Wednesday 11 December 2019

TAA Yasaidia Kutokomeza Mimba za Utotoni Tabora


Mbunge wa Viti Maalum wa Jimbo la Tabora, Mhe. Munde Tambwe (wenye gauni la kijani na njano) hivi karibuni akiwa na Kaimu Meneja Masoko wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Rose Comino (wa tatu kushoto) akimwakilisha, Mhandisi Julius Ndyamukama kukabidhi saruji tani 12.5 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa kike wa Kata mbalimbali za Tabora.
Na Mwandishi Wetu
 MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imeungana na Mbunge wa Viti Maalum na Wakazi wa Mkoa wa Tabora kusaidia jitihada zao za kutokomeza mimba za utotoni kwa kutoa msaada wa tani 12.5 za saruji kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa kike wa shule za sekondari.

Akikabidhi saruji hiyo hivi karibuni katika Kata ya Itonjanda, Manispaa ya Tabora, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mhandisi  Julius Ndyamukama, ambayo ni sawa na mifuko 250 ya saruji, Kaimu Meneja wa Biashara wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Rose Comino, amesema TAA, ipo bega kwa bega katika suala zima la kusaidia jamii katika masuala mbalimbali likiwemo la Elimu, ambapo watoto wote ni sawa na wanastahili kupata elimu na sio kukatizwa masomo kutokana na vikwazo mbalimbali zikiwemo mimba za utotoni.
Kaimu Meneja Masoko wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Rose Comino (wa pili kushoto) hivi karibuni  akimwakilisha, Mhandisi Julius Ndyamukama akiwa kwenye picha ya pamoja na Mbunge Viti Maalum (CCM), Mhe. Munde Tambwe (wa tatu kushoto) mara baada ya kukabidhi msaada wa saruji tani 12.5, kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya watoto wa kike wa shule za sekondari. Wengine pichani ni Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora, Joseph Kashushura (kushoto) na Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Tabora (wapili kulia).
 Rose amesema Wananchi wa Tabora waungane kwa pamoja kuunga mkono jitihada za  Mbunge wa Viti Maalum Munde Tambwe la ujenzi wa mabweni kwa ajili ya watoto wa kike wa shule za sekondari, ambao wanatembea umbali mrefu kwenda shule, ambapo sasa wanatokomeza mimba za utotoni na kushirikiana kuwabaini wale wote wenye kutenda matendo hayo maovu.

“Kwa pamoja tuoneshe jitihada za dhati kwa kuhakikisha watoto wetu wanakuwa sehemu salama mabwenini, nina uhakika wa asilimia 100 kwa 100 tutapata watoto wengi wa kike watakaomaliza shule na kufanya vizuri katika masomo yao,” amesema Rose.

Amesema TAA ni miongoni mwa taasisi ya serikali iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Wakala wa Serikali Na.30 ya mwaka 1997 na kupewa dhamana na Serikali ya kuvisimamia na kuviendesha jumla ya viwanja 58,  imekuwa ikitekeleza sera yake ya kurudisha kwa Jamii katika masuala mbalimbali yakiwemo ya elimu.

Moja wa Shule ya sekondari ya Kata ya Itonjanda ya Manispaa ya Tabora, ambayo itajengwa bweni la watoto wa kike ili kuondoa mimba za utotoni. Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) hivi karibuni  imetoa msaada wa saruji tani 12.5 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni hayo.
Rose amesema viwanja vya ndege vinatoa fursa mbalimbali za kibiashara zikiwemo za kuendesha migahawa, hoteli, maduka ya bidhaa mbalimbali, usafirishaji wa mizigo ikiwemo mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Pia viwanja vya ndege vimekuwa miongoni mwa eneo linalozalisha ajira rasmi na zisizo rasmi, ambazo zinahusisha mashirika mbalimbali ya ndani na nje ya nchi yenye kutoa huduma katika maeneo ya viwanja vya ndege.

Naye Tambwe ameushukuru uongozi mzima wa TAA kwa kusaidia jitihada hizo, ambazo anauhakika kwa lengo alilojiwekea ataweza kusaidia ujenzi wa mabweni mengi katika kila kata ya Mkoa wa Tabora.

“Naomba ndugu zangu tuunge mkono jitihada hizi nilizoanzisha, na pia kuungana na  Rais John Pombe Magufuli za kutoa elimu bure, mimi nimezaliwa hapa Tabora na nimeona jinsi gani mabinti zetu wanavyotembea umbali mrefu kwenda na kurudi shule jambo ambalo linachangia kupata vishawishi njiani na kujikuta wanapata mimba za utotoni.” Amesema Tambwe.

Hatahivyo, amesema mifuko 100 kati ya hiyo 250 itapelekwa kwenye Kata ya Itonjanda, ili ujenzi uanze mara moja, na 150 iliyosalia itapelekwa kwenye shule nyingine.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Itonjanda ameshukuru msaada huu uliotolewa na TAA kwani watoto wamekuwa wakitembea umbali wa Kilometa 10 kwenda shule, na wamekuwa wakiathirika kutokana na kupata mimba.

“Tumuunge mkono Rais wetu kwani Tanzania bila elimu haitaenda tuunge jitihada hizi kwani watoto wanakuwa wananawiri sana wanapoingia shule za sekondari, kwani wamekuwa wakipewa fedha ndogo ndogo ambazo zimekuwa zikiwaponza na kujikuta wanapata ujauzito, ” amesema.

Tuesday 3 December 2019

Uchukuzi Sports Club Yakabidhi Mataji ya Mei Mosi 2019


Kaimu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Sekta ya Uchukuzi, Gabriel Migile (wa pili kushoto) akipokea moja ya vikombe vya Michuano ya Mei Mosi 2019 kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa Uchukuzi Sports Club (USC), Hassan Hemed. Wa pili kushoto ni Katibu wa USC, Mbura Tena na Mkurugenzi Msaidizi Utawala Hamidu Mbegu.

Na Mwandishi Wetu
TAASISI zilizopo katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano zimetakiwa kupanga bajeti ya michezo  katika bajeti zao za mwaka ili kuhakikisha wanashiriki vizuri katika michezo,  imeelezwa.
Hayo yalisemwa jana na Kaimu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Sekta ya Uchukuzi, Gabriel Migile baada ya kukabidhiwa vikombe vya ushindi wa Mashindano ya Mei Mosi 2019 kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa Uchukuzi Sports Klabu (UCS), Hassan Hemed.

Akijibu changamoto zilizotolewa na Katibu Mkuu wa Uchukuzi Sports Club, Mbura Tenga, ambaye katika risala yake ya utangulizi alieleza moja ya changamoto zinazowakabili ni kwa baadhi ya taasisi kushindwa kutenga fedha kwa ajili ya michezo.

Tenga alisema kuwa hilo la kushindwa kutenga fedha linatokana na taasisi hizo kutokuwa na bajeti kabisa ya michezo na wengi wa maofisa rasilimali watu wake kutojua kabisa umuhimu wa michezo kazini na kuona kama ni kupoteza muda na fedha tu.

Migire alisema kuwa taasisi nazo zinatakiwa kuiweka michezo katika bajeti za idara zao za kila mwaka ili kuhakikisha wachezaji wao wanashiriki kutoa wachezaji katika Uchukuzi Sports Club.

Migile pia aliipongeza Uchukuzi Sport Klabu kwa kutwaa ubingwa wa jumla kwa mara ya pili mfululizo katika Mashindano ya Mei Mosi, baada ya mwaka huu kutwaa jumla ya vikombe tisa, vinne vikiwa katika nafasi ya kwanza, ambavyo ni Kuvuta Kamba kwa Wanaume na Wanawake na Baiskeli kwa Wanauame na Wanawake.

Uchukuzi Sports Klabu katika Mashindano ya Mei Mosi mwaka huu yaliyofanyika Mbeya, walitwaa vikombe tisa kati ya 14, ambavyo hushindaniwa kila mwaka.

Uchukuzi pia ndio klabu pekee katika mashindano hayo kupeleka timu za michezo yote 14 ya mashindano hayo, tofauti na wizara zingine, ambazo wakati mwingine hupeleka timu au mchezaji mmoja.

Akijibu kuhusu timu ya Uchukuzi mara mbili kualikwa Zanzibar (Unguja na Pemba) na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ya Zanzibar (ZAA) na kufanya utalii wa ndani,  alisema hilo ni suala ni muhimu sana, hasa ukizingatia linahusu Muungano, ambapo liwataka kupanga utaratibu kuona USC wanafanyaje ili kuwaalika Bara Wazanzibari.

Pia alisema changamoto ya kutokuwa na ofisi inayoikabili USC llinaweza kushughulikiwa, hasa ukizingatia kuwa Katiba ya UCS inaeleza kuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, lazim atoke wizarani, hivyo itakuwa rahisi kuwepo kwa ofisi wizarani kwa ajili ya klabu yao.

Akielezea kuhusu ushindi huo wa jumla, alisema kuwa ni mkubwa sana, hivyo hauwezi kupita kimya kimya, kwani lazima na wakubwa nao wajue nini kimeletwa na USC, hivyo hafla hiyo itaandaliwa tena kwa ukubwa wake.

Aidha, Tenga alisema wanatarajia Februari 7, 2020 kufanya Mkutano mkuu kwa ajili ya mabadiliko ya Katiba pamoja na kuchagua viongozi wapya, ambapo kila taasisi ina kuwa na mwakilishi katika klabu hiyo, tofauti na sasa ambapo taasisi moja inaweza kuwa na zaidi ya mjumbe mmoja na nyingine isiwe nayo kabisa.

MultiChoice waandaaseminamaalummsimu wa saba {7}tuzo za ‘Africa Magic Viewers’ Choice Awards !


Na Mwandishi Wetu
BAADA ya kusibiri kwa muda mrefu, hatimaye Africa Magic kwa kushirikiana na Kampuni ya Multi-Choice Africa, imetangaza rasmi kupokea maombi ya kushiriki kwenye msimu wa saba wa tuzo za kimataifa za Africa Magic Viewers’ Choice Awards 2019 maarufu kama AMVCA Awards.

Akizungumza katika semina maalum kwa ajili ya tuzo hizo za awamu ya saba na wadau wa tasnia ya filamu hapa nchini, Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya MultiChoice Tanzania Bi. Grace Mgaya amesema kuwa baada ya muda mrefu hatimaye tuzo hizo zimerejea tena.

Tuzo hizo ni mahususi kwa ajili ya filamu za Afrika na hufanyika kila mwaka ili kutambua jitihada kubwa za watengenezaji filamu, waigizaji pamoja na mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika sekta hii ndani ya mwaka husika.

Naye Ofisa Maendeleo ya filamu , Bodi ya Filamu Tanzania, Clarence Chelesi aliongeza: “Kampuni ya MultiChoice imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za wazalishaji wa filamu hapa nchini kwetu, hivyo nitoe rai yangu kwa magwiji wote wa filamu hapa Tanzania kuweza kutumia fursa hii adimu kwa kushiriki katika mchakato huu ambao utawawezesha kujitangaza na kuzitangaza kazi zinazotengenezwa hapa nyumbani katika Nyanja za kimataifa kupitia tuzo hizi”, alieleza Chelesi.

Maandalizi kwa ajili ya msimu huu wa saba yanaendelea na tuzo hizi zitafanyika Machi mwakani ili kuwapata vinara mbalimbali wa filamu kutoka barani Afrika.

Maombi yanayokaribishwa kwa ajili ya kushiriki ni ya kazi za filamu na televisheni ambazo zilitayarishwa na kuoneshwa kuanzia April 1, 2018 hadi Novemba 30, 2019.
Ufuatao ni mwongozo wa jinsi ya kutuma kazi kwa ajili ya kushiriki:

Hatua ya 1: Andaa clip ya dakika 5 (reel) kwa ajili ya online submission.
Hatua ya 2: Ingia kwenye tovuti ya Africa Magic kupitia www.africamagic.tv/AMVCA. na click kwenye banner ya AMVCA Seventh edition itakayokupelekea kwenye ukurasa wa kutuma maombi

STEP 3: Jaza fomu za kuomba kushiriki halafu upload clip yako. Kila online submission iliyokamilika itapewa namba ya kumbukumbu kuthibitisha

STEP 4: Hakikisha video ya kazi yako ina uzito usiozidi mb 300

STEP 5: Weka namba yako ya kumbukumbu , kisha tuma hard drive ya kazi uliyoiwasilisha mtandaoni kwenda: Margaret Mathore
2 nd floor, MNET offices
Local Production Studio
Jamhuri Grounds off Ngong road
Nairobi Kenya