Na Mwandishi
Wetu
KOCHA mpya wa
Yanga, Mwinyi Zahera (pichani) kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) amewapa
mbinu wachezaji wa timu hiyo ili kuwafunga mahasimu wao wa jadi, Simba, katika
mchezo utakaofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Mchezo huu
unakuja wiki tatu tangu klabu hiyo ikimbiwe na aliyekuwa kocha wake, Mzambia
George Lwandamina aliyerejea kwao ikielezwa kujiunga tena na Zesco United ya
huko.
Na baada ya
waliokuwa wasaidizi wa Lwandamina kuiongoza timu katika mechi tatu bila
ushindi, ikitoa sare mbili zote za Ligi Kuu na zote 1-1 dhidi ya Singida United
na Mbeya City katikati ya kipigo cha 1-0 cha Wolaita Dicha nchini Ethiopia
katika Kombe la Shirikisho, uongozi umeleta kocha mpya.
Huyo ndiye
Zahera ambaye baada ya kufika kambini Morogoro alianza kwa kukutana na makocha
waliopo, Mzambia Noel Mwandila na wazawa Nsajigwa Shadrack na kocha wa makipa,
Juma Pondamali.
Habari kutoka
kwenye kambi hiyo ya Yanga zimesema kwamba Zahera amepata fursa ya kuitazama
Yanga inavyocheza katika mechi zake kadhaa zilizopita na kuwatazama pia Simba
kabla ya kuingia mazoezini kutoa mbinu zake kusaidia maandalizi ya pambano
dhidi ya watani Jumapili.
Zahera
hatakaa benchi Jumapili na kimsingi ataanza kazi rasmi kwenye mechi za makundi
Kombe la Shirikisho, Yanga ikianzia ugenini dhidi ya USMA Alger Mei 7, mwaka
huu mjini Algiers, Algeria.
Simba ambayo
inafundishwa na kocha Mfaransa, Pierre Lechantre anayesaidiwa na Mtunisia,
Aymen Mohamed Hbibi, Mrundi, Masoud Juma na mzawa Muharami Mohamed ‘Shilton’, inaongoza
Ligi Kuu ikiwa na pointi 59 baada ya kucheza mechi 25, wakati Yanga inafuatia
kwa nyuma kidogo wakiwa na pointi 48 baada ya kuingia uwanjani mara 23.
Yanga
inazidiwa pointi 11 na Simba SC na ina viporo viwili, maana yake ili kutetea
ubingwa wao, itabidi washinde Jumapili na washinde mechi zao zote zilizobaki za
Ligi Kuu, huku wakiwaombea mahasimu wao hao wapoteze mechi nyingine pia moja,
jambo ambalo sio rahisi.
No comments:
Post a Comment