Wednesday, 25 April 2018

Ikulu, Uchukuzi Kuamua Bingwa Netiboli Mei Mosi



Mfungaji tegemeo wa timu ya Uchukuzi, Matalena Mhagama (mwenye mpira) akimrushia mfungaji mwenzake Bahati Herman (GS kulia) akimtoka mlinzi Zaujath Mdemu (GK) wa RAS Iringa katika mchezo wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika leo kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki Iringa (RUCU), ambapo Uchukuzi waliibuka washindi kwa magoli 31-17. (Picha Zote na Bahati Mollel wa TAA).

Na Bahati Mollel-TAA, Iringa
TIMU za Ofisi ya Rais Ikulu na Uchukuzi zitaamua bingwa wa mchezo wa netiboli wa michuano ya Kombe la Mei Mosi inayofanyika mkoani hapa, baada kushinda mechi zao tatu kila mmoja na kujikusanyia pointi sita.

Hata hivyo, Ikulu ambao ndio mabingwa watetezi, wamewazidi Uchukuzi kwa kujikusanyia magoli 159 na kufungwa 12, wakati Uchukuzi wamefunga 130 na kufungwa 33, ambapo mchezo wao unaotabiriwa kuwa mkali utakaofanyika keshokutwa kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCU).

Baadhi ya viongozi wa kamati ya Michezo ya Mei Mosi leo   wakiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa timu ya Uchukuzi na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Katika mchezo wa netiboli uliochezwa leo kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCU), timu ya Uchukuzi iliwachapa RAS Iringa kwa magoli 31-17. Washindi walikwenda mapumziko wakiwa mbele kwa magoli 14-7, ambapo wafungaji wake Matalena Mhagama alifunga magoli 26 na Bahati Herman kafunga magoli matano.

Hadi sasa Uchukuzi imeshatwaa vikombe vya ubingwa wa baiskeli kwa wanawake na wanaume, huku kamba wanawake wametwaa ushindi wa pili. Bingwa wa kamba wanawake ni RAS Iringa.

Mchezaji Mwadawa Hamis (aliyenyoosha kidole) wa Uchukuzi akiwaelekeza wenzake jinsi ya kuendelea kufanya vyema wakati wa mapumziko wa mchezo wa netiboli wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika jana kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki Iringa (RUCU), ambapo Uchukuzi walishinda kwa magoli 31-17. 

Katika hatua nyingine, timu ya Tumbaku ya Morogoro jana iliwafunga Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa magoli 5-0 katika mchezo wa soka uliofanyika kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa.

Washindi ambao tayari wametinga hatua ya nusu fainali kutoka Kundi ‘A’ walipata bao lao la kwanza katika dakika ya 14 kupitria kwa Kelvin Makamba, huku Salum Idd akifunga bao la pili katika dakika ya 16.

Mshambuliaji Salum Idd aliongeza bao la tatu katika dakika ya 21, na Makamba alipachika bao la nne katika dakika 45 na Ramadhani Silegondo alifunga hesabu kwa bao la tano dakika ya 51.

Mchezaji Warda Sapali (mwenye mpira) wa timu ya RAS Iringa) akimrushia mfungaji wao Zitaamanzia Kididi (GA aliyenyoosha mkono juu) huku Mary Kajigiri (C ) wa Uchukuzi akitafuta mbinu za kuupokonya mpira huo katika mchezo wa netiboli wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika leo kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki Iringa (RUCU), ambapo Uchukuzi walishinda kwa magoli 31-17. 

Katika mchezo wa kuvuta kamba wanaume uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Mlandege, timu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) waliwavuta Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu (NAO) kwa mvuto 1-0; nao Uchukuzi wanawake waliwavuta NCAA kwa mivuto 2-0.

Michuano hiyo itaendelea leo mchezo wa riadha wanawake kilometa nane na wanaume kilometa 10.

Wachezaji wa timu ya kamba ya wanawake ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wakiongozwa na Neema Mbuja (wa kwanza mbele) wakicheza na RAS Iringa, katika mchezo wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mlandege mkoani Iringa, hata hivyo Tanesco walivutwa kwa mivuto 2-0. 

Washindi wa pili wa michuano ya Mei Mosi timu ya wanawake ya Uchukuzi wakimalizia mchezo wao kwa kuwavuta Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorogoro leo kwa kuwavuta mivuto 2-0. Mchezo ulifanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mlandege. 




No comments:

Post a Comment