatikana kupitia viwanja vyetu anapelekwa huko,” amesema Bw. Thobias.
Mbali na kuweka mashine mbalimbali kwenye viwanja vya ndege nchini, pia TAA ikiwa ni mmoja wa wadhamini imechangia Tshs. Milioni 5 kwa ajili ya kampeni ya kutoa elimu juu ya ugonjwa wa Ebola kwa wananchi.

Ugonjwa wa Ebola unasambazwa na virusi vya Ebola na husababisha homa kali inayoweza kuambatana na kutokwa damu mdomoni, puani, masikioni, machoni na sehemu nyingine za wazi na unaenea kwa haraka, na namna ya kujikinga na ugonjwa huu ni pamoja na kuepuka kugusa damu, machozi, jasho, matapishi, kamasi, mkojo au kinyesi cha mtu mwenye dalili za ugonjwa; pia mtu hatakiwi kugusa, kuosha au kuzika maiti ya aliyekufa kwa Ebola; pia usiguse au kula wanyama kama popo, sokwe au swala wa msituni.
Mwakilishi wa Mkurugezi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Raulence Thobias akizungumza wakati wa hafla ya kuelimishana kuhusu ugonjwa wa Ebola iliyofanyika Karimjee Jijini Dar es Salaam leo.
Dalili za Ebola ni pamoja na homa kali, maumivu ya kichwa na misuli, mwili kulegea, kutapika, kuharisha, vipele na kutokwa damu maeneo mbalimbali ya mwili.






Thursday 20 September 2018

Simba SC Yafia CCM Kirumba Mwanza, Yafungwa 1-0

Mchezaji wa timu ya soka ya Simba, Shiza Kichuya(kushoto) akimlamba chenga Pastory Athnas wa Mbao FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza jana. Mbao walishinda 1-0.

Na Mwandishi Wetu
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, Simba wamefungwa bao 1-0 dhidi ya Mbao katika mchezo uliochezwa leo kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba jijini Mwanza.
Ni mchezo wa kwanza Simba inapoteza tangu kuanza kwa msimu huu, lakini pia, rekodi yake ya kuifunga Mbao ikivunjwa.

Mbao ilipata bao hilo dakika ya 26 likifungwa na Said Khamis kwa mkwaju wa penalti baada ya Pastory Athanas kuzuiwa na kipa Aishi Manula alipokuwa akijaribu kufunga.
Kwa ushindi huo, Mbao unaisogeza hadi kileleni mwa msimamo wa ligi kwa pointi 10 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi tisa, JKT tisa, Azam nane na Simba ikiwa katika nafasi ya tano kwa pointi saba.

Wekundu hao wa Msimbazi walimiliki mpira kwa dakika 90 na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini walishindwa kuzitumia kutokana na ukuta uliowekwa na wapinzani.
Kocha Patrick Aussems wa Simba alifanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji akiwatoa Mohamed Ibrahim, Shiza Kichuya na kuingia Meddie Kagere na Rashid Juma lakini bado haikusaidia.

Mbao walicheza muda wote kwa kujihami na kuwaacha wachezaji wachache kushambulia kwa kushtukiza lakini walishindwa kuzitumia baadhi ya nafasi walizokuwa wakizipata ili kuendeleza mabao.

Rekodi zinaonesha tangu Mbao ipande Ligi Kuu haijawahi kuifunga Simba. Msimu wa 2016/2017  wekundu hao walivyokuwa nyumbani waliifunga bao 1-0 na kwenye Uwanja wa Kirumba walishinda 3-2.

Pia, msimu wa 2017/2018 Simba ugenini ilipata sare ya mabao 2-2 na nyumbani ilishinda 5-0.

Mechi nyingine zilizochezwa jana ni African Lyon iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Singida United naTanzania Prisons ikilazimishwa sare nyumbani ya mabao 2-2 dhidi ya Kagera Sugar.

Viwanja vya ndege vyapongezwa kwa huduma bora



Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Kulia ni Mkrugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA), Paulo Rwegasha.

