Wednesday 20 July 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuweka jiwe la msingi uwanja wa ndege Dodoma



 

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO

MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE
 






Simu:  +255 22 2842402-3                                                                                                                             S.L.P 18000,
Fax:    +255 22 2844495                                                                                                                                DAR ES SALAAM
                                                                                                                                                                        19/07/2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim M. Majaliwa kesho, tarehe 20/07/2016, anatarajiwa kuweka jiwe la msingi la mradi wa ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha ndege cha Dodoma.

Ukarabati huo utajumuisha urefushaji wa barabara ya kuruka na kutua ndege hadi kufikia urefu wa kilometa 2.5 kutoka Kilometa 2 za awali.
Kurefushwa kwa barabara hiyo, sasa kutatoa fursa kwa ndege kubwa Bombardier Q400, Gulfstream 550, ATR 72 n.k zenye uwezo wa kubeba abiria 90.
Ukarabati huo unafanyika kwa fedha za Serikali ya Tanzania na unasimamiwa na Wahandisi wa Mamlaka ya Viwanja Vya Ndege Nchini kwa ushirikiano  na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS).

Ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Dodoma ni miongoni  mwa Miradi mbali mbali inayotekelezwa na Mamlaka ya viwanja Vya Ndege nchini kama vile Viwanja vya Tabora, Bukoba, Kigoma na Mwanza ambayo imekwisha anza na miradi mipya ya viwanja vya ndege vya Shinyanga na Sumbawanga itakayoanza hivi karibuni.

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ni wakala wa viwanja vya ndege iliyoanzishwa kwa Tangazo la Serikali Namba 404 la mwaka 1999, chini ya Sheria ya Wakala za Serikali Na. 30 ya mwaka 1997.
Dira:
Kuwa mtoaji wa Huduma za Viwanja vya Ndege kwa kiwango cha Kimataifa

Dhima:
Kutoa Huduma Bora na Viwezeshi katika Viwanja vya Ndege kwa kuzingatia ufanisi katika matumizi ya rasilimali zilizopo

Imani kuu za Mamlaka:
·         Kuwajali  Wateja
·         Kuwaendeleza Wafanyakazi wa Mamlaka
·         Ulinzi na Usalama Viwanjani
·         Kufanya kazi kwa pamoja
·         Kuwa na Uongozi wa Mabadiliko
·         Uadilifu

IMETOLEWA NA KITENGO CHA SHERIA NA MAHUSIANO TAA

Monday 11 July 2016

Caf yaipiga faini yanga ya milioni 10 kwa wachezaji wake kumzonga mwamuzi walipocheza na timu ya Angola



Na Mwandishi Wetu
KLABU ya Yanga imesema kuwa inatafakari adhabu ya dola 5,000 (sawa n ash milioni 10) waliyopigwa na Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) baada ya wachezaji wake kuchelewesha muda.

Caf juzi ilitangaza kuiadhibu Yanga baada ya baadhi ya wachezaji wake kumzonga mwamuzi na kusababisha kuchelewesha mchezo wake timu hiyo ilipocheza na GD Sagrada Esperanca uliofanyika Angola Mei 18, 2016.

Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit anakiri wachezaji wao kumzonga mwamuzi lakini kwa sasa wanatafakari kabla ya kutoa tamko kamili.

Mchezo huo ulikuwa ni wa hatua ya kutafuta nafasi ya kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Afrika.

Uamuzi wa mchezo huo Na. 100 ulifanywa na Kamati ya Nidhamu ya CAF inayoundwa Mwenyekiti Raymond Hack Raia wa Afrika Kusini na wajumbe Mustapha Samugabo (Burundi) na Gbenga Elegbeleye (Nigeria). Pia alikuwako Amina Kassem kutoka Sekretarieti ya CAF ambaye ni Mtawala katika Kitengo cha Nidhamu.

Katika mkutano huo uliofanyika Cairo, Misri Makao Mkuu ya CAF, Julai 3, 2016, kamati ilipitia taarifa zote za mchezo na kufikia uamuzi wa kuipiga faini Yanga.

Taarifa za mchezo zinasema, wachezaji wa timu hiyo walionesha utovu wa nidhamu kwa kumzonga mwamuzi na kumsukuma mara baada ya kutoa adhabu ya penalti kwa wapinzani. 

