Na Mwandishi Wetu
LICHA ya ushindi mnono ulioiweka katika nafasi nzuri
ya kukaribia kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, kocha wa
Yanga George Lwandamina, amewataka wachezaji wake kutowadharau wapinzani wao
Welayta Dicha.
Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Taifa Dar
es Salaam, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, hivyo kujiweka mguu moja
mbele katika harakati za kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo ya pili kwa
ukubwa katika ngazi ya klabu Afrika.
Akizungumza na gazeti hili Lwandamina alisema Welayta
Dicha na timu nzuri na wanapaswa kujiandaa kikamilifu ili kuweza kuwadhibi
wakiwa kwao vinginevyo wanawezakujikuta katika wakati mgumu na ikiwezekaa
kupoteza nafasi ya kucheza hatua ya makundi.
“Mbali na mbinu za kucheza ugenini, ambazo nimeanza
kuwafundisha vijana wangu lakini kitu kingine cha muhimu nimekuwa
nikiwakumbusha kwamba bado tuna kibarua kizito na ushindi tulioupata hapa
nyumbani unapaswa tuulinde kwa kucheza kwa kushambulia ili tupate mabao
mengine,” alisema Lwandamina.
Kocha huyo raia wa Zambia alisema kitu cha msingi
ameamua kuanza nacho katika marekebisho yake kabla ya mchezo huo ni safu yake
ya ulinzi, ambayo ilifanya makosa mengi ikifuatiwa na ile ya ushambuliaji
ambayo nayo ilipoteza nafasi nyingi walizotengeneza.
Alisema kama wangeweza kuzitumia vizuri nafasi zote
walizozipata kazi yao katika mchezo wa marudiano ingekuwa nyepesi lakini mabao
mawili bado hayampi uhakika wa kusonga mbele kutokana na ubora wa wapinzani wao
ambao watakuwa nyumbani Addis Ababa.
Yanga inatarajiwa kuondoka nchini mwishoni mwa wiki
hii kuelekea Ethiopia ambapo ndiko utakapofanyika mpambano huo na endapo
watafanikiwa kusonga mbrele watacheza hatua ya makundi ya michuano hiyo kama
ilivyokua mwaka 2016 chini ya kocha Hans van der Pluijm.
No comments:
Post a Comment