Na Mwandishi Wetu

IKIWA zimepita siku kadhaa tangu Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kutoa ufafanuzi juu ya tuhuma za wizi katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Mtanzania aishie nje ya nchi amejitokeza na kuipongeza TAA kwa ubora wa huduma ambazo inatoa kwa watumiaji wa uwanja huo.

Mtanzania huyo aliyefahamika kwa jina la Bw. Barnabas Kijika ameipongeza TAA kwa taarifa nzuri ambayo imeitoa kwa Umma kuhusiana na suala la kupotelewa mizigo kwakuwa hata yeye alishawahi kupotelewa mizigo JNIA lakini alipofuatilia alipata yote ikiwa haijaibiwa.

“Mimi nasikia moyo wa kuishukuru TAA na wafanyakazi wote kwa sababu hata mimi hili suala hilo limewahi kunitokea kipindi nimekuja Tanzania nikitokea nchi za Uarabuni ambapo mizigo miwili ikawa imepotea.

Lakini nikatoa maelezo kwa wahusika na baada ya siku moja nikapigiwa simu kupitia namba niliyoacha kwa ajili ya kupewa taarifa kwamba mizigo yangu imepatikana na nilipoikagua nikakuta mizigo yangu ipo salama yote hakuna kilichopotea,” amesema Bw. Kijika.

Pia Bw. Kijika amesema siku za nyuma alishughudia baada ya siku moja upatikanaji wa mizigo ya watalii wawili waliokuwa wakisafiri kupitia JNIA baada ya taarifa ya kupotea kwa mizigo hiyo kuwafikia wafanyakazi wa JNIA.

Katika sehemu ya barua pepe ambayo Bw. Kijika alituma kupitia anwani ya info@airports.go.tz na sauti aliyojirekodi na kuirusha kwa njia ya Whatsapp amebainisha kwamba, kwa muda mrefu amekuwa akitumia viwanja mbalimbali vya ndege vya Tanzania na changamoto ambazo anaziona ni za kawaida.

 “Kwa zaidi ya miaka 15 nimekuwa nikitumia airports za Tanzania sijawahi kujuta isipokuwa changamoto za kawaida hata Ulaya zipo,” amebainisha Bw. Kijika.

Hivi karibuni abiria mmoja Mtanzania mwenye asili ya Kiarabu alilalamikia kuibiwa pochi lenye fedha na vitambulisho mbalimbali wakati akisafiri kupitia JNIA kwenda nchi za Falme za Kiarabu, ambapo hata hivyo Kaka yake, Bw. Wael Hassan alipooneshwa picha zilizopigwa na kamera za usalama (CCTV), walikiri hakuna uwizi wowote na ndugu yao hakuibiwa na aliomba radhi kwa niaba ya ndugu yao huyo.



Wednesday 19 September 2018

Waamuzi Watakaochezesha Stars, Cape Verde Hawa


Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Soka Afrika (Caf) limetaja waamuzi kutoka nchini Mali ndio watakaochezesha mchezo wa kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika, Afcon 2019 kati ya Cape Verde na Tanzania katika Uwanja wa Taifa wa nchi hiyo mjini Praia Oktoba 12 mwaka huu.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Mario Ndimbo amesema leo kwamba kwenye mchezo huo, Mwamuzi wa katikati atakua Boubou Traore akisaidiwa na Mwamuzi namba moja, Drissa Kamory Niabe, Mwamuzi msaidizi namba mbili Baba Yomboliba na Mwamuzi wa akiba Gaoussou Kane na Kamishna wa Mchezo anatokea G. Equatorial Tadeo Nsue Onva.

Aidha, mchezo wa marudiano kwa timu hizo utakaochezwa Oktoba 16, 2018 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam wenyewe utachezeshwa na Waamuzi kutoka Djibouti.

Mwamuzi wa katikati atakuwa Souleiman Ahmed Djama na Mwamuzi msaidizi namba moja Farhan Bogoreh Salime, Mwamuzi msaidizi namba mbili Rachid Waiss Bouraleh na Mwamuzi wa akiba Bilal Abdallah Ismael.