Kwa tukio hilo, mchezo huo ulisimama kwa dakika sita. Polisi waliingia uwanjani kudhibiti hali hiyo.

Kwa kosa hilo, Wachezaji wa Yanga walivunja Ibara ya 82 inayozungumza utaratibu wa mawasiliano. Kwamba chama chochote cha mpira wa miguu, klabu, ofisa au mtu yoyote wakiwamo wachezaji, lazima waheshimu utaratibu za kuvumilia, uadiliufu na uanamichezo.

Kwa mujibu wa Kamati hiyo ya Nidhamu ya CAF, Yanga ilistahili kutozwa faini ya dola 10.000 za Marekani kwa makosa ambayo si uungwana kwenye soka yaliyoonyeshwa na wachezaji wake.

Lakini kwa kuwa Yanga haikuonyesha utovu wa nidhamu katika mchezo mingine ya kimataifa iliyofuata dhidi ya MOB ya Algeria na TP Mazembe ya DRC, imepunguziwa adhabu na sasa wametakiwa kulipa dola 5,000 za Marekani kama faini.
Faini hiyo haina budi kulipwa mara moja. Na imetakiwa kuendelea kuwa na nidhamu, vinginevyo adhabu hiyo itawarudia.

Wachezaji yanga walivyopamba utoaji zawadi kwa washindi wa American Super Market



Mkurugenzi wa Uhariri wa Quality Media Group, Theophil Makunga (kulia), akimkabidhi funguo ya pikipiki mshindi wa kwanza wa shindano la wateja wa American Super Market , luteni Reajero Mirambo jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu
WACHEZAJI wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga jana walisimamisha kwa muda shughuli American Super Market walipotinga katika hafla ya kutoa zawadi kwa washindi wa draw iliyoendeshwa na duka hilo.

Baadhi ya wachezaji hao walioongozwa na nahodha wao, Haroub Cannavaro ni pamoja na Donald Ngoma, Geofrey Mwasuiya, Malim Busungu, Donald Ngoma na Juma Abdul.
Wachezaji wa Yanga walipowasili American Super Market.
Wachezaji hao waliongozana na meneja wa timu hiyo, Hafidh Busungu.

Katika hafla hiyo, wachezaji wa Yanga Cannavaro na wengine walitoa zawadi kwa washindi wa pili na tatu,


Meneja wa Yanga, Hafidh Ally (kulia) akiwa na baadhi ya wachezaji wa timu hiyo.
Meneja wa timu hiyo Hafidh katika `waliteka kwa muda ASKARI wa Kikosi cha Jeshi cha 831 Mgulani JKT, luteni Reajero Mirambo ametwaa pikipiki baada ya kuibuka wa kwanza katika shindano la American Super Market (ASM)juzi.

`Mjeda huyo alikabidhiwa pikipiki hiyo yenye thamani ya sh milioni 1.4 aina ya Fighter katika hafla iliyofanyika katika duka hilo lililopo Quality Centre, Dar es Salaam na kuhudhuriwa pia na baadhi ya wachezaji wa Yanga.

Mshindi watatu, Neema Mosha akipokea jezi iliyosainiwa na wachezaji wa Yanga. Katikati ni  Peter Minja meneja mahusiano wa Quality Group.
Baadhi ya wachezaji hao wa Yanga wakiongozwa na nahodha wao, Nadir Haroub Cannavaro, walikabidhi zawadi kwa washindi hao,ambao walioshinda kutokana na bahati nasibu iliwashindanisha wanunuzi wa bidhaa zinazouzwa dukani hapo.

Mshindi wa pili wa shindano hilo, ambalo liliwashindanisha wateja wa ASM walionunua bidhaa za kuanzia sh. 100,000 ni Alex Munishi aliyepata mpira, ambao aliutoa hapo hapo kwa mtoto wake ambaye ni kipa wa Yanga, Deo Munishi au Dida.

Nahodha wa Yanga SC, Nadir Haroub Cannavaro (kulia) akimkabidhi mpira mshindi wa pili, Alex Munishi. Katikati ni meneja mahusiano wa Quality Group, Peter Minja.
Mshidi watatu alikuwa mwanadada, Neema Mosha ambaye ni shabiki wa Simba na alipata jezi ya Yanga iliyosainiwa na wachezaji wote wa timu hiyo.

