Na Mwandishi Wetu
Tanzania imepata wawakilishi wawili
watakaoshiriki katika msimu wa saba wa tuzo maarufu barani Afrika kwa wanafunzi
wapenzi wa masomo ya Sayansi na Teknolojia ijulikanayo kama - DStv Eutelsat
Star Awards.
Wanafunzi hao Michael Ditrick wa shule ya Sekonday Ilboru – Arusha
na Taher Rasheed wa Al-Madrasat Ussaifiyatul Burhaniyah
ya jijini Dar es Salaam
Michael ameshika nafasi ya kwanza katika
uandishi wa insha maalum na Taher kwa mchoro maalum kuhusiana na sayansi ya
Setelait ambapo wanafunzi zaidi ya 150 kutoka shule mbalimbali nchini
walishiriki katika mashindano hayo ya mwaka huu. Washindi hao walipatikana
kutakana na utahini uliofanywa na jopo la majaji sita.
Kazi za washindi hao zimewasilishwa MultiChoice
Africa ambapo zitapambanishwa na kazi kama hizo kutoka kwa washindi wa nchi
nyingine kote barani Afrika na hatimaye kupatikana mshindi wa jumla katika kila
kipengele yaani wale walioandika insha na wale walioandaa mchoro.
Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania
Maharage Chande, amesema tuzo za mwaka huu zimekuwa na ushindani mkubwa ambapo
shule kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya, Arusha,
Dodoma, Pwani zimeshiriki.
“Kuongezeka wa idadi ya wanafunzi wanaoshiriki
katika tuzo hizi ni ishara njema na tunaamini kwa viwango walivyoonyesha, bila
shaka mwaka huu tutapata ushindi mkubwa kuliko hata ule wa mwaka jana” alisema
Maharage.
Amesema tuzo hizi zinalenga kuwajengea vijana
wetu ari ya kushiriki katika masomo ya sayansi na pia kuhamasisha ubunifu na ugunduzi
katika tasnia ya sayansi.
Amewataka walimu kuwahimiza wanafunzi wao kushiriki
katika tuzo kama hizi za kimataifa kwani ni kipimo kizuri kwa wanafunzi wetu na
pia inajenga kujiamini kwa wanafunzi wetu.
Tuzo hizi ambazo zinahusisha uandishi wa insha
maalum au kuandaa bango vyenye ujumbe kuhusiana na elimu ya anga hususan
Setelait ni za wazi kwa wanafunzi wote wa shule za sekondari wenye umri kati ya
miaka 14 – 19.
Mwaka
huu, washindani walitakiwa kuandika insha au kubuni bango kuhusu manufaa yaliyoletwa
na uvumbuzi wa setelaiti katika maisha ya kila siku hapa ulimwenguni na ni
jinsi gani setelait imekuwa kama kiungo muhimu kwa shughuli zote zinazofanyika
kote duniani.
Kama kawaida tuzo hizi zina zawadi kabambe ambapo mshindi wa Insha
atapata fursa ya kuzuru kituo cha Eutelsat nchini Ufaransa na pia kwenda Guiana
kushuhudia mubashara urushwaji wa setelait angani.
Mshindi wa bango atajishindia safari ya kwenda nchini Afrika Kusini na
kutembelea kituo cha anga cha nchi hiyo na pia makao makuu ya MultiChoice Africa
akiwa kama mgeni maalum. Shule
zitakazotoa washindi hao zitapata zawadi ya kufungia huduma ya DStv bure.
Wanafunzi wengine waliofanya vizuri katika mchakato huo ni pamoja na Pio
Mwita wa UWATA Sekondari ya Mbeya ambaye ameshika nafasi ya pili kwenye insha
na Peter Kiama wa Feza Boys ya Dar es Salaam aliyeshika nafasi ya pili kwa
upande wa bango.
Mwaka jana Tanzania iliibuka mshindi wa pili kwenye insha baada ya
Davids Bwana wa FEZA Boys kunyakua nafasi hiyo nyuma ya mwanafunzi Leoul Mesfin kutoka Ethiopia.
No comments:
Post a Comment