Kamishna wa mchezo anatokea Malawi Maxwell Mtonga, Mtathmini waamuzi anatokea Rwanda Michael Gasingwa.

Wakati huo huo: CAF imewateua waamuzi kutoka nchini Tanzania kuchezesha mchezo wa kufuzu AFCON 2019 Cameroon kati ya Shelisheli na Afrika Kusini utakaochezwa Uwanja wa Stade Linite Oktoba  16,2018.

Kwenye mchezo huo Mwamuzi wa katikati atakua Mfaume Ali Nassoro akisaidiwa na Mwamuzi namba 1 Ferdinand Chacha, Mwamuzi msaidizi namba 2 Alli Kinduru na Mwamuzi wa akiba Elly Sasii. Mtathmini waamuzi anatokea Uganda Ronnie Kalema na Kamishna wa mchezo anatokea France Yves, Jean-Baptiste Etheve.

Pia Shirikisho la Mpira wa Miguu Africa (CAF) limemteua Bwana Ahmed Idd Mgoyi kuwa kamishna wa mchezo wa Kufuzu kucheza AFCON 2019 Cameroon, mchezo ambao utazikutanisha Malawi na Cameroon mchezo utakaochezwa Oktoba 16, 2018 Kamuzu Stadium katika Mji wa Blantyre.

Naye Leslie Liunda ameteuliwa kuwa mtathmini Waamuzi mchezo utakaowakutanisha Congo DR na Zimbabwe utakaochezwa Kinshasa Complexe OmniSports Stade Des Martyrs Oktoba 13,2018.

Atletico Madrid Yatoka Nyuma na Kuifunga Monaco


MONACO, Ufaransa
TIMU ya Atletico Madrid ilitoka nyuma na kuifunga Monaco 2-1 katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi A wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya uliofanyika hapa.

Wenyeji Monaco ndio walikuwa wa kwanza kupata bao la kongoza kupitia kwa Samuel Grandsir baada ya kutumia vizuri makosa ya uzuiaji yaliyofanywa na wote, Saul na Angel Correa.

Diego Costa aliisawazishia Atletico Madrid baada ya kupata pasi safi kutoka kwa Antoine Griezmann na kufunga bao huku Jose Gimenez akifunga kwa kichwa kocha ya Koke na kuwapatia wageni uongozi wa mchezo huo.

Lakini Atletico, huku kocha wake Diego Simeone akiwa jukwaani, nusura wafungwe bao katika dakika za majeruhi wakati mpira wa kichwa uliopigwa na Kamil Glik ulipopaa juu ya lango.

Kocha huyo Muargentina alikuwa akitumikia mechi yake ya mwisho baada ya kufungiwa mechi nne za Ulaya, baada ya kufanya kosa katika mechi ya nusu fainali ya Ligi ya Ulaya walipocheza dhidi ya Arsenal.

Winga Thomas Lemar, aliyesajiliwa kwa pauni Milioni 62 akitokea Monaco, alipata mapokezi mazuri wakati alipoingia katika kipindi cha pili akiichezea Atletico.
Wachezaji wa Monaco.
Katika mchezo mwingine wa Kundi A, Borussia Dortmund iliondoka na pointi zote tatu katika kundi lake baada ya kuifunga Club Brugge 1-0 shukrani kwa bao la ushindi la dakika za mwisho la Christian Pulisic katika dakika ya  20. Chipukizi wa  Dortmund, Jadon Sancho alikuwa akicheza kwa mara ya kwanza mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Katika Kundi C, mashabiki 50,.000 walishuhudia timu ya Red Star Belgrade ikitoka suluhu na kikosi cha kocha wa Napoli, Carlo Ancelotti katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya tangu mwaka 1992.

Katika mchezo mwingine, kipa wa FC Porto Iker Casillas amekuwa mchezaji wa kwanza katika kampeni tofauti 20 za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya baada ya timu yake kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Schalke katika mchezo wa Kundi D, huku Galatasaray ikiifunga Lokomotiv Moscow 3-0.