Katika hafla hiyo, mshindi wa kwanza ambaye alikabidhiwa pikipiki aina ya Fighter yenye thamani y ash. milioni 1.4, ni askari jeshi mwenye cheo cha luteni kutoka 831 KJ, Reajero Mirambo.

Mshindi wa kwanza, luteni Reajero Mirambo akizungumza na waandishi wa habari.
Mirambo akizungumza baada ya kukabidhiwa pikipiki hiyo alisema kuwa, itamsaidia kuondoa tatizo la usafiri akienda na kurudi kazini kwake au wakati wa shuguli zingine kutokana na msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.

Washindi hao walipatikana baada ya kununua bidhaa za kuanzia sh 100,000 na kuendelea, ambapo moja kwa moja waliingizwa katika draw na kupatikana washindi hao watatu.

Saturday 9 July 2016

Ureno yaivaa Ufaransa katika fainali ya Mataifa ya Ulaya ya euro 2016 kesho Jumapili



PARIS, Ufaransa
BEKI wa kushoto mwenye kipaji, Raphael Guerreiro ni mmoja kati ya wachezaji watatu wa Ureno ambao watakaikabili nchi yao waliyozaliwa, wakati watakapokutana na Ufaransa kwenye fainali ya mataifa ya Ulaya, Euro 2016, kesho Jumapili saa nne usiku kwa saa za hapa Bongo.

Guerreiro na golikipa, Anthony Lopes walizaliwa na kukulia nchini Ufaransa, ambako ni nyumbani kwa Wareno wengi wahamiaji.

Kiungo Adrien Silva aliishi nchini Ufaransa hadi akiwa na umri wa miaka 12, wakati alipohamia nchini Ureno na familia yake.

Nilichagua Ureno. Yalikuwa maamuzi yangu muhimu. Si familia yangu wala marafiki zangu ambao waliweza kuubadilisha uamuzi wangu, amesema Guerreiro mwenye umri wa miaka 22, ambaye mwezi uliopita alikubali uhamisho wa kwenda kwa miamba ya Ujerumani, Borussia Dortmund akitokea Klabu ya Lorient inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa, Ligue 1.

Guerreiro alizaliwa kitongoji cha Le Blanc Mesnil jijini Paris, umbali mfupi kutoka kwenye Uwanja wa Stade de France ambako fainali hiyo inachezwa leo.

Ufaransa inaingia kwenye mchezo huo ikiwa ni nchi ya kwanza kufika mara mbili fainali ya Euro ikiwa nchi mwenyeji wa mashindano, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1984.

Michel Platini bado anashikilia rekodi ya magoli mengi zaidi kwenye msimu mmoja wa michuano ya Euro (magoli 9, Euro 1984) magoli matatu zaidi ya Antoine Griezmann aliyefunga magoli 6 hadi sasa Euro 2016. 

Kwa upande wao Ureno hadi wanamaliza hatua ya makundi walikuwa hawajashinda mchezo hata mchezo mmoja. Ni mfumo tu wa mashindano ya mwaka huu ndiyo uliwapa nafasi ya kutinga hatua ya 16 bora, kupitia mlango wa nyuma.

Ureno mechi yao katika hatua ya 16 bora ilishuhudia dakika 90 zikiisha kwa sare. Bao la ushindi likapatikana dakika ya 117, dakika tatu kabla ya dakika za nyongeza kumalizika.
Ureno kwenye hatua ya Robo fainali waliitoa Poland kwa mikwaju ya penalti baada ya sare ya bao 1-1 dakika 120. 

Cristiano Ronaldo ameifikia rekodi ya gwiji wa Ufaransa, Michel Platini ya kufunga magoli 9 ya Euro. Ronaldo alifunga goli lake la kwanza kwenye michuano ya Euro mwaka 2004.

Anahitaji goli moja ili kuwa mfungaji bora wa muda wote kwenye michuano ya Euro.

Mara ya mwisho timu kutinga fainali kiujanja ujanja namna hii kama Ureno, ilikuwa Italia kwenye kombe la Dunia 1982 na ikawa bingwa.