MANCHESTER, England
MANCHESTER City inaweza kupunguza maumivu ya kufungwa
na Liverpool katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kwa kutwaa taji la
Ligi Kuu ya England kesho wakati itakapocheza dhidi ya majirani zao wa Manchester
United.
Mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Etihad,
ambako ni nyumbani kwa Man City, utaanza kuanzia saa 1:30 usiku kwa saa za
Afrika Mashariki.
Man City Jumatano ilipokea kichapo cha mabao 3-0
kutoka kwa Liverpool katika mchezo wa kwanza wa robo fainali uliofanyika kwenye
Uwanja wa Anfield na hivyo ushindi wa leo utaipa faraja kubwa timu hiyo
inayofundishwa na kocha Mhispania, Pep Guardiola.
Endapo Man City itashinda leo itakuwa imefikisha jumla
ya pointi 87, ambazo hazitaweza kufikiwa na timu nyingine yoyote ikiwemo Manchester
United iliyopo katika nafasi ya pili yenye pointi 68, ambapo ikishinda mechi
zote zilizobaki itafikisha pointi 86 tu, ambazo zitakuwa tayari zimepitwa na
City.
Vijana wa Guardiola watakuwa timu ya kwanza katika
historia ya miaka 26 ya Ligi Kuu ikitwaa ubingwa huku ikiwa imebakisha mechi
sita mkononi, endapo leo itaibuka na ushindi katika mchezo huo.
Man City ina pointi 16 mbele ya Jose Mourinho, ambaye
timu yake iko katika nafasi ya pili, na endapo watashinda leo litakuwa taji la
kwanza kwa kocha Guardiola tangu aanze kufundisha soka England.
Vinara hao wa
Ligi Kuu wamekatishwa tamaa na kipigo cha 3-0 kutoka kwa Liverpool katika
mchezo huo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kwenye Uwanja wa Anfield.
Mpambano huo unakuja ikiwa ni siku tatu kabla ya
kupigwa kwa mchezo wa marudiano wa Ulaya na Guardiola anakabiliwa na kibarua
cha kubadili matokeo watakaporudiana kwenye Uwanja wa Etihad.
No comments:
Post a Comment