Messi Apiga Hat-trick Barcelona Ikiifunga PSV 4-0


BACELONA, Hispania
LIONEL Messi alifunga hat-trick yake ya 48 katika historia ya soka wakati Barcelona ikiwasambaratisha mabingwa wa Uholanzi, PSV Eindhoven kwa mabao 4-0 katika mchezo wa ufunguzi wa hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Nahodha huyo wa Barca alianza mbio zake hizo za kufunga mabao matatu katika mchezo huo pale alipofunga bao la kwanza kwa mpira wa adhabu kabla shuti la Luis Suarez la umbali wa kama meta 20 kugonga mtambaa panya.

Ousmane Dembele, ambaye yuko katika kiwango kizuri cha uchezaji aliwatoka mabeki wawali na kuiwezesha Barcelona kupata bao lake la pili akipiga mpira mkutoka nje ya boksi.
Messi alifunga bao la tatu baada ya kupata pasi pasi ya juu kutoka kwa Ivan Rakitic kabla beki wa Barcelona, Samuel Umtiti kutolewa nje baada ya kupewa kadi ya pili ya njano.

Licha ya kuwa 10 uwanjani, Barcelona walipata bao la nne wakati Suarez hajampatia Messi mpira, ambaye aliupiga na kumpita kipa Jeroen Zoet kutoka umbali wa kama meta 15.

Katika mchezo m,wingine wa Kundi B ulishuhudia Inter Milan ikitoka nyuma na kuichapa Tottenham 2-1 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa San Siro.

Messi, ambaye sasa ni nahodha wa Barcelona baada ya kuondoka kwa Andres Iniesta, anaonekana kuwa kuweka kando kufanya vibaya katika Kombe la Dunia nchini Urusi, baada ya kufunga mara moja tu katika fainali hizo katika hatua ya 16 bora.

Sasa mchezaji huyo amefunga mabao saba katika mechi sita msimu huu, na alikaribia kufunga pale alipopiga mpira wa adhabu katika kipindi cha pili na kutengeneza nfasi nzuri kwa Suarez na Roberto.

Mabao yake yote matatu yalikuwa mazuri. La kwanza alifunga kwa mkwaju wa adhabu likiwa ni la nane kufunga kwa staili hiyo, baada ya kupiga mpira uliojaa katika kona ya juu ya upande wa kulia wa lango.

Hadi sasa amefunga mabao 104, zikiwemo hat-trick nane katika mashindano na amepachika mabao katika mechi mfululizo 14 za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, akifikia rekodi ya gwiji wa Real Madrid, Raul.

MWAKA WA BACELONA?
Barcelona kwa miaka mitatu mfululizo imekuwa ikitolewa katika hatua ya robo fainali, huku maadui zao Real Madrid wakitwaa taji hilo katika vipindi hivyo vyote.

Wachezaji wa Barca katika kipindi hiki cha majira ya joto walizungumzia kuhusu umuhimu wa Ligi ya Mabingwa kwao wakati wakijaribu kushinda taji hilo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2015.

Msimu uliopita washindi hao wa mataji mawili wa Hispania walionekana wako shapu dhidi ya wapinzani wao baada ya kushinda mechi saba huko nyuma na alifunga mabao 13 katika mechi mbili huko nyuma, ingawa PSV walikuwa wazuri zaidi tofauti na matokeo yalivyokuwa.

Wakianza na wachezaji tisa kati ya 11 waliocheza na Roma msimu uliopita, Barceloma ilianza mchezo huo kwa nguvu huku Philippe Coutinho, akiichezea timu hiyo kwa mara ya kwanza katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, alipiga kichwa mpira wa krosi iliyochingwa na Suarez.

Zoet alifanya kazi kubwa kuokoa michomo ya wazi kutoka kwa Sergi Roberto na Coutinho.

