Filbert Bayi mara baada ya kutua kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) akitokea Gold Coast, Australia, ambako alipewa tuzo ya kutukuka. Kushoto ni mkewe, Anna Bayi. |
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imezitaka kampuni mbalimbali kujitokeza kudhamini riadha badala ya kung’ang’ania soka.
SERIKALI imezitaka kampuni mbalimbali kujitokeza kudhamini riadha badala ya kung’ang’ania soka.
Bayi akiwasili JNIA. |
Hayo yameelezwa mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa wa
Pwani, Everist Ndikilo katika hafla ya
kumpongeza mwanariadha wazamani wa Tanzania, Filbert Bayi kwa kupata tuzo iliyotukuka
iliyotolewa na Shirikisho la Michezo ya Jumuiya ya Madola (CGF).
Bayi alipewa tuzo hiyo wiki iliyopita wakati wa
michezo hiyo iliyomalizika juzi Gold Coast, Australia kufuatia mchango wake
katika michezo hiyo, ikiwemo kuweka rekodi ya Madola iliyodumu kwa miaka 44
sasa bila kuvunjwa.
Mwanariadha huyo nguli, aliweka rekodi ya dunia
sambamba na ile ya Jumuiya ya Madola ya mbio za meta 1500 mwaka 1970 wakati ile
ya dunia ilivunjwa baada ya miaka mitano, lakini ya Madola bado anaishikilia
hadi leo.
Wanafunzi wa shule yake wakimsubiri kwenye Kiwanja cha Ndege. |
Ndikilo alisema kuwa mafanikio ya Bayi yalikuja
kutokana na juhudi zake binafsi pamoja na uzalendo kwa nchi yake.
Alisema makampuni yameng’ang’ania kudhamini soka,
hivyo aliyaomba kujitokeza kudhamini na riadha ili kuuletea mafanikio mchezo
huo, ambao umeiletea sifa kubwa nchi.
Ndikilo alimpongeza Bayi kwa tuzo hiyo na kuwataka
wanariadha chipukizi kujituma zaidi katika mchezo huo, kwani juhudi zinalipa
kama alivyofanikiwa Bayi na sasa Jumuiya ya Madola imeamua kumuenzi.
Alisema kuwa mkoa wake uko tayari kushirikiana na
kusaidia taasisi yoyote, ambayo itakuwa tayari kusaidia kudhamini mchezo wa
riadha ili kuhakikisha unakuwa.
Kwenye Kiwanja cha Ndege, Bayi alipigwa na mshituko baada ya kukutana mapokezi makubwa kutoka kwa wadau wa michezo wa mkoa wa Pwani pamoja na wanafunzi na walimu wa shule yake na kupewa shada la maua huku ukiwa na mabango ya kumpongeza.
Bayi aliwasili kutoka Gold Coast na kupokewa katika
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) na wadau mbalimbali
wa michezo kabla ya kuondoka kwa msafara
mzito ulioongozwa na pikipiki ya usalama barabarani na gari la polisi kwenda Mkuza Kibaha, alikoandaliwa sherehe hiyo ya kumpongeza.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Everisy Ndikilo akimpongeza Bayi pamoja na Kamanda wa Polisi (RPC) wa mkoa huo, Jonathan Shana (kulia) |
Awali, Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania
(TOC), Henry Tandau alisema kuwa tuzo hiyo imetokana na utendaji bora na
jitihada za Bayi katika riadha, hasa kuvunja rekodi hiyo, ambayo sasa itadumu
hadi mwaka 2022.
No comments:
Post a Comment