Kocha mchezaji Judith Ilunda (mwenye
mpira) wa Uchukuzi akizuiwa na mlinzi Lilian Selidion wa Ikulu katika mchezo wa
netiboli wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Chuo
Kikuu cha Katoliki Iringa (RUCU). Ikulu walishinda magoli 32-20. (Picha Zote na Bahati Mollel wa TAA).
Na Bahati Mollel-TAA, Iringa
WAKATI timu ya Ikulu ikitetea ubingwa wake wa
netiboli kwa kuifunga Uchukuzi katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCU),
nayo timu ya Geita Gold Mine (GGM) imeambulia nafasi ya tatu katika mchezo wa
soka wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika kwenye uwanja wa Samora mkoani
Iringa.
Ikulu ambao wanawatumia wachezaji warefu na wepesi
wakiongozwa na kocha wao mzoefu Mary Protas waliwafunga Uchukuzi kwa taabu iliyoongozwa
na kocha wake mchezaji Judith Ilunda kwa magoli 31-20. Washindi wakimtegemea
mfungaji wake Fatuma Machenga aliyefunga magoli 31 walikwenda mapumziko wakiwa
mbele kwa magoli 17-9.
Mshambuliaji Issack Hassan (17) wa
Uchukuzi akijitahidi kujinasua kutoka miguuni mwa mlinzi Enock Magole wa Geita
Gold Mine (GGM) katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu wa michuano ya Kombe
la Mei Mosi uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa. GGM
walishinda kwa penalti 6-5.
Magoli ya Uchukuzi yalifungwa na mchezaji mkongwe
Matalena Mhagama magoli 13 na Bahati Herman magoli saba. Uchukuzi imetwaa kombe
la ushindi wa pili kwa matokeo hayo.
Katika mchezo soka wa kutafuta mshindi wa tatu timu
ya GGM iliyovuliwa ubingwa na Tumbaku, sasa imeambulia nafasi ya tatu kwa
kuwashinda Uchukuzi kwa mbinde baada ya kupigiana penati 6-5, baada ya kumaliza
dakika 90 za kawaida bila kufungana.
Mchezaji Bahati Herman (mwenye mpira) wa
Uchukuzi akijiandaa kumrushia mpira Mary Kajigili (wa kwanza kushoto) katika
mchezo wa netiboli wa dhidi ya Ikulu wa michuano ya Kombe la Mei Mosi
uliofanyika leo kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki Iringa (RUCU). Ikulu
walishinda kwa magoli 32-20.
Timu hizo zilipigiana penati tisa kila mmoja, lakini
GGM walikosa tatu na Uchukuzi walikosa nne, ambapo waliofunga penalti za GGM ni
Mohamed Salum, Oswald Binamungu, Yusufu Paul, Amos Mrutu, Enock Magole na
kipa Emmanuel Sangra, huku waliokosa kwa
kupaisha na nyingine kudakwa na kipa ni pamoja na Ferdinand Makaranga, Jonathan
Mhagama na Yassin Abdallah.
Kocha Mkuu wa timu ya Uchukuzi, Mputa Zenno alisema
wameshindwa kufanya vyema kwenye michuano hiyo kutokana na kuwa na majeruhi
wengi.
“Tumekuwa na majeruhi wengi kutokana na wachezaji
wetu wengi wamekuwa wakifanya mazoezi baada ya kusikia mashindano fulani, jambo
ambalo linasababisha kutokua fiti kwa muda mrefu, hivyo natoa wito waendelee na
mazoezi hata kama mashindano yameisha,” alisema Mputa.
Mfungaji Regina Runyoro (GS mwenye mpira)
wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) akitafuta mbinu ya kumtoka mlinzi
Imelda Hango (GK) wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) katika mchezo wa Kombe
la Mei Mosi.
Naye Kocha Mkuu wa GGM, Mikidadi Mbaruku alisema
mchezo wa mshindi wa tatu ulikuwa mzuri na mashindano kwa ujumla hayakuwa
mazuri kutokana na kushirikisha timu chache, ambazo hazikutoa ushindani mkubwa.
Kwa upande wa Uchukuzi waliopata ni pamoja na David
Kunambi, Ramadhani Madebe, Karim Sabu, Seleman Kaitaba na Abubakar Hamis, huku
waliokosa kwa kupaisha juu na kipa kudaka ni Erick Mpunga, Issack Ibrahim, Ally
Poloto na Said Chembela.
Katika mchezo wa kuvuta kamba kwa wanaume, timu ya
Uchukuzi ilitwaa ubingwa baada ya kuwavuta Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)
kwa mivuto 2-0 katika mchezo uliofanyika kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha
Katoliki (RUCU). Nayo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) walivutana na
Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu (NAO) na kushinda mivuto 2-0
.
.
No comments:
Post a Comment