HISTORIA YA MESSI
Barcelona imeshinda mechi 25 kati ya 27 zilizopita za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya walizocheza kwenye uwanja wao wa Nou Camp, wakitoka sare mbili. Na kwa mara ya mwisho walipoteza mchezo kwenye uwanja huo, Mei 2013 walipocheza dhidi ya Bayern Munich (3-0).

PSV Eindhoven haijashinda mechi zake tisa zilizopita za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya (wakitoka sare mara nne na kupoteza tano).

Messi amefunga katika mechi tofauti 30 za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, huku akipitwa na Raul (33) na Cristiano Ronaldo (32) wakifunga dhidi ya wapinzani tofauti tofauti.
Amefunga mara nane kwa mikwaju ya adhabu mwaka huu.

Muangetina huyo amefunga hat-trick nyingi zaidi kuliko mchezaji yeyote katika historia ya Kombe la Ulaya (8). Ameifungia Barcelona hat-trick 42 na sita ameifungia timu yake ya taifa ya Argentina.

NINI KIFUATACHO?
Barcelona itakuwa mgeni katika mchezo wa marudiano utakaofanyika kwenye Uwanja wa Wembley wakati itakapokabiliana na Tottenham katika mchezo wa raundi ijayo, huku PSV itakuwa mwenyeji wa Inter Milan – zote zitafanyika Jumatano, Oktoba 3.

Tuesday 18 September 2018

MAMLAKA VIWANJA VYA NDEGE KUSIMAMA BEGA KWA BEGA NA WAMILIKI WA VIWANJA KATA YA MSONGOLA



Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sekta ya Uchukuzi Mhandisi Atashasta Nditiye akiwa katika ofisi ya Mkurugezi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, TAA, Richard Mayongela.

 Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sekta ya Uchukuzi Mhandisi Atashasta Nditiye, akiongozana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Bw. Richard Mayongela leo wamefanya ziara katika mtaa wa Luhanga, Kata ya Msongola wilaya ya Ilala, eneo ambalo wananchi wa Kipunguni A na Kipunguni Mashariki wanapewa viwanja ili  kupisha upanuzi wa Kiwanja cha ndege cha Julius Nyerere (JNIA).


Mkazi wa Kiboga Luhanga Manispaa ya Ilala , Mrisho Kayete (katikati) akitoa malalamiko yake mbele ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sekta ya Uchukuzi Mhandisi Atashasta Nditiye, namna Kampuni ya Remix ilivyoshindwa kuwalipa toka walipoingia makubaliano juu ya uuzwaji wa mashamba yatakayokuwa viwanja ili kupewa wakazi waliopisha upanuzi wa Kiwanja cha ndege cha JNIA.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri Nditiye alipokelewa na malalamiko ya kutokulipwa fedha za fidia kutoka kwa wamiliki wa mashamba kabla ya upimaji wa viwanja katika mtaa wa Luhanga ambavyo ndivyo vinavyotakiwa  kugaiwa kwa wananchi wa Kipunguni A na Mashariki.

Akiwasilisha malalamiko yake kwa Mhandisi Nditiye, mmoja wa wamiliki wa viwanja katika eneo la Luhanga, Bw. Mrisho Hashim Kawete  alieleza kwamba mkataba unaelekeza kwamba ndani ya miezi minne walipaswa kuwa wamelipwa pesa zao zote lakini mpaka sasa, hilo halijatekelezwa.

Mwakilishi wa kampuni ya  Remix(T)ltd , Lwembu Henjewel (kushoto) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri Mhandisi  Atashasta Nditiye(kulia) , namna kampuni yao ilipofikia juu  ya zoezi la  ugawaji wa viwanja kwa wananchi.

“Kwa mujibu wa mkataba tulitakiwa kupewa malipo yetu ndani ya miezi minne tangu kusainiwa kwa mkataba lakini mpaka leo hii tunashangaa wanakuja watu wengine kupewa viwanja kabla hatujamaliziwa malipo yetu”, alisema Bw. Hashim.

Akiwasilisha pia malalamiko yake kwa Naibu Waziri Aliyekua mjumbe wa Luhanga  katika kipindi mchakato unaanza Bw. Elisante Kisingo Mmwiri ameeleza kwamba mradi huo wameupokea kwa mikono miwili lakini inawakatisha tamaa kuona kama ndani yake kuna ajenda za siri. 


Mkurugenzi  wa TAA, Mh .Richard  Mayongela akifanunua jambo mbele ya waandishi wa habari , namna TAA ilivyofanya mchakato wa malipo ya pesa  kiasi cha Sh bilioni 3.7  kwa Kampuni ya Remix (T) Ltd iliyopewa kwa ajili ya kusimamia kutafuta viwanja  537 vya wananchi waliobomolewa kupisha upanuzi wa Kiwanja cha dege cha JNIA.
“Kwa kweli tunashindwa kuelewa mkutano huu una ajenda gani ya siri, maana hata wananchi hawapewi taarifa juu ya ujio wa Viongozi, mradi huu tumeupokea na tunapenda maendeleo lakini kuna vikwazo vingi sana katika huu mradi”, alisema Bw. Mmwiri.

Naye mwakilishi wa Kampuni ya Tanzania Remix ambayo ndio imepewa jukumu la kusimamia upatikanaji na ugawaji wa viwanja kwa wakazi wa Kipunguni, Bw. Lwembu Henjewele ameeleza kwamba kutokana na uwepo wa asilimia arobaini na asilimia sitini tayari kuna mgawanyo, mfano kama mtu ana viwanja kumi basi vinne vya Tanzania Remix sita vya kwake na huyo hastahili kulipwa fidia isipokua kama anakubali sehemu ya viwanja vyake sita vilivyo bakia viingie kwenye mauzo basi atastahili kupata fedha yake inayotoka kwenye mauzo. 
 
Baada ya Malalamiko hayo Naibu Waziri Nditiye ametoa maagizo kwa Mkurugenzi Mkuu wa TAA kwamba ndani ya wiki moja atarejea tena kuja kuangalia viwanja na asikute migogoro katika eneo hilo.

“Mimi nakupa wiki moja na leo ni Jumatatu, mimi nitakuja jumatatu tena ili tuwe na uamuzi wa mara moja ili tuweze kuwakamata hawa watu wa Tanzania Remix kama watashindwa kutuonesha viwanja visivyokua na Mgogoro 537”, alisema Naibu Waziri Nditiye.

Naibu Waziri Muhandisi  Atashasta Nditiye  mwenye shati jeupe na kofia ( katikati) akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa Viwanja vya Ndege Tanzania, TAA, Richard Mayongela(kulia) wakikagua viwanja eneo la Kiboga Luhanga  Kata ya Msongola lililopo Manispaa ya Ilala ambavyo ilibidi wakabidhiwe wananchi waliopisha upanuzi wa kiwanja cha ndege cha kimataifa JNIA.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAA ameeleza kwamba ameyapokea maelekezo ya Naibu Waziri na kwamba Mkataba umeshaisha muda wake hivyo utekelezaji wake utafanyika ndani ya kipindi cha wiki moja.

“Ndani ya wiki moja kama atakua hajatekeleza maagizo haya yaliyotolewa basi hakutakua na njia nyingine zaidi ya kuchukua hatua za kisheria ikiwepo kudai viwanja ambavyo tulikua tunahitaji, pia napenda kusisitiza kwamba hatupendi kuona wananchi wanapata shida hivyo wananchi watambue kwamba hatujawaacha na kwamba tutashirikiana mpaka mwisho, hakuna haki ya mwananchi itapotea kila mtu atapata haki yake” alisema Bw. Mayongela

Mkataba kati ya Tanzania Remix na Mamlaka ya viwanja vya Ndege TAA ulisainiwa tarehe 28 mwezi Mei mwaka 2014 na ukomo wake ukiwa tarehe 27 mwezi Aprili 2015, ambapo malipo yalifanyika kwa awamu mbili, ya kwanza ikiwa ni Pesa za kitanzania milioni 700 na awamu ya pili pesa za kitanzania bilioni 3.