Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Michezo ya Jumuiya ya Madola (CGF) limempatia
tuzo ya Utumishi Uliotukuka gwiji wa riadha wa Tanzania, Filbert Bayi kutokana
na mchango wake katika mchezo huo.
Bayi, alitwaa medali ya dhahabu, ambapo mbali na kuvunja
rekodi ya dunia ya mbio za meta 1500 katika Michezo ya Jumuiya ya Madola Chrischurch,
New Zealand mwaka 1974, aliweka pia rekodi mpya ya Jumuiya ya Madola, ambayo
amedumu nayo hadi sasa, ikiwa ni miaka 44.
Kwa upande wa rekodi ya dunia ya mbio hizo, Bayi ambaye
ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), alidumu nayo kwa takribani
miaka mitano, kabla haijavunjwa na Sebastian
Coe, ambaye kwa sasa ni Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Riadha,
IAAF.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano wa
CGF, Ben Nichols, Bayi alipewa tuzo hiyo pamoja na viongozi wengine wa
mashirikisho ya michezo kutoka nchi mbalimbali duniani.
Bayi aliliambia Habari Leo jana kwa njia ya simu kuwa,
pamoja na jambo la kushtua, lakini kwake jambo muhimu na kubwa ni kutambuliwa
kwa juhudi zake.
Alisema jambo jema kama hilo daima ni furaha kubwa na
linamkubusha mazuri, ambayo ameyafanya wakati wake akiwa mwanariadha wa kitaifa
na kimataifa.
“Mafanikio daima hayaji kirahisi, juhudi binafsi,
nidhamu kujituma ni muhimu sana na tuzo hiyo ni kwa ajili ya familia yangu,
wanamichezo pamoja na mashabiki wangu, “alisema Bayi.
Akitoa rai, Bayi aliwaomba Watanzania kuwa na
utamaduni na kutambua wanamichezo walioliletea taifa heshima katika maeneo
mbalimbali, ikiwemo katika michezo pamoja na utendaji mzuri wa kazi.
Alisema kuwa hatua hiyo itahamasisha wanamichezo
wadogo na watendaji katika vyama na mashirikisho ya michezo.
No comments:
Post